Madaraka Nyerere ni mmoja kati ya watoto wanane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tangu kifo cha Mwalimu, amekuwa akiishi Butiama akiwa Mratibu wa asasi ya kijamii ya Butiama Cultural Tourism Enterprise (BCTE) inayotangaza Butiama kama kivutio cha kihistoria na kiutamaduni kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania .
Jana, tarehe 14 Oktoba 2013, tumetimiza miaka 14 tangu kufariki Mwalimu Julius Nyerere, kiongozi wa kwanza wa Tanganyika huru, na baadaye Tanzania.
Tangu kufariki kwake na kila tunapoadhimisha siku aliyofariki kunaibuka mjadala mkubwa kuhusu uongozi ikizingatiwa kuwa Mwalimu Nyerere bado anaheshimika kama aliyekuwa muadilifu, na ambaye aliweka masilahi ya Taifa mbele. Uadilifu huu unatokana na sera alizoziasisi zilizotanguliza umuhimu wa walio wengi kufaidika na rasilimali na maendeleo kwa jumla, lakini pia katika mwenendo wake wa uongozi.
Ukweli unabaki kuwa kiongozi anaweza kuwa na sera zinazohitaji masilahi ya Taifa na masilahi ya wengi, lakini bado akawa ni mfano mbovu kabisa wa uadilifu na mtu anayetanguliza masilahi yake binafsi na kuacha mahitaji ya wengi yakitapatapa kwenye mawimbi na kina cha bahari yakitafuta pa kuhemea.
Imekuwa desturi tangu kufariki kwake kutafakari maisha ya utumishi wa Mwalimu Nyerere kwa umma kila tunapoadhimisha kifo chake. Na mimi naona sina budi kufanya hivyo, haswa kwa kuzingatia kuwa mawazo yanayotolewa na kila mmoja wetu yanaweza kuchangia mjadala kuhusu changamoto za kisiasa na kijamii ambazo nchi yetu na watu wake wanakabiliana nazo sasa na wakati huo huo kuchangia mawazo kuhusu namna ya kukabiliana na baadhi ya changamoto hizo.
Uamuzi wa kuzikwa Butiama
Mwalimu Nyerere tunamkumbuka kama mtu ambaye alikuwa na misimamo thabiti. Alifanya uamuzi kwa kufanya tafakari za kina na siyo kwa masuala makubwa tu yaliyokabili Taifa, bali hata kwa uamuzi ambao ulihusu maisha yake binafsi.
Wakati akiugua saratani ya damu, Mwalimu Nyerere aliarifiwa na daktari wake kuwa, kwa kawaida ya magonjwa ya aina hiyo, jitihada za tiba hufikia kikomo na hatimaye hazisaidii katika kurefusha maisha ya mgonjwa.
Alipopewa hii taarifa Mwalimu Nyerere alitoa maagizo ni wapi angetaka azikwe na kuonesha sehemu alipozaliwa kwenye eneo la Mwitongo, kijijini Butiama. Ni sehemu ambako alikulia kabla hajaanza kusoma akiwa na umri wa miaka 14. Mwitongo ndipo sehemu aliyoifahamu katika hatua za kwanza za maisha yake, akiwa mmoja wa watoto wa Mtemi Nyerere Burito aliyeongoza kabila la Wazanaki wa eneo la Butiama, na ambaye alikuwa na wake 22. Mama yake Mwalimu, Mgaya wa Nyang’ombe, alikuwa ni mke wa tano wa Nyerere Burito.
Ulizuka mjadala baada ya kifo chake kwa baadhi ya Watanzania ambao walipenda Mwalimu Nyerere azikwe eneo la Tanzania tofauti na Butiama. Baadhi walitaja Dar es Salaam wakati wengine walipendekeza Dodoma, na hoja ilikuwa maeneo hayo yangewezesha Watanzania wengi zaidi kuweza kuzuru kaburi lake. Butiama iko pembezoni kwa Watanzania wengi na siyo rahisi kufika huko.
Wengi wetu hutafakari sababu ambayo ilimshawishi Mwalimu kuzikwa Butiama na tunaamini kuwa ulikuwa ni uamuzi sahihi. Kuna mijadala mikali ambayo huzuka nchini Zimbabwe mara anapofariki kiongozi na unapochukuliwa uamuzi wa, ama kukubali, au kukataa asizikwe kwenye eneo ambalo linaitwa Heroes Acre; eneo ambalo limetengwa kwa madhumuni ya kuzika mashujaa wa Zimbabwe. Uamuzi wa nani ni shujaa unafanywa na Kamati Kuu ya chama cha Zanu-PF, chama ambacho kimeongoza Serikali ya Zimbabwe tangu kupatikana Uhuru wao mwaka 1980. Baadhi ya watu wanalalamikia uamuzi huo. Wanasema unapendelea zaidi wale waliokiunga mkono chama hicho.
Inawezekana kuwa wazo la kumzika Mwalimu sehemu nyingine zaidi ya Butiama lingeibua mijadala ya aina hiyo na badala ya kumfanya apumzike kwa amani, lingekuwa linamhagaisha huko aliko. Tayari kuna makundi ya watu yanayodai kuwa mchango wake katika kuleta Uhuru wa Tanganyika ulikuwa ni mdogo kuliko historia inavyoeleza na inawezekana kuwa makundi ya aina hiyo yangezua mjadala mkubwa kuhusu kuwapo nchini Tanzania kwa eneo maalumu la kuzikwa viongozi wa kitaifa.
