Na Mwandishi Wetu

MADAKTARI tari wa Tanzania wamerejea nchini baada ya kuhitimisha Kambi tiba nchini Comoro kwa kutoa huduma kwa wagonjwa  2,770 na kufanya upasuaji kwa wagonjwa  saba.

Kwenye kambi hiyo ya siku saba wameweza kubaini wagonjwa takriban 269 wanahitaji rufaa za matibabu zaidi nje ya nchi na pia kuainisha fursa zaidi za ushirikiano katika sekta ya Afya.

Akizungumza leo mara baada  kuwasili katika uwanja wa ndege  wa Julius Nyerere, Mkurugenzi wa Global Medicare, ambao ndio waratibu wakuu wa kambi hiyo, Abdulmalik Mollel, alisema kambi imekwenda vizuri na wamefanikiwa kuwahudumia watu wengi.

Alisema nje ya kambi hiyo walifanya kikao maalum na Waziri wa Ulinzi wa Comoro ambaye pia ni Msaidizi wa Rais na Katibu  Mkuu wa Chama tawala kinachoongoza Jamhuri ya Comoro.

“Namshukuru Dk Peter Kisenge kwa imani aliyoonyesha kunipa kazi ya kuandaa kambi, naishukuru Wizara ya Afya kwa kunipa fursa ya kuandaa kambi hii,  namshukuru Profesa Mohamed Janabi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Utalii Tiba, natoa wito hospitali kubwa nchini kuwa wafungue mipaka waende nchi jirani na sisi Global Medicare tutashirikiana kutimiza azma ya Rais Samia ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii tiba,” alisema

“Kwenye vikao kama saba tulivyofanya tulijadili fursa mbalimbali za uwekezaji na ushirikiano kwenye sekta ya afya baina ya Tanzania na Comoro na yeye Msaidizi wa Rais kwenye kikao aliongelea fursa kama watapatikana madaktari wa Tanzania kufanyakazi Comoro,”

“Nje ya kambi tuliangalia uwezekano wa hospitali ya Tanzania kuchukua kazi za hospitali moja ya Comoro yenye vitanda 100 na kuangalia uwezekano wa kuangalia utaalamu ambao haupatikani Comoro sisi watanzania tuupeleke kwao,” alisema

“Tumefanya vikao mbalimbali vyenye tija, tumekaa na Waziri wa Afya wa Comoro na tumekaa na Mshauri Mkuu wa Rais wa Comoro kuangalia mambo ya msingi ambayo tunaweza kushirikiana na uwekezaji ambao umefanyika Tanzania,” alisema

“Tulikaa na Jumuiya  inayojihusisha na elimu ya saratani tulikaaa na Mkuu wa idara ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Comoro tukachambua kozi za afya ambazo wanazitoa kwenye vyuo vyao na ambazo hazitolewe kwao lakini Tanzania zipo ili tuweze kuzipeleka,” alisema

Mollel alisema vikao hivyo vilihudhuliwa na Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Said Yakub, Mkurugenzi wa JKCI, Dk Peter Kisenge, Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Aisha Mahita na Mkurugenzi wa Global Medicare, Abdulmalik Mollel.

Naye Dk Kisenge aliushukuru ubalozi wa Tanzania nchini Comoro na mratibu wa kambi hiyo, Global Medicare ikiongozwa na Mkurugenzi wake, Abdulmalik Mollel kwa kufanikisha kambi hiyo.

Aliishukuru wakurugenzi wenzake wa hospitali mbalimbali ambao waliridhia madaktari wa hospitali kutoa madaktari na wataalamu mbalimbali kwenda Comoro kushiriki kambi hiyo.

Alimshukuru Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi, MOI, Ocean Road, Benjamin Mkapa, kwa kukubaliana kufanya kambi hiyo kwa pamoja na ambayo alisema imefanyakazi nzuri sana kuliko kambi iliyowahi kufanyika.

Dk. Kisenge aliishukuru Global Medicare ambayo ilikuwa mratibu mkuu wa kambi hiyo kwa mafanikio yaliyopatikana na aliwashukuru madaktari walioshiriki kwenye kambi hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya na kuweka jina kubwa nchini Comoro kwenye kambi hiyo.

Dk Kisenge alisema kuwa kambi iliyomalizika Comoro imekutanisha wadau mbalimbali na kufanya vikao vitakavyoleta tija kwenye ushirikiano wa sekta ya afya Comoro na Dar es Salaam.

“Kwa uwekezaji tulionao kwenye hospitali zetu ili nchi zinazotuzunguka zinufaike na uwekezaji huo lazima tumuunge mkono Rais wetu kwa kufanya kama Comoro na Global Medicare isichoke kuratibu kambi kama hizo kwasababu tunataka kupiga hatua nyingine na madaktari wote nchini wawe tayari inapotokea kambi kama hii wawe tayari kwenda kama walivyofanya Comoro,” alisema

Naye mwakilishi wa Wizara ya Afya, Aisha Mahita alishukuru Wizara ya Afya kwa kuridhia yeye kwenda Comoro ambapo ameona halihalisi ya uhitaji mkubwa wa madaktari wa Tanzania nchini Comoro.

Aliishukuru Global Medicare kwa kuratibu kambi hiyo kwa ufanisi mkubwa  na kuongeza kuwa kwamba wamegundua kuwa afya ni uchumi na tiba ni talii  na ni fursa.