Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza
Zaidi ya Madaktari bingwa 60 wameweka kambi Jijini Mwanza kwaajili ya kutoa huduma mbalimbali za kimatibabu kwa wananchi pamoja na kuwajengea uwezo watoa huduma katika hospitali zao ili waweze kuendelea kutoa huduma zilizo bora.
Hayo yamebainishwa Leo Jumatatu Novemba 4, 2024 na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Elikana Balandya wakati akizindua huduma za kibingwa na bingwa bobezi awamu ya pili katika Hospitali za Halmashauri zitakazofanywa na madaktari wa Rais Dkt.Samia Suluhu kuanzia Novemba 4 hadi 9 Mwaka huu.
Balandya alisema huduma ambazo zitatolewa na Madaktari hao ni magonjwa ya wanawake na ukunga, magonjwa ya watoto na watoto wachanga, huduma ya upasuaji na upasuaji wa mfumo wa mkojo, magonjwa ya ndani, huduma ya kinywa na meno pamoja na upasuaji wa mifupa.
Alisema wananchi wa Mkoa huo wenye matatizo ya kiafya wanapaswa kuhudhuria katika hospital zao ili waweze kupata matibabu Kwa Madaktari bingwa na bingwa bobezi katika kambi walizopiga ambapo itawasaidia kuepuka gharama za usafiri, kusafiri umbali mrefu pamoja na baadhi ya wagonjwa kutoka nje ya wilaya na Mkoa.
Balandya alieleza kuwa huduma hizo zitatolewa katika hospital 9 zenye hadhi ya Wilaya ambazo ziko katika Halmashauri nane za Mkoa wa Mwanza.
“Hosptali hizo ni Ilemela, Nyamagana, Buchosa, Kwimba, Misungwi, Magu, Sengerema, Nansio pamoja na Bwisya”, alizitaja Balandya.
“Huduma hizi zimesogezwa kwetu inabidi na sisi wananchi wa Mkoa wa Mwanza tuzitumie vyema kwani huwa ni mara chache sana huduma hizi za kibingwa na bingwa bobezi kuzipata katika maeneo yetu” Alisema Balandya.
Amesema kuwa huduma hizo zinahitajika ili kuendelea kuboresha afya ya wananchi wa Mkoa huo ukizingatia wamekuwa wakipokea wagonjwa wengi wa nje Kwa ajili ya matibabu.
Kwaupande wake Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za afya ya Mtoto,mtoto mchanga na vijana Felix Bundala alisema tangu kuanzishwa Kwa huduma hiyo ya matibabu tayari wameweza kutoa huduma Kwa mikoa 20, Halmashauri 137, vituo 139 pamoja na kuwafikia wagonjwa elfu 60.
Nate Daktari Bingwa wa upasuaji kutoka Hospital ya Chuo Kikuu cha Dodoma, Timothy Kibina alieleza kuwa utoaji wa huduma hiyo umewasaidia watu wengi kutokana na hospital kubwa kuwa mbali na mazingira wanayoishi.