Uamuzi wake wa kuzikwa Butiama unafanana na uamuzi wake wa kurudi Butiama baada ya kustaafu mwaka 1985 na kijiendeleza na shughuli za kilimo. Kwa hakika, kwa yeye Butiama ni nyumbani, katika uhai na katika kifo chake; na hili linadhihirishwa na uamuzi wake wa kuzikwa alikozaliwa.
Uamuzi wangu wa kuishi Butiama
Baada ya Mwalimu kuzikwa Butiama mnamo Oktoba 23, 1999 mimi nilichukua uamuzi wa kubaki Butiama na nimekuwa nikiishi huko tangu wakati huo.
Kwangu ilikuwa rahisi kuchukua uamuzi wa kuhamia Butiama kwa sababu familia yangu ilikuwa nje ya nchi, na nilidhani kuwa ilikuwa muhimu kwa mmoja wetu, yaani mmoja wa watoto wake, aweze kuwa karibu na Mama Maria. Kwa hiyo nikabaki hapa baada ya mazishi ya Mwalimu ingawa haukuwa uamuzi rahisi kuutekeleza.
Unapokuwa na mazoea ya kuishi Dar es Salaam inakuwa vigumu sana kuishi sehemu nyingine ya Tanzania; na kwa kweli mwanzoni nilikuwa najikuta nikisafiri mara kwa mara kwenda Dar es Salaam, lakini sasa hivi nimeshazoea kuishi Butiama na hufika Dar es Salaam mara moja moja.
Tofauti ya sasa na wakati Mwalimu akiwa hai
Ni dhahiri kuwa, kwa kawaida, kuondokewa na kiongozi wa familia kunaacha pengo kwa familia na haikuwa tofauti kwa familia ya Mwalimu Nyerere. Lakini labda tushukuru kuwa mwanadamu ameumbwa kukabili mabadiliko yanayoandama maisha yake. Kadiri miaka inavyozidi kupita, hali ya kukosekana kwa kiongozi wa familia inajisawazisha yenyewe na unaibuka uhusiano mpya ambao unaakisi hiyo hali mpya.
Siwezi kusema familia yake imezoea kutokuwapo kwa Mwalimu, lakini labda ni sahihi tu kusema kuwa maisha yanaendelea kwa kadiri ya wale waliopo wanavyoyasukuma, kila mmoja akiwa anachangia anavyoweza majukumu yake ya kifamilia.
Lakini naweza kukiri kuwa yeye alituunganisha kama familia, na kutokuwapo kwake kunasababisha kuibuka kwa matawi yake ambayo kila moja linatafuta nafasi yake katika ulimwengu huu na katika maisha kwa jumla. Sisemi kuwa kufariki kwake hakujatutenganisha kama familia, ila kuondoka kwake ni hatua tu ambayo familia nyingi zinapitia. Yeye mwenyewe alikabiliana na hali hiyo baba yake alipofariki dunia mwaka 1942 na kuanza kuchukua dhima ya kusimama mwenyewe na kuunda familia yake miaka kumi baadaye; na sisi pia tunapitia mzunguko wa aina hiyo kama sehemu ya kukabiliana na mabadiliko.
Nakumbuka maneno ya Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru, tuliyekuwa naye London siku Mwalimu alipofariki dunia. Aliniambia mimi na kaka yangu Makongoro kuwa kifo cha Mwalimu kinatufanya sisi sasa kuwa watu wazima kwa sababu tunabeba majukumu ambayo hatukuwa nayo hapo awali. Alisema, “Watu walipofika nyumbani walikuwa wanamuulizia Mwalimu. Lakini leo hii wakifika nyumbani watakuulizia Madaraka au Makongoro.” Na wengine, ambao hakuwataja Mzee Kingunge.
Maisha yake wakati wa uongozi
Mwalimu alikuwa ni mtu aliyefuata ratiba kwa umakini mkubwa. Baadhi ya walinzi wake wa zamani wanakumbuka kuwa akiambiwa ratiba inaanza saa fulani, basi kama ni safari kwa hakika atakuwa tayari kuondoka saa ile ile bila kupoteza dakika.
Alikuwa na desturi ya kila siku kuamka mapema sana, kusikiliza taarifa za habari za nje ya nchi na za nchini pia za Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ya wakati ule. Alitumia muda pia kufanya mazoezi ya viungo na alihudhuria ibada kila siku kabla ya kuelekea kazini Ikulu, wakati huo tukiwa tumehamia kwenye makazi yake yaliyopo eneo la Msasani ambalo siku hizi linaitwa Mikocheni.
Kuna baadhi ya wageni walifika Msasani kumuona, lakini wengi waliishia Ikulu. Ofisi yake ya Msasani ilikuwa kwenye ghorofa ya chini na huko ndiko alipoonana na wageni, au kwenye sebule iliyopo ghorofa ya chini.
Kwenye ghrofa ya juu ilikuwa sebule ya juu, na chumba chake cha kulala. Alipohamia sebule ya juu tulitambua kuwa shughuli zake za kikazi zilikuwa zimeisha na huko tulipata fursa ya kuongea naye kama mzazi na mwanafamilia.
Kwa kawaida yake hakupenda kuchanganya familia yake na shughuli zake za kikazi. Kwa hiyo ilikuwa ni nadra sana kwa wageni wake kufika kwenye ghorofa ya juu na kuonana na wanafamilia au wanafamilia kuteremka chini na kuchanganyika na wageni wake rasmi.
