“Ninyi mu wasaliti na wezi; nimekusudia kuwang’oa na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu nitawang’oa. Kama watu wangelikuwa wanajua dhuluma kali iliyopo kwenye mifumo yetu ya kifedha na kibenki, basi kungelikuwa na mapinduzi kabla ya asubuhi.”
Andrew Jackson, Rais wa Marekani; akiwahutubia wajumbe wa Benki waliokwenda kuomba aidhinishe kuendelea kuwapo kwa Benki Kuu nchini – 1832.
“Mfumo wetu wa fedha ndivyo ulivyo; kama madeni yasingekuwapo kwenye mfumo wetu wa fedha, kusingekuwapo na fedha yoyote.”
Marriner S. Eccles, aliyekuwa Mwenyekiti, Bodi ya Federal Reserve Bank – 1935-1948.
Ukweli wa kauli iliyo kwenye nukuu ya kwanza ya hapo juu upo hai karibu katika kila nchi leo. Rais wa saba wa Marekani, Andrew Jackson, alikuwa anawahutubia wajumbe wa Benki waliokwenda kuomba aidhinishe kuendelea kuwapo kwa iliyokuwa Benki Kuu ya nchi hiyo, wakati mkataba wake ulipokuwa unakaribia kwisha.
Andrew Jackson alikataa katakata; na kaulimbiu yake kwenye uchaguzi mkuu wa awamu yake ya pili ilikuwa ni: Jackson na Hakuna Benki – “Jackson and No Bank”. Alishinda kwa kishindo. Hadi leo Jackson ndiye Rais pekee aliyewahi kulipa deni lote la taifa la Marekani; ni Rais pekee aliyewahi kuua Benki Kuu ya nchi hiyo.
Na hii nukuu ya pili kadhalika, ingawa Marriner Eccles alikuwa Mmarekani lakini hiyo “mfumo wetu” inagusa mifumo iliyopo ulimwengu mzima – kwa sababu hivyo ndivyo ilivyo. Tafsiri ya anachosema Marriner Eccles ni kuwa: ingawa watu binafsi wakiwa hawana madeni ya kulipa wanabakiwa na fedha mifukoni mwao au kwenye akaunti zao za benki, lakini kama makampuni na mataifa yote pamoja na watu binafsi wote wasipokuwa na madeni ya kulipa, ulimwengu utakaukiwa na fedha. Hakutakuwa na senti hata moja mwenye mzunguko (in circulation).
Kwa mujibu wa ukweli huu, viongozi wanaposema ‘tufunge mikanda ili tumalize kulipa madeni ya taifa’, huwa hawasemi kweli kwa sababu watakuwa wanafahamu kuwa chini ya mfumo unaotawala ulimwengu hivi sasa, kuwapo kwa fedha yoyote kunatokana na ulazima wa kuwapo kwa madeni.
Katika makala hii ninajadili hili suala la uzalishaji wa fedha (money creation) unaotegemea kuwapo kwa madeni pamoja na utamaduni wa kuwa na taasisi za benki kuu zenye majina yanayofanya zionekane kama za kitaifa lakini si mali ya taifa; na jinsi ambavyo mifumo ya kifedha imekuwa ni kiini cha kuzua madeni ya taifa duniani (national debts), madeni ambayo aghalabu hayalipiki na wala haikusudiwi yalipike; madeni yanayomfanya kila mja awe mtumwa kwa wanaomiliki mabenki tangu siku ya kuzaliwa hadi siku anaingizwa kaburini.
Mataifa, kama inavyotokea kwa watu binafsi, huwa yanajikuta mara nyingi yakilazimika kufanya matumizi yanayokwenda ng’ambo ya mapato, yaani matumizi ya nakisi (deficit spending) kwa lugha ya Kiingereza. Mtu binafsi hili linapomtokea huwa anakwenda kukopa ama kwa ndugu na marafiki au mwajiri wake. Lakini wale ambao bahati inakuwa bahili kwao wanaweza kujikuta kwenye mikono ya watu wanaoitwa mapapa wa mikopo (loan sharks).
Kwa mataifa huwa ni tofauti; hili linapotokea nchi zina njia kuu mbili za kukabiliana nalo, nazo ni: kuzalisha fedha kwa njia ya karadha, kwanza, kupitia benki kuu; na ya pili, kupitia mabenki ya biashara.
