Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Arusha
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema chama cha madaktari bingwa wa maradhi ya Saratani (TOS) kinapaswa kuhamasisha madaktari waliomaliza masomo na wanaofanya kazi kujiunga katika kusomea programu ya Saratani(oncology) ili kuweza kuondokana upungufu wa madaktari bingwa wa Saratani ambao mpaka sasa wapo 38 hapa nchini.
Rai hiyo imetolewa na mkurugenzi wa taasisi ya Saratani Ocean road Dkt Julius Mwaisilage wakati akisoma hotuba ya waziri wa Afya Ummy Mwalimu katika ufunguzi kongamano la kwanza la kimataifa la Saratani lililojumuisha wataalamu na wadau mbalimbali
Ambapo amesema kuwa kutokana na upungufu mkubwa wa madaktari bingwa wa Saratani daktari mmoja kwa mwaka anahudumia wagonjwa 1200 hali ambayo inasababisha daktari kuzidiwa na wagonjwa na ufanisi kuwa hafifu.
Dkt Mwaisilage alisema kama chama wana malengo yao lakini kikubwa wahamasishe wataalamu waweze kusomea kwani serikali inatoa ufadhili kila mwaka kwa kupeleka fedha chuo kikuu cha Afya na sayansi shirikishi Muhimbili(MUHAS) hivyo wawahamasishe ili kupunguza upungufu huo.
Aidha alisema kuwa kulingana na takwimu wanazoziona katika hospitali kwa mwaka wanawaona wagonjwa asilimia 33 ambapo idadi hiyo ni ndogo kwani Tanzania ina zaidi ya wagonjwa elfu 42 wa Saratani.
Sambamba na hayo alisema kuwa serikali imejipanga katika kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya kutibu ugonjwa wa saratani ikiwemo tiba ya upasuaji na uchunguzi wa ugonjwa huo katika hospitali zote za kanda na taifa nchini.
Amesema tiba ya mionzi inaendelea kuboreshwa nchini ikiwa sasa wanaendelea katika hospitali ya KCMC pamoja na Benjamin Mkapa ikifuatiwa na Mbeya lengo ni kuhakikisha huduma za utambuzi wa saratani zinawafikia wananchi katika kanda zote.
Kwa upande wake Rais wa TOS Dkt Jerry Ndumbaro amesema lengo la kongamano hilo la kimataifa ni kubadilishana uzoefu wa kisayansi katika kuboresha huduma kwenye eneo la saratani ikiwa idadi ya wagonjwa kwa sasa inaongezeka hasa maeneo ya vijijini.
Amesema kupitia chama hicho wanampango mkakati wa kufanya huduma za upimaji na ugunduzi wa mapema wa saratani katika jamii ambapo watapita kila mkoa kuhakikisha huduma hiyo inawafikiwa wananchi wa ngazi zote.