Mara chache ambapo aliamua kutuita chini kuonana na wageni wake ni alipofika Rais mstaafu wa Zambia, Dk. Kenneth Kaunda. Mgeni mwingine ambaye tulionana naye alikuwa Rais wa India wa nyakati zilizopita ambaye sikumbuki jina lake. Aidha, alipompokea Malkia Beatrice wa Uholanzi, akiwa katika ziara rasmi nchini, Mwalimu alituita Ikulu kukutana naye na familia yake.
Ratiba ya Mwalimu Nyerere alipokuwa Butiama inaweza kugawanywa katika vipindi viwili; alipokuwa Rais wa Tanzania na alipostaafu uongozi wa nchi.
Akiwa Rais, Mwalimu Nyerere aliweka utaratibu wa kusafiri kwenda Butiama kwenye mapumziko kila mwisho wa mwaka. Lakini ingawa alikuwa huko kwa mapumziko alitumia muda mrefu wa likizo yake akujishughulisha na kilimo kwa kushirikiana na wanakijiji wengine.
Pamoja na kuwa mapumzikoni, kwa kuwa alikuwa kiongozi wa nchi, basi ilikuwa kawaida kwa watu mbalimbali wenye matatizo kufika kumuona ili kuomba awasaidie kutatua hayo matatizo.
Alipotoka shambani na katika muda wake wa mapumziko alitumia muda mrefu kujisomea baadhi ya vitabu vyake. Alipofariki mwaka 1999 aliacha maktaba ya vitabu vyake zaidi ya 8,000 ambavyo karibia vyote aliweza kuvisoma. Hivi ni vitabu alivyoanza kuvikusanya alipoanza kusoma katika ngazi ya chuo, lakini pia kuna vitabu ambavyo aliendelea kununua au alivyozawadiwa na waandishi tofauti wa vitabu, au watu mbalimbali ambao walimtumia vitabu ambavyo waliamini angependa kusoma.
Katika kipindi cha kustaafu kwake akiwa Butiama aliendelea kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na akawa pia na wadhifa wa Mwenyekiti wa Tume ya Kusini na msuluhishi wa mazungumzo ya amani ya Burundi. Kwa sababu ya kazi hizi, majukumu yake yalihusisha kufika Butiama kwa baadhi ya wageni ambao walihusika na kazi za Tume ya Kusini, pamoja na usuluhishi wa Burundi.
Kuna wageni kutoka maeneo mbalimbali ya dunia na Bara la Afrika ambao pia walifika Butiama kuonana naye kwa masuala mbalimbali. Kuna mmiliki mmoja wa hoteli ya mjini Musoma anayekumbuka kumuona kwenye hoteli yake marehemu Laurent Kabila, kabla ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, akiwa hotelini mjini Musoma kwake kwa siku kadhaa akisubiri kuelekea Butiama kuonana na Mwalimu Nyerere. Wageni wa aina hii ni wengi ambao walifika Butiama kuonana na Mwalimu Nyerere.
Mwalimu kama mzazi na kiongozi wa familia
Kama ambavyo naamini ni hali ya kawaida katika familia yoyote, Mwalimu akiwa kama baba na kiongozi wa familia, alikuwa na upendo wa kawaida tu kwa familia yake. Kwenye familia za Kibantu, tofauti na katika jamii nyingine, hatuwezi kuzungumzia matukio mahususi ambayo yanamtanabahisha mzazi kuonesha mapenzi kwa familia yake. Sisi tunaamini kuwa alikuwa na mapenzi ya kawaida tu kwa familia yake.
Lakini tunakumbuka kwamba alikuwa ni mzazi ambaye alipenda kuunganisha ukoo wake kila ilipotokea fursa na aliacha msingi imara uliyounganisha ukoo wa baba na babu yake.
Mandhari ya Mwitongo
Nikizungumza kama mkazi wa Mwitongo na mdau wa shughuli za kupaendeleza Mwitongo kama eneo la kihistoria na la utamaduni wa kabila la Wazanaki, napenda kusema kuwa tunajitahidi kuweka vizuri mazingira ya eneo hilo ili lipendeze kama Mwalimu alivyokusudia kwa kuwa na mazingira yanayovutia.
Tunakusudia kuendeleza mradi wa upandaji miti ambao yeye aliuanzisha, lakini ambao hatujapata fursa ya kuuendeleza mpaka sasa. Changamoto kubwa ni kuwa baadhi ya wakazi wa Butiama huvamia huu msitu alioupanda na kukata miti bila idhini. Aidha, kuacha mipango hii, hakuna jitihada mahususi za kupanda miti katika eneo la Butiama.
Mwalimu na kilimo, changamoto za leo
Shughuli za kilimo alizoendeleza Mwalimu ni kama zimesimama kwa sasa na kuna wanafamilia wachache tu ambao wanajihusisha na kilimo, lakini kwa kiwango kidogo kulinganisha na kilimo alichoendesha Mwalimu.
Maeneo aliyolima Mwalimu yanavamiwa
Jambo moja ambalo linaathiri mipango ya muda mrefu ya kuendeleza kilimo ni kuwa baadhi ya yale maeneo ambayo Mwalimu Nyerere alikuwa analima hayakuwa maeneo yake binafsi, bali yalikuwa na mpaka sasa ni maeneo yaliyopo chini ya mamlaka ya Kijiji cha Butiama. Yeye aliazimwa tu na kijiji kulima. Na hata pale wapimaji kutoka serikalini walipoendesha upimaji maeneo hayo na kutaka kumpa miliki, alikataa na kusisitiza kuwa ni maeneo ya kijiji.
Hata hivyo, kuna taarifa kuwa, kwa kutambua kwamba hakuwa na ardhi, uongozi wa kijiji jirani cha Buturu ulimpa eneo Mwalimu Nyerere, lakini jambo la kushangaza ni kuwa baadhi ya viongozi wa hivi karibuni wa kijiji hicho wanasema hawakumbuki au hawana habari na hizo taarifa za kupewa ardhi Mwalimu Nyerere. Kusema hawakumbuki inawezekana kuwa ni kweli kwa sababu wengi wao wana umri mdogo na siyo rahisi kuwa na kumbukumbu hizo kichwani.
Kwa hiyo, kinachotokea sasa ni mmoja wa viongozi hao wa zamani kuendelea kukalia hilo eneo na kuligawa kwa kuwakodishia watu wengine.
Mwalimu Nyerere alipokuwa akiendesha shughuli za kilimo baadhi ya wasaidizi wake walikuwa wanalima kwenye eneo hilo ambalo sasa limeporwa, na wanathibitisha kuwa ni eneo ambalo Mwalimu Nyerere alipewa na Kijiji cha Buturu.
Ni dhahiri leo hii zikitoka taarifa kuwa familia ya Mwalimu Nyerere imenyang’anywa ardhi na kiongozi wa zamani wa Kijiji cha Buturu desturi ya siku hizi ni kuamini kuwa siku zote ni viongozi na familia zao ndiyo wanayo tabia ya kupora mali za wananchi. Ukweli unaweza kuthibitishwa, lakini kwa mlolongo mrefu ambao unamshuku zaidi yule mwenye jina kuliko yule ambaye hana jina.
Baadhi yetu ndani ya familia tunatambua kuwa suala hili lina athari kubwa za kisiasa. Mwalimu Nyerere asingekuwa kiongozi muadilifu, leo hii familia yake ingekuwa inamiliki ardhi hata yenye ukubwa wa Mkoa wa Mara!
Lakini unaanzaje kudai haki dhidi ya wahusika ambao wao wenyewe wana masilahi ndani ya shauri hilo hilo? Kwa maneno ya siku hizi tunaita kupeleka kesi ya kenge kwa mamba. Kwa mfano, mimi niliitwa kwenye kikao kimoja cha uongozi wa Kijiji cha Buturu na kuombwa nitoe uthibitisho wa umilikishwaji wa lile eneo kwa Mwalimu Nyerere. Ni kweli kuwa Kijiji cha Buturu kina kumbukumbu sahihi za uamuzi wake wote kwa miaka 25 au 30 iliyopita? Sidhani. Na iwapo wangekuwa wanazo, wangezitoa kweli hadharani wakati watu wale wale ambao wanashikilia hayo maeneo wako kwenye uongozi wa kijiji? Sidhani.
Eneo la Mwalimu Nyerere la Mwitongo linajulikana kwa mwenyeji yeyote wa Butiama kuwa ni eneo lake. Lakini ukiomba kupata nyaraka za kuthibitisha miliki hiyo ukweli ni kuwa hazipo. Lakini haibadilishi ukweli kuwa ni eneo la Mwalimu Nyerere. Serikali ya Kijiji cha Butiama inaweza kuthibitisha hilo kwa taarifa ambazo inaweza kuziandaa leo hii, lakini uwezekano wa serikali hiyo hiyo kufanya hivyo wakati baadhi ya viongozi wake wa hivi karibuni wana njama za kujitwalia maeneo hayo ya Mwitongo inakuwa vigumu. Hili ndilo tatizo lililopo Buturu sasa hivi, lakini ni kiashiria kizuri cha aina gani ya viongozi ambao tunao sasa hivi. Na haya kama yanamtokea Mwalimu Nyerere, basi hakuna kizingiti chochote cha kuathiri haki kwa mwananchi wa kawaida.
Kuna taarifa kuwa eneo lote hilo, lile la Kijiji cha Butiama na lile ambalo alipewa Mwalimu Nyerere, lina madini ya dhahabu kwa hiyo tatizo hapa linaweza kuwa ni dhahabu na siyo ardhi ya kulima.
Unaweza kuwa unafikiri unapambana na wanakijiji ambao wanatafuta eneo la kulima, kumbe ni suala pana zaidi ya hapo. Nimewahi kusikia taarifa ambazo siwezi kuthibitisha zinazosema kuwa kuna watu wanasubiri Mama Maria afariki ili waanze kuchimba hiyo dhahabu. Kufanya hivyo kwa sasa akiwa hai kunaweza kuibua changamoto za kisiasa ambao zitaleta matatizo badala ya neema.
Watanzania tunapenda sana kuongea, kwa hiyo haya ya kumtakia maisha mafupi Mama Maria yanaweza kuwa siyo ya kweli. Lakini kama ni ya kweli, na ukiongezea ukweli kuwa Mwalimu Nyerere ananyang’anywa ardhi ambayo alipewa, basi ujue maadili, hekima na busara ambavyo vilitawala enzi zake, leo hii vimetoweka na tumebaki na jamii na viongozi ambao wanatumia nafasi zao kujinufaisha kwanza na kuangalia masilahi ya wengine inapolazimika, lakini siyo kama madhumuni ya msingi ya uongozi.
Labda muhimu pia kugusia kuwa Mwalimu Nyerere alifahamu taarifa za kitafiti kuonesha kuwa hilo eneo linayo dhahabu, lakini nimeambiwa kuwa kauli aliyotoa ni kuwa suala la kilimo na uhakika wa chakula lilikuwa muhimu kuliko uchimbaji dhahabu.
Kwa maoni yangu ni kuwa eneo lote la Kijiji cha Butiama na Kijiji cha Buturu, libaki eneo la kumbukumbu chini ya Sheria ya Mambo ya Kale ili lilindwe dhidi ya miradi yoyote ya uchimbaji madini. Niliwahi kumsikia afisa mwandamizi wa kampuni ya Anglo Gold aliyetembelea Butiama akisema kuwa eneo hilo lina dhahabu, lakini siyo ya kiasi kikubwa sana kiasi cha kuibua nia ya kampuni kubwa kama Anglo Gold kukusudia kuchimba dhahabu pale. Ni dhahabu kidogo ambayo kampuni ndogondogo tu ndiyo zitaona kuwa ni mali, lakini siyo Anglo Gold.
Kwa maana nyingine, Serikali haiwezi kukosa mapato makubwa kwa kulitangaza lile eneo kama eneo maalumu la kumbukumbu kwa heshima ya Mwalimu Nyerere aliyelitumia kama eneo la kilimo akisisitiza umuhimu wa kilimo na uhakika wa chakula na akitahadharisha ukomo wa shughuli za uchimbaji madini.
Hata hivyo, kwa sera ambazo tunazo sasa hivi Serikali ilishajitoa kwenye shughuli zote za uchumi na kuacha nafasi kwa sekta binafsi kusimamia shughuli hizo. Kwa maana hiyo, mradi wowote wa uchimbaji dhahabu katika eneo la Mwibanza (yalipo mashamba ya Mwalimu) utatoa nafasi kwa watu wachache tu kunufaika na rasilimali hiyo na siyo umma wa Watanzania.
Kama uongozi wetu wa sasa na hata wa miaka ijayo unayo dhamira ya kweli ya kuthamini mchango wa Mwalimu Nyerere katika kuendeleza kilimo, basi hapa wanayo fursa nzuri ya kufanya hivyo. Labda Serikali inaweza kutoa nguvu, taaluma na mtaji kuonesha mfano mzuri wa utekelezaji wa Sera ya Kilimo Kwanza kwenye shamba hili.
Familia ya Mwalimu, uhusiano na Serikali
Pamoja na maneno yanayoashiria uhusiano mbaya kati ya familia ya Mwalimu Nyerere na Serikali, ukweli ni kuwa uhusiano ni mzuri. Jukumu la Serikali, kwa mujibu wa sheria, ni kutoa stahili kwa mjane wa Rais mstaafu, Mama Maria Nyerere. Na hilo jukumu inalifanya vizuri tu na hata wakati mwingine kwa kuvuka mipaka.
Tathimini ya enzi za Mwalimu na sasa
Hata hivyo, katika mtizamo mpana zaidi wa kitaifa tunaona kuwa kuna baadhi ya upungufu unaojitokeza tunapoadhimisha kifo cha Mwalimu Nyerere. Inakuwa vigumu kuepuka kulinganisha hali ya maadili, utaifa, uzalendo, uchumi wa kujitegemea, umoja na mshikamano vilivyopo sasa na wakati wa uhai wake.
Maadili
Inatosha tu kusema kuwa maadili ya kijamii na ya kisiasa yemeshuka kwa kiwango kikubwa sana. Unapoona mshiriki na mshindi wa Big Brother Africa ambaye akiwa ndani ya jengo la mashindano Afrika Kusini akifanya vitendo ambavyo kimaadili havifanyiki hadharani, anapopokewa kama shujaa anaporudi Tanzania, ujue kuna kasoro kubwa ndani ya jamii yetu.
Ukiona kuwa matumizi ya pesa kwenye uchaguzi wetu wa kutafuta uongozi yamekuwa ni jambo la kawaida na hayupo mtu wa kukemea hali hii kwa sababu wa kukemea nao wanazo kasoro zile zile ambazo zinahitaji kukemewa, basi ujue kuwa nchi imetumbukia ndani ya shimo la uchafu ambalo kihistoria tunaona linaweza kupata suluhisho kutoka kwenye mapinduzi tu kwa sababu tukio kama hilo linasafisha uozo wote na kuanza upya na maadili mapya.
Lakini taratibu zote za kidemokrasia zinapingana na taratibu za mapinduzi kwa hiyo suluhisho kwa kweli ni gumu sana. Ungefikiri kuwa suluhisho ni kufundisha kada mpya yenye maadili mapya, lakini unaweza kweli kuweka matumaini kwa mwalimu afundishe maadili mapya wakati mwalimu kamuuzia mzazi mtihani, na mwanafunzi anafahamu kuwa mzazi wake kamnunulia mtihani?
Kuporomoka kwa maadili nafikiri kuna chanzo fulani. Mimi nafikiri chanzo kikuu ni kudharau au kupuuza mila na desturi zetu ambazo zote zinaonekana hazifai wakati ni dhahiri ndani ya mila na desturi hizo kulikuwa na mafundisho ambayo yalizingatia kulinda maadili yetu kwa vijana waliyokuwa wanaelekea rika ya kuwa watu wazima.
