Katika gazeti la Jamhuri la Jumanne Agosti 19 – 25, 2014 ISSN No. 1821-8156 Toleo No. 150, zilichapishwa taarifa potofu zenye kichwa cha habari;
KASHFA IKULU;
· Nyalandu atumia Leseni ya Rais kuua wanyamapori 704 bure,
· Watakaouawa wamo pia tembo 8, chui 8, Simba 8, ndege,
· Wauaji ni Wamarekani marafiki wa Waziri wa Maliasili.
I. Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuwafahamisha Umma kuwa, tuhuma hizi si za kweli. Tuhuma hizi zimetolewa na watu wenye nia ovu na zimelenga kuchafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na kumchafua mheshimiwa Waziri Lazaro Nyalandu, kumshushia Heshima, kumdhalilisha kwa umma ili kumpunguzia dhamira, malengo na kasi ya kupambana na ujangili.
Kwanza ieleweke wazi kuwa si sahihi Nyalandu kuzigeuza tuhuma zake binafsi kuwa za wizara nzima. Nyalandu anatuhumiwa kama mtu binafsi na kwa hiyo kitendo cha kutaka kufanya tuhuma hizi kuwa za Wizara ni ubabaishaji. Hakuna siri kwamba, ukiacha wapambe wake aliowaweka ofisini kwa mabavu na kwa kukiuka sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, Nyalandu amekuwa tatizo. Haelewani na watendaji wa Wizara. Majukumu ya Katibu Mkuu, Mwanasheria wa Wizara na wakurugenzi kajivika yeye. Kwa hiyo hoja kwamba jina la Wizara linachafuliwa kwa kuibua kashfa za Nyalandu imekosa mashiko.
Ukweli ni kwamba Familia ya Freidkin ilipewa Leseni Maalum/Leseni ya Rais (Special License/President’s License) ya kuwinda kwa mujibu wa Kifungu cha 58 (1) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 ikisomwa kwa pamoja na Tangazo la Serikali Na. 273 la mwaka 1974 ambacho kinampa mamlaka Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori baada kupata ridhaa ya Waziri mwenye dhamana ya Wanyamapori kutoa kibali maalum kwa malipo au bure. Aidha, kibali hicho hutolewa baada ya Waziri kuridhika kwamba kibali hicho kina maslahi kwa taifa na hakikinzani na sheria na mikataba ya kimataifa kama CITES.
Tangazo la Serikali hutolewa kama nyongeza kukidhi mapungufu au kuimarisha sheria iliyopo. Haiwezekani Sheria ya Mwaka 2009 iimarishwe na tangazo la mwaka 1974. Kutaja Tangazo hili kuna nia mbaya ya kuuhadaa umma kuwasheria imefuatwa wakati si kweli.
Kufuatana na Kifungu hicho cha 58 (1) Leseni Maalum hutolewa kwa mtu yeyote kwa masilahi ya kitaifa ikiwemo:-
1. Utafiti wa kisayansi
2. Makumbusho
3. Elimu
4. Utamaduni na
5. Chakula wakati wa dharura
Maslahi ya taifa ni pamoja na leseni kutolewa kwa watu mashuhuri kama vile Wakuu wa nchi, Wafalme, Malkia, Wakuu wa dini pamoja na watu ambao katika utendaji wao wametoa michango yenye manufaa maalum kitaifa au michango mikubwa katika shughuli za uhifadhi wa wanyamapori.
Maslahi ya taifa ni hayo yaliyoainishwa hapo juu (1-5). Hamna mahali sheria inapomruhusu Nyalandu kutumia kichwa chake kujitungia maslahi mengine ya Taifa. Kama haya anayoongeza Nyalandu yangekuwa yamo, kwa nini yasingeorodheshwa au angalau kikaongezwa kipengele katika orodha kinachosomeka na mengineyo kama itakavyoonekana inafaa?
Katika utaratibu huu, kwa mwaka 2013 hadi sasa, Leseni ya Rais zimetolwa kwa watu wafuatao:-
Na. Jina Kibali Na. Kampuni iliyowindisha Bure/Malipo
1 H.H. Sheikh Abdullah Mohamed Buli Al Hamed 000000657 cha 22/8-6/09/2013 Kilombero North Safaris/Green Mile Safaris Bure
2 H. H Sheikh Mohamed Rashid Al Maktoum 0000676 cha 16/01 – 26/01/2014 Ortello Business Corporation (OBC) Bure
3 Familia ya Freidkin ya Watu wanane 00006678-85 za 1-21/08/2014 Tanzania Game Trackers Safaris Ltd Kwa malipo
4 Kiongozi wa Bohora Duniani Bure
Familia ya Freidkin imekuwa na sifa ya kupewa Leseni ya Rais kutokana na mchango wake mkubwa kwa taifa katika shughuli za uhifadhi wa Wanyamapori kwa kipindi cha zaidi ya miaka ishirini iliyopita bila kukoma.