(a) Benki kuu ndizo zinazozalisha fedha wanazoziita, kibenki, fedha za msingi au ‘base money (physical currency)’; yaani sarafu na noti zote ambazo Benki kuu zinachapisha baada ya kupokea bondi kutoka serikalini halafu inaikopesha hizo fedha serikali hiyo hiyo tena kwa riba. Na fedha hizi kawaida huwa asilimia tatu (3%) ya fedha zote zinazokuwa kwenye mzunguko katika taifa na kwa mwendelezo duniani.
(b) Njia ya pili ni kupitia mabenki ya biashara kwa kununua na kuuza dhamana za hazina au bondi – madeni ya taifa; pamoja na mfumo wa kuhifadhi sehemu tu ya akiba ya benki na kukopesha nyingine zote kwa watu binafsi, makampuni na mataifa kwa mbinu iitwayo ‘fractional reserve banking’. Lakini hili sitaligusia leo.
Fedha zitokanazo na mabenki ya biashara zinaiitwa ‘broad money’ yaani fedha katika tafsiri pana au kwa tafsiri yake, kwani vinginevyo isingestahili ziitwe fedha kwa sababu si chochote bali tarakimu tu kwenye makompyuta. Pamoja na hili, asilimia tisini na saba (97%) ya fedha katika nchi na dunia kwa ujumla huwa zinazalishwa kwa njia hii na zipo katika muundo huu.
Mchakato wa uzalishaji fedha unaanza wakati Serikali inapoielekeza Wizara ya Fedha ichapishe vitu vinavyoitwa hati za dhamana au bondi (treasury bonds), bili za hazina na noti za hazina (treasury bills & treasury notes) na kuzipeleka benki kuu ya taifa husika. Mabenki haya yanakwenda kwa majina tofauti katika nchi mbalimbali ulimwenguni lakini asili na kazi zao ni moja.
Mathalani, Uingereza inaitwa Benki ya England (Bank of England), Marekani wanaita Mfumo wa Shirikisho la Benki za Hifadhi (Federal Reserve System), zipo benki 12 kwenye hii klabu. Halafu zipo Benki Kuu ya Japan, Benki Kuu ya China, Benki Kuu ya Urusi, Benki Kuu ya Afrika Kusini, Benki Kuu ya Kenya, Benki Kuu ya Nigeria; Tanzania inaitwa Benki Kuu ya Tanzania (The Bank of Tanzania) na kadhalika.
Jambo la muhimu la kukumbuka ni kwamba hizi benki pamoja nyinginezo za aina yake duniani, ni makampuni binafsi na si mashirika ya umma au idara za serikali. Yamkini hivi sasa kuna nchi tano tu duniani zenye benki kuu za taifa ambazo ni mali ya umma, nazo ni: Korea ya Kaskazini, Iran, Cuba, Sudani ya Kaskazini na Syria.
Hii nchi ya mwisho kutajwa ni kwa muda gani itaendelea kuwapo kwenye orodha hii ni jambo ambalo haliwezi kutabirika kwa usahihi wowote, hasa tukizingatia kuwa nchi kama Afghanistan, Iraq na Libya zote zilikuwa na benki kuu ambazo ni mali ya taifa kabla hawajafunguliwa makopo ya ‘demokrasia’ kwa mtutu wa bunduki kama ambavyo inajiri huko Syria hivi sasa.
Hizi bondi au dhamana za serikali (government securities) zinachosema ni kwamba: ‘Nikopeshe fedha kiasi kadhaa (shilingi labda milioni moja) na baada ya miaka kadhaa fedha hizi zitalipwa pamoja na faida’. Kwa kawaida bondi huwa ni za muda mrefu, yaani zinatakiwa zilipwe (au ziwe zimepevuka, kwa lugha ya kibenki) baada ya miaka kati ya kumi hadi 30; wakati ‘treasury bills & treasury notes’ huwa ni za mihula ya miezi mitatu, sita au miaka kati ya miwili, mitano, saba hadi kumi, kitu ambacho si tofauti ni kimoja – zote hizi ni ala za madeni (instrument of debt), deni ambalo litalipwa na wewe na mimi kupitia kodi ya mapato.
Katika vitabu vya uhasibu au uchumi wakati mwingine hizi hati za dhamana zinaitwa IOUs (I owe you) yaani serikali inaziambia benki na makampuni yanayonunua haya madeni ya taifa kuwa: “unanidai na hati hii ndiyo risiti ya deni langu kwako.”
Suala jingine la kuzingatia katika hatua hii ni kwamba kwa kuwa fedha zote katika nchi zinazalishwa na benki kuu pamoja na benki za biashara; mataifa ambayo hayana benki kuu ambazo ni mali ya umma, basi serikali zao huwa zimejitoa kwenye mchakato mzima wa uzalishaji na udhibiti wa fedha nchini. Waasisi wa taifa la Marekani (founding fathers) waliliona hili ndiyo sababu wakaweka kwenye katiba yao (ibara ya kwanza kifungu cha 5) kuwa Bunge (Congress) ndilo litakalokuwa na mamlaka ya kudhibiti uzalishaji (issuance) na ugawaji (supply) wa fedha inchini. Jinsi gani hicho ni kinyume cha mambo yalivyo huko Marekani leo hii, naliweka nje ya makala hii.
Deni hewa lisilolipika
Baada ya kupokea hii IOU (bond) kutoka hazina, benki kuu huwa inafungua mtambo wake na kuchapisha kiasi kilichoombwa. Lakini kabla ya makabidhiano, benki kuu inadai si tu taifa kusaini mkataba wa kulipa hili deni pamoja na faida ya asilimia sita (6%) ya thamani ya kila noti (ambayo gharama yake ya kuichapisha ilikuwa senti tatu na nusu tu kwa kila noti); bali pia inataka dhamana au hakikisho (guarantee) ya jinsi gani serikali itazilipa hizi fedha, ikizingaitiwa kwamba serikali si mradi wa kibiashara. Jawabu la Serikali huwa ni kuweka poni (collateral) wananchi wake kwa kuidhinisha benki kuu kutoza kodi ya mapato (income tax) kwa kila mmoja wa raia wake ili kulilipa deni hili.
Hati za dhamana ndiyo deni lenyewe la taifa; halafu ikumbukwe kuwa ni serikali inayotoa leseni kwa benki kuu binafsi ya kuchapisha fedha halafu inaikopesha hizo fedha serikali hiyo hiyo kwa riba; wakati serikali ingeweza kuifanya hiyo kazi yenyewe bila kujiingiza katika madeni au kulazimika kutoza kodi watu wake (ambao ni maskini mno kulinganisha na wenye benki kuu) ambao hizo fedha wanapelekewa.
Wakati umefika wa kuwauliza viongozi duniani “kwa nini mnakuwa wasaliti wa watu na nchi zenu? Au ndiyo hizo hongo zinazotoka benki kuu zinawatoa utu na ubinadamu wenu?
Baadhi ya nchi, wizara ya fedha huwa inakabidhiwa jukumu la kukusanya hizi kodi za mapato kwa niaba ya benki kuu; wakati nchi kama Marekani wameunda idara maalum (ambayo nayo si sehemu ya serikali) inayokusanya kodi ya mapato wanayoiita Huduma ya Mapato ya Ndani (Internal Revenue Service-IRS).
Nchini Tanzania, wana Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambayo ni sehemu ya Serikali, lakini inatumikishwa tu bure na Benki Kuu kama raia wa ulimwengu wanavyotumikishwa kila mwaka na benki kuu zao.
Hivyo basi, ukweli ambao watu wengi katika nchi nyingi hawaufahamu ni kwamba fedha zote za kodi ya mapato hakuna hata senti moja inayokwenda kwenye gharama za kuendesha nchi. Haziendi kulipa mishahara ya watumishi wa umma (madaktari na manesi, wanajeshi na askari polisi, walimu na kadhalika); hazijengi mabarabara, madaraja, mashule wala mahospitali; haziendi kujenga na kuendesha maktaba za taifa; bali fedha hizo zote zinakwenda kulipa deni la benki kuu ambayo ni kampuni binafsi kwa asilimia zote.
Namna nyingine ya kuliangalia hili suala ni kwamba watu wote katika nchi wanalazimika kutumia theluthi moja ya mapato ya jasho lao, kiasi ambacho ni sawa na kazi ya miezi mitatu kila mwaka kwenye hii kodi ya mapato; fedha zinazokwenda kuongeza utajiri wa taasisi yenye utajiri wa kutisha – benki kuu; benki isiyo na tija yoyote kwao na ni kampuni ambayo haina umuhimu hata chembe katika shughuli za kuendesha taifa lolote duniani; kwani hakuna kitu chochote benki kuu inachofanya ambacho kisingewezekana kufanywa na wizara za fedha.
Laiti serikali ingelichapisha yenyewe hizi noti, deni hili la taifa lisingelikuwapo; laiti serikali ingelichapisha yenyewe hizi noti, ulipaji wa riba kwa benki kuu ungelitoweka. Mtu mwenye fikra hakosi kujiuliza ni nani anayefanywa bwege kwenye utaratibu huu mzima, je, huu tuuite ujinga au ni upumbavu ama ni woga na ubinafsi?
Tanzania, mathalani, enzi ambazo kitabu kilikuwa ni fumbo kali kwa watu wengi; kanuni ya kuwalazimisha wananchi kwenda kulima kwenye mashamba ya wakoloni bila ijara ni moja ya sababu kuu zilizosababisha Vita ya Majimaji (1905-1907) wakati Tanzania Bara ilipokuwa chini ya ukoloni wa Kijerumani.
Tatizo aina hiyohiyo pia lilichangia mlipuko wa Vita ya Mau Mau nchini Kenya ilipokuwa chini ya ukoloni wa Kiingereza. Kadhalika, Wakenya waliokuwa wengi zama hizo walikuwa hawajui kusoma wala kuandika. Jambo la kushangaza ni kuwa leo pamoja na uhuru na maendeleo makubwa ya elimu, bado mja anafanywa mtumwa lakini hakuna hata dalili dhaifu ya kuonesha kuwa anatambua kuwa yupo utumwani! Tena huu ndiyo ukweli si kwa Tanzania na Kenya pekee bali karibu dunia nzima. Kweli, huyo aliyebuni hii mbinu alikuwa na akili na uwezo wa mchwa.
Inasemekana kwamba mwasisi wa huu mfumo alipata kuhojiwa na mmoja wa watu wake wa karibu, kwamba hivi huu utapeli utakapogundulika wananchi na mapanga mikononi hawatasaka wenye haya mabenki kila kona? Jibu lake lilikuwa hili: labda mtu mmoja kati ya milioni atagundua na hao wachache watakaogundua watakuwa wanafaidika kiasi cha kutokuwa na motisha ya kufanya mabadiliko; hadi muda huu jibu lake linaonekana kuwa ni kuntu.
Baada ya benki kuu kupokea bondi kutoka hazina ya kuomba kuchapishiwa shilingi milioni, moja kwa mfano; basi mtambo unafunguliwa na kuchapisha kiasi cha fedha zilizohitajiwa. Lakini benki inatoza riba ya asilimia sita (6%) ya hii milioni moja; ndiyo kusema baada ya makabidhiano, vitabu vitaonesha kuwa hazina imepokea Sh. 1,000,000/- + Sh. 60,000/- (za riba) jumla Sh. 1,060,000/-; na leja za benki kuu pia zitaonesha zimekabidhi hizo shilingi milioni moja na elfu sitini. Hili ndiyo linalokuwa deni letu la taifa kwa sasa.
Lakini hali halisi ni kuwa benki ilichapisha sh.1,000,000/- peke yake na ndizo zilizopokewa na hazina, hii ina maana kwamba hizi sh. 60,000/- ambazo zipo na zitaendelea kuzaa faida (kwa mujibu wa vitabu vyote vya mahesabu ya hazina na benki kuu) kiukweli hazipo, hazikupata kuwapo na wala hazitakuwapo.
Hivyo basi, katika mazingira hayo, hili deni ni la kughushi, deni hewa; kibaya zaidi hata kama serikali itakuwa na nia njema kabisa ya kuzilipa hizi Sh. 60,000/-, haitawezekana kwa sababu hela zenyewe hazipo kabisa katika mzunguko (circulation) kwani hazikuzalishwa.
Watu wanaweza kujisaili kwa nini serikali isipeleke tena huko benki kuu bondi ya Sh. 60,000/- kwa ajili ya kulipa hilo deni la faida? Huo hauwezi kuwa ufumbuzi wa tatizo lililopo; hazina ikipeleka bondi nyingine ya Sh 60,000/- itabidi zichapishwe upya, na litakuwa ni deni jipya litakalozaa riba ya asilimia sita ambayo ni Sh. 3,600/- na ambazo tena hazitakuwa zimezalishwa, na kama kawaida ya mfumo huu zitaingizwa upya kwenye mabuku ya hesabu kama ilivyotokea kwenye huo mfano wa milioni moja wa hapo juu.
Na kuwahadaa wananchi zaidi, haya madeni yanaposhindikana kulipwa kama ilivyokusudiwa, si kwa ukosefu wa dhamira ya kulipa bali kwa sababu ya jinsi madeni yenyewe yalivyosukwa; hawa ‘manyang’au’ wanaomiliki haya mabenki wamediriki kwenda kwenye nchi zenye kushindwa kulipa madeni yao na masharti ya ukatili wa kinyama kabisa (structural adjustment programmes-SAPs) ambayo matokeo yake ni hizo nchi kunyang’anywa mali zao kwa kuwalazimisha kuuzia wageni kwa bei ya chee rasilimali zenye thamani kubwa sana – ardhi na maji, madini, mashirika ya umma. Utapeli huu unapakwa rangi maridhawa na kunadiwa kama soko huria na utandawazi.
Matokeo mengine ya hizi SAPs ni kuzilazimisha serikali zifute misaada yote inayotolewa kwa wananchi kupitia elimu na matibabu bure, misaada ya pembejeo kwa wakulima na kadhalika. Idadi ya watu waliokufa kwa magonjwa yanayotibika kwa sababu hawakuwa na fedha za kulipia matibabu yao, tangu huu unyama wa SAPs upitishwe ni kubwa mno. Inapofikia hapo, huu tena hauwi ni wizi tu wa kimachomacho bali uuaji; na tukizingatia kuwa kinachodaiwa chenyewe kilikuwa ni fedha na madeni ya kugushi (hewa); basi huu ni ujambazi wa kisiasa na kiuchumi (political and economic banditry).
Hadi sasa nimegusia upeo wa kwanza wa uhewa wa madeni ya taifa. Upeo wa pili ni huu ufuatao: Hizi pesa za makaratasi au noti (fiat currency) hazitegemezwi kwenye kitu chochote chenye thamani kama vile dhahabu au fedha (silver).
Ndiyo kusema thamani ya noti inatokana, kwanza, na amri ya serikali ya nchi husika inayosema hii ni ‘fedha halali kwa malipo ya shilingi X’ yaani legal tender. Pili, ni imani ambayo wananchi wanakuwa nayo kwenye kauli hiyo ya serikali yao; zaidi ya hapo hiyo noti iliyo mfukoni mwako au benki ni karatasi ambayo si chochote wala lolote.
Aidha, hizo fedha za makaratasi jinsi ambavyo zimepewa thamani hakuna tofauti na mazingaombwe au kiinimacho – kitu ambacho uwepo wake haupo – kwa Kiingereza wanasema ‘conjuring currency out of thin air’.
Kadhalika, uamuzi wa kuipa benki kuu ukiritimba (monopoly) wa kuchapisha fedha nao haitegemezwi kwenye sababu yoyote yenye uzito na ujazo. Sasa iwapo hela yenyewe imekuwa ‘conjured’ kimuujiza, yaani ni bandia, itawezekanaje deni linalotokana na hela hiyo liepuke damu (DNA) ya kukosa uhalali kwa maana ya kuwa ‘deni hewa?’
Hali hii itatofautiana vipi na mwizi, mathalani, anayekwenda mahakamani na kusema: “Namshitaki huyu mtu hataki kunilipa fedha nilizomkopesha; fedha ambazo nilichapisha mwenyewe – za bandia.” Ni yupi hapo mwenye hatia zaidi – huyu mwenye kutengeneza fedha feki au huyu mwenye kudaiwa hizo fedha? Hivyo basi, hizi fedha za makaratasi pamoja na madeni ya taifa yatokanayo na fedha hizi ni ngano za kisheria legal fiction na jaribio la kumaliza kulipa madeni ya taifa katika mfumo wa kifedha na kibenki tulionao, hakuna tofauti na kitendo cha mtu kukifukuza kivuli chake mwenyewe – ni ukichaa.
Makala ijayo nitachambua jinsi mabenki ya biashara yanavyozalisha asilimia 97 ya fedha zinazokuwapo katika mzunguko.
Harid Mkali ni Author & Journalist, anaishi London, Uingereza. Simu: +447979881555, barua pepe: [email protected], tovuti: www.haridmkali.com