Nafikiri kinachotokea ni kuwa wale ambao wamekuwa kwenye mazingira yasiyo na miongozo ile ya kimaadili ambayo baba zetu walipitia sasa wamefikia utu uzima na wanashika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya jamii. Ni sawa na kumfanya mtoto awe baba ndani ya nyumba. Ni dhahiri kuwa mambo mengi yataanza kwenda kombo, siyo kwa makusudi, ila ni kwa kutokuwa na mifano na mafunzo ya jambo gani ni sahihi na jambo gani ambalo halistahili kuvumiliwa.
Utaifa
Taifa linaloundwa na viongozi na raia wasio waadilifu linaathiriwa na hatari ya kudhoofu kwa misingi ya utaifa ambayo iliwasukuma wazalendo walioungana zaidi ya miaka hamsini iliyopita kudai Uhuru wetu.
Uzalendo ni kama suala ambalo ni kichekesho siku hizi. Kuna watu hawaamini kuwa wapo Watanzania ambao wako tayari kujitoa muhanga kulinda utaifa kwa kusukumwa na uzalendo.
Uchumi wa Kujitegemea
Tunasikia mara kwa mara kuwa hakuna sababu yoyote ya Tanzania kuwa nchi masikini; na kwamba kuna vyanzo vya kutosha kuweza kuleta maendeleo makubwa. Lakini kwa sera hizi za ubinafsishaji na utukuzaji wa sekta binafsi, sidhani kama jitihada hizi za kujenga uchumi usiyo tegemezi zinaweza kuleta mafanikio na maendeleo ya haraka.
Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nazo zinaashiria kuwa usimamizi mzuri wa mapato na matumizi ya Serikali vinaweza kuwa mchango mkubwa wa kusukuma maendeleo yetu.
Mimi siku zote ninaamini kuwa, kuacha ung’ang’anizi wa kiitikadi tu, haipo sababu ya msingi ambayo inaweza kushikilia hoja ya Serikali kujitoa kwenye shughuli za kiuchumi. Tunapoitoa Serikali kumiliki hisa kwenye shughuli kuu za kiuchumi tunafanikisha masuala mawili ya msingi na yote ambayo hayana manufaa yoyote kwa masilahi ya umma. Kwanza, tunaipunguzia Serikali vyanzo vya mapato ambayo yatatumika kwa manufaa ya wote; pili, tunatoa fursa kwa mashirika au watu wachache kunufaika na rasilimali zetu na kuwanyima wengi nafasi ya kunufaika na rasilimali hizo kupitia hisa ambazo zingeshikwa na Serikali.
Hivi karibuni mzozo wa mpaka na Malawi ulizua hisia kuwa Tanzania ingeweza kupigana vita na Malawi. Kwa bahati nzuri, tulimsikia Rais Kikwete akisema kuwa hatuwezi kufikia hatua ya kupigana vita kwa sababu anaamini kuwa mzozo huu utatatuliwa kwa njia za kidiplomasia. Kwa sera ambazo tunazo sasa hivi, na kama siyo kwa busara hizo za kuepuka vita, ingewezekana kabisa kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupigana vita kali na kuleta hasara ya mali na maisha, halafu rasilimali zote ambazo zimezusha vita zikapewa mwekezaji kwa manufaa yake na ya kampuni yake na sisi kuambulia chini ya asilimia 5 ya mapato ya yule mwekezaji!
Hizi vita bado zinapiganwa kwa jina la Tanzania ingawa siyo kwa kutumia silaha, na faida zake kwenda kwa kampuni chache au watu wachache. Mimi nafikiri umewadia wakati wa kurudisha, siyo kwa nadharia tu, lakini kwa vitendo, umiliki wa dhati wa rasilimali za nchi kwa watu wake ili wote tunufaike nazo na siyo genge la watu wachache ambao wanatuimbia wimbo usioisha kuwa sekta binafsi ndiyo mwarobaini wa kila kitu.
Serikali haipaswi kushiriki katika kila mradi wa kiuchumi, lakini yanaweza kuchanguliwa maeneo nyeti ambayo Serikali itakuwa na hisa za kutosha na kuacha sehemu ya hisa hizo kumilikiwa na sekta binafsi.
Sekta binafsi iwepo na ifanye kazi pamoja na Serikali, lakini huu uongo kuwa Serikali haina nafasi katika shughuli za kiuchumi unatoa fursa kwa wachache kunufaika na rasilimali; na wengi kulishwa takwimu tu kuwa uchumi wetu unakua kwa kasi nzuri.
Umoja na mshikamano
Mimi naamini kuwa suala la umoja na mshikamano limepata pigo kubwa sana katika miaka ya hivi karibuni na kwa kweli inawezekana kuwa ukiitisha kura ya maoni Watanzania wa upande wa Zanzibar watachagua kutupilia mbali Muungano.
Aidha, kuna masuala ya kisiasa na dini ambayo sasa yanaanza kuwatenganisha Watanzania. Mwalimu Nyerere alisema kuwa unapoona kiongozi anaanza kutumia udini au ukabila kutafutia umashuhuri, basi ni dhahiri kuwa kiongozi huyo hana hoja za msingi na anatafuta kura za huruma zisizohitaji tathimini ya kweli ya mpiga kura.
Kutangazwa makao mapya ya wilaya mpya ya Butiama
Mimi nakiri kuwa ni mmoja wa watu ambao sikufurahia uamuzi wa Butiama kutangazwa kuwa Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Butiama kwa sababu niliamini kuwa kuja kwa wilaya kutaleta pia athari kadhaa.