Familia ya Freidkin imekuwa ikitoa mchango huo kupitia Kampuni ya Uwindaji wa Kitalii iitwayo Tanzania Game Trackers Safaris Ltd. Pamoja na Asasi yake iitwayo Freidkin Conservation Fund (FCF tangu miaka ya 1990).
Kwa sheria ipi? Sheria zipo ili zifuatwe. Na sheria hizi zimeandikwa kwenye vitabu. Haiyumkiniki sheria za nchi ziwe zimeandikwa kwenye kichwa cha mtu (Nyalandu). Je ni Friedkin pekee ambaye amekuwa akitoa michango katika uhifadhi?
FCF imekuwa ikitoa michango mikubwa hususan ya kukabiliana na ujangili.
Bw. Freidkin kwa kupitia Taasisi hii amekuwa akichangia na hata kushiriki katika shughuli za kuzuia ujangili na shughuli za kijamii kwa kufanya yafuatayo:-
a. Kwa kushirikiana na watumishi wa Idara ya Wanyamapori katika kazi za kuzuia ujangili amekuwa akichangia mafuta ya doria katika Mapori ya Akiba ya Kizigo, Maswa, Moyowosi, Ugalla na Pori Tengefu la Lake Natron
b. Kutoa magari ambayo hutumika kwenye kuzuia ujangili
c. Kutoa helikopta kwa ajili ya kufanya doria kwenye mapori husika
d. Kuchangia malipo ya doria kwa askari wa Idara.
e. Kuchangia katika shughuli za maendeleo ya jamii kama vile kujenga vituo vya doria (outposts) na ujenzi wa shule mpya (kwa mfano Kizigo Sekondari/Manyoni)
Kwanza ieleweke kuwa si TGTS pekee ambao wamekuwa wakitoa misaada kusaidia uhifadhi kama Nyalandu anavyotaka kuuaminisha umma. Makampuni mengi ya uwindaji yamekuwa yakifanya hivyo. Pili, kuchangia maendeleo ya jamii na shughuli za uhifadhi ni moja ya masharti kwa wawekezaji na ni kigezo muhimu kinachofikiriwa mwekezaji anapoomba kitalu cha uwindaji. Hamna mahali inapoelezwa kwamba mwekezaji atazawadiwa Leseni ya Rais kutokana na kutimiza wajibu huu ambao uko kisheria na kikanuni.
JE; TGTS WANASTAHILI HESHIMA YA KUPEWA LESENI YA RAIS?
Nyalandu anajitetea kwamba Familia ya Friedkin ina sifa za kupata Leseni ya Rais kutokana na mchango wake katika uhifadhi. Nyalandu anaficha ukweli kwamba makampuni ya Friedkin ndiyo yanazoongoza kwa kuivuruga Idara ya Wanyamapori. Ubabe wa wakurugenzi wa Kampuni hizi ummeikosesha serikali mamilioni ya Dola kutokana na kufanya fujo katika vitalu ilivyotaka kupora kutoka kwa wamiliki halali. Makampuni haya ya FCF yameishtaki Serikali mara kadhaa na kushindwa kesi lakini bado yameendelea kuisumbua Idara.
Kutokana na ubabe wa Makampuni ya FCF wamiliki halali wa vitalu vya Lake Natron (East) na Makao WMA walishindwa kuendesha shughuli za uwindaji wa kitalii na hivyo kuikosesha nchi mamilioni ya fedha za kigeni. Makampuni haya yalitumia magari na helikopta kutishia wageni wa makampuni mengine na hivyo kuwafanya wageni hao kuondoka na wengine kufuta safari zao kutokana na dhana iliyojengeka kwamba hamna usalama kwenye maeneo ya uwindaji. Aidha, wananchi ambao walikuwa wafaidike kutokana na uhifadhi wameshindwa kutokana na kutokufanyika uwindaji kwenye meneo yao.
La kushangaza ni kwamba wakati Serikali inahangaishwa na Makampuni haya, Nyalandu ambaye alikuwa Naibu Waziri wakati huo alishirikiana nao bega kwa bega kuihujumu serikali.
Kampuni za FCF ziliwahi kutoa tuhuma nzito za uwongo kwenye baraza la Congress dhidi ya watendaji wa Serikali, tuhuma ambazo zilijibiwa kikamilifu na Wizara. Katika majibu hayo. Serikali iliweka wazi tabia za Kampuni za FCF kama ifuatavyo:
- Kimsingi, kampuni za WWS and TGTS zimekuwa na tabia ya ubabe na usumbufu katika tasnia ya uwindaji wa kitalii. Tabia hizi zimeonekana katika sehemu mbalimbali ambapo kampuni hizi zimekuwa zinawinda yakiwemo mapori ya akiba ya Selous, Rungwa na Ugalla.
- Pamoja na mgogoro wa Lake Natron, mgogoro mwingine unaohusiana na kampuni hