Na WAF – Iringa
Mpango kabambe wa madaktari bingwa wa Dkt. Samia utasaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa kuwajengea uwezo watoa huduma wengine katika Hospitali za Halmashauri kwa kuwa dhamira ya Serikali ni kuwa na wodi maalum za watoto wachanga (NCU) katika Hospitali hizo ili kuokoa maisha ya watoto wachanga wenye siku 0-28.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Mei 6, 2024 wakati akizundua Mpango kabambe wa utoaji wa huduma za Kibingwa kwenye Hospitali 184 katika ngazi ya Halmashauri zinazofanywa na Madaktari bingwa wa Dkt. Samia yenye kauli mbiu isemayo “Tumekufikia, Karibu Tukuhudumie”.
“Nasisitiza tena kwamba, sambamba na utoaji huduma na kujenga uwezo wa watoa huduma wetu, Madaktari bingwa saidieni uanzishaji na kuimarisha utendaji wa NCU kwa kuwa katika mpango huu mtafikia Hospitali zote za Halmashauri.” Amesisitiza Waziri Ummy.
Waziri Ummy ameongeza kuwa kila mwanamke mjamzito anayefika Hospitali kwa ajili ya kujifungua anatakiwa atoke salama yeye na kichanga chake.
“Tunaweza kuokoa maisha ya watoto wachanga endapo tutaanzisha wodi maalum za watoto wachanga, tukaviwekea vifaa tiba ili endapo mtoto akiwa na changamoto yoyote aweze kupata huduma”. Amesisitiza Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka rekodi Duniani kwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 80, kutoka vifo 556 kati ya vizazi hai 100,000 mwaka hadi vifo 104 kati ya 100,000.
“Tumsaidie Rais Samia kuvunja rekodi nyingine Duniani, ya kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa kuwa vifo hivyo tumevipunguza kwa asilimia nne tu, kutoka vifo 25 katika kila vizazi hai 1,000 hadi vifo 24 katika kila vizazi hai 1,000 takwimu za Mwaka 2020/22.” Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy ametoa wito kwa viongozi wa Mikoa na Halmashauri kufanya kazi kwa karibu na ushirikiano wa hali ya juu kwa madaktari bingwa wa Rais Samia kwa kuwa wamekuja hapa kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za mama na mtoto Dkt. Felix Bundala amesema katika siku Tano Mikoa ya Tanga, Songea pamoja na Geita wamefikiwa wateja 6,381.
“Kati ya wateja 6,381 walioonwa, waliofanyiwa upasuaji ni 166 sawa na 3% waliopewa rufaa ni 42 ambao ni sawa na mtu Mmoja katika watu 100 amepata rufaa.” Amesema Dkt. Bundala.