Kwanza, inafahamika kuwa makao ya wilaya yanahitaji maeneo yenye ukubwa mahususi ya kujenga makao yenyewe rasmi ya wilaya, ikiwa ni pamoja na ofisi za taasisi mbalimbali ambazo zinaambatana na uamuzi huo. Na mimi naamini kuwa ardhi ya Butiama ni ndogo kiasi kwamba italeta matatizo katika kuainisha maeneo hayo ya kuweka hayo majengo na taasisi bila kuathiri wakazi wa Butiama.
Hata hivyo, naamini kuwa limechaguliwa eneo sasa ambalo halina wakazi wengi na ambalo pengine litapunguza huu mgongano ambao nauzungumzia.
Pili, kuna uasilia ambao unaambatana na eneo fulani kuwa kijiji na uasilia huu unaambatana na desturi fulani ambazo zinapambanua eneo moja la Tanzania na jingine. Ujio wa wilaya na halmashauri unakuja pia na mambo ya kimjini mjini ambayo kwa desturi yake, hufuta uasilia wa eneo husika, na utaifanya Butiama badala ya kuwa kijiji chenye desturi mahususi kuwa kama eneo lingine lolote la mji la Tanzania.
Watu wengine wanasema kukubali wilaya ni suala la kwenda na wakati, lakini kwa kuwa mimi najihusisha na uratibu wa asasi ya jamii inayosimamia uendelezaji wa tamaduni chini ya Mpango wa Utalii wa Utamaduni unaosimamiwa na Bodi ya Utalii Tanzania, nina wasiwasi kuwa kuja kwa wilaya kunazua changamoto nyingine katika kulinda na kutunza mila na desturi za Wazanaki na kutadhoofisha hii azma ya kulinda tamaduni ambazo tayari zimeshaanza kupotea kutokana na kasi ya mawasiliano mapya na nguvu ya utandawazi.
Siyo suala la kujenga ukabila, ila ni suala tu la kutunza na kulinda asili ya eneo husika.
Nimesikia mmoja wa viongozi wetu akisema kuwa faida za kuwa na wilaya ni kuwa Serikali itaweza kutenga fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu kama vile upatikanaji wa maji safi na salama, mawasiliano na barabara. Hayo, bila shaka yakija yatakuwa na manufaa kwa wote.
Labda baada ya miaka 50 itakuwa rahisi watu kutathimini kama Butiama itakuwa imenufaika kwa kuwa wilaya au itakuwa imeathiriwa kwa uamuzi huo. Kila jambo lina faida na hasara zake, na hili litabaki hivyo kwa uamuzi huu pia.
Wageni Butiama
Nikiwa kama Mratibu wa asasi ya kijamii inayojulikana kama Butiama Cultural Tourism Enterprise (BCTE) tumekuwa tunasimamia sehemu ya kazi ya kupatangaza Butiama kama kivutio cha kihistoria na kiutamaduni, tukishirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania.
Kwa wastani tunapata wageni 450 kwa mwezi na kwa kawaida mwezi huu wa Oktoba ndiyo tunapata wageni wengi zaidi kwa kuwa Oktoba 14, siku ambayo alifariki Mwalimu Nyerere, tunakuwa na idadi kubwa ya watu wanaozuru Butiama.
Sehemu kubwa ya wageni hawa ni Watanzania, lakini tunapata wageni pia kutoka nchi jirani za Kenya na Uganda na baadhi ya nchi za nje.
Butiama iko karibu na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa hiyo baadhi wa wageni wanaokwenda au kutoka huko hupita Butiama.
Tuhuma za kuuawa kwa Mwalimu Nyerere
Binadamu wengi wanapenda sana kuamini kuwa kila jambo likitokea, basi kuna mkono wa mtu unahusika. Na hivi karibuni kifo cha Mwalimu Nyerere kimehusishwa na njama mahususi za kumuua.
Kwa desturi za Kizanaki hakuna mtu ambaye anakufa kwa sababu ya ugonjwa au uzee, lazima yuko mtu miongoni mwa wale waliobaki hai ambaye amesababisha kifo chake kwa njia za uchawi! Kwa mfano, Bibi Christina Mgaya wa Nyang’ombe, mama mzazi wa Mwalimu Nyerere, mara baada ya kifo cha mume wake Mtemi Nyerere Burito tarehe 30 Machi 1942, alitimuliwa Butiama na kuhamia kwa ndugu zake katika kijiji jirani cha Muryaza baada ya kutuhumiwa kuwa alisababisha kifo cha mume wake.
Kwa hiyo, hakurithiwa kama ilivyo desturi za wakati ule za mila za Kizanaki. Aliishi kwa jamaa zake hadi Mwalimu Nyerere alipotoka masomoni Uingereza na kudai arudi nyumbani na akarudi, ingawa baadhi ya ndugu zake hawakufurahia kurudi kwake Butiama.
Kwa hiyo basi, ni kawaida kabisa kwa hisia kama hizi kuwapo ndani ya jamii. Lakini kusema hivi haina maana kuwa haiwezekani kuwa tuhuma hizo ni za kweli. Lakini mtu yeyote muungwana hawezi kuanza kutoa shutuma nzito kama hizi bila kuwa na ushahidi usiotiliwa shaka na ambao hauna dosari.
Lakini naweza kuelewa kwanini baadhi ya watu ambao wanashikilia hizi tuhuma kuwa zinaweza kuwa ni kweli. Tunamfahamu Mwalimu Nyerere kuwa, hata baada ya kustaafu, hakukalia kimya uamuzi au matukio ambayo aliamini yanaathiri baadhi ya msingi ambayo yeye aliiona kuwa ni nguzo inayoshikilia nchi yetu. Baadhi ya haya ni uadilifu ndani ya uongozi, umoja, uzalendo na sera zenye kujali masilahi ya wengi badala ya sera zinazokuza na kulinda nafasi kwa wachache kujinufaisha.
Na kwa kweli ukichunguza baadhi ya matukio kwenye nyanja ya siasa katika kipindi hiki ambacho amefariki dunia, yametokea mengi ambayo tunaamini kuwa kama angekuwa hai asingenyamaza na angeyazungumzia kuyapinga na kuyakemea au kuyatungia kitabu pale ambako ujumbe wake aliona unapuuzwa.
Kwa hiyo, mtu yeyote ambaye anafuatilia hali ya uongozi nchini, na watu wengi wanasema hivi, ni kuwa Mwalimu Nyerere angekuwapo labda baadhi ya uamuzi na mienendo ya baadhi ya viongozi wetu ungekuwa tofauti kwa kuogopa kauli yake au kuandikiwa kitabu ambacho kitajenga hoja inayopingana na uamuzi wa viongozi. Na pengine baadhi ya uamuzi ambao umefanyika usingefanyika.
Kwa mantiki hii unaweza kuanza kujenga hoja kuwa baadhi ya wale waliyofanya uamuzi unaoonekana unaenda kinyume, au cha maadili ya uongozi, au unapingana na masilahi ya umma, walitafakari kuwa njia rahisi ya kurahisisha mipango yao ni kumuondoa huyu mzee mapema. Hiyo unaweza kusema, lakini haitakuwa sahihi kufanya hivyo bila kuwa na ushahidi.
Nimewahi kusikia tuhuma kuwa Rais Kikwete anatuhumiwa kuwa ndiye mtu aliyetumwa na nchi za Magharibi kukimaliza Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nilivyosikia tuhuma hizi niliona kichekesho, lakini ukiangalia baadhi ya matukio katika uongozi wake ambayo yanaweza kuashiria hoja hiyo unaweza kuyapata.
Enzi za Mwalimu Nyerere waliotuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya uongozi waliitwa pembeni na kuambiwa wajiuzulu. Miaka ya hivi karibuni wale ambao walikabiliwa na tuhuma za aina hiyo waliombwa kutafakari wao wenyewe uamuzi sahihi wa kuchukua. Uamuzi mgumu haufanyiki, upinzani wanapata mada ya kuzungumzia kwenye mkutano wao ujao, na CCM inazidi kudhoofu. Kama nilivyosema, hakuna ushahidi wa wazi, lakini kuna viashiria tu.
Nafikiri njia nzuri ya kufunga mjadala huu ni kuzungumza kama wanasheria wanavyosema; hakuna ushahidi mpaka sasa unaothibitisha hizo tuhuma juu ya njama za kumuua Mwalimu Nyerere.
Hoja kuwa uchunguzi ufanyike kubaini kama aliuawa sioni kama zitaleta faida yoyote kwa sababu ameshafariki tayari na hakuna uchunguzi ambao utarudisha uhai wake. Mwalimu Nyerere tunamkumbuka kwa maandishi na matamshi yake. Na naamini kuwa katika uhai wake aliandika na kutamka masuala yote ambayo aliamini ni ya msingi kwake na kwa jamii.
Kuna kiongozi mmoja ambaye amewahi kusema iwapo kuna wazo la msingi ambalo binadamu amelisema katika uhai wake, basi hilo wazo litadumu hata kama aliyelisema hayuko tena duniani. Badala ya kutafuta wachawi sasa hivi mimi nafikiri wale wote ambao wanaamini kuwa Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa kwa nchi hii watumie muda wao kutafakari kazi aliyofanya na kujumuisha fikra zake na matendo yake kupima yale ambayo bado yanaweza kuwa suluhisho dhidi ya baadhi ya changamoto zinazoikabili Tanzania sasa hivi.
Iwapo hoja zake zina nguvu katika mazingira ya sasa, basi hazihitaji yeye mwenyewe kuzisemea. Wanaoziamini wazichambue na wazitumie kama silaha ya kupambana na upungufu ambao tunauona leo katika nyanja mbalimbali.
Lakini pia ni muhimu kwa vijana kujitafutia elimu kuhusu hayo yaliyopita ili kupata mifano mizuri ya uongozi ambayo iliweka masilahi ya Taifa mbele na kuzuia kabisa hizi hoja za siku hizi za kumpa kila mtu fursa ya kufanya anavyotaka. Zinazungumzwa fursa za mwananchi, lakini ukweli ni kuwa baadhi ya viongozi wanapigana vikumbo na wananchi hao hao kutafuta fursa zao binafsi.
Madaraka Nyerere ni mmoja kati ya watoto wanane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tangu kifo cha Mwalimu, amekuwa akiishi Butiama akiwa Mratibu wa asasi ya kijamii ya Butiama Cultural Tourism Enterprise (BCTE) inayoitangaza Butiama kama kivutio cha kihistoria na kiutamaduni kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania.
e-mail: [email protected]
selula: 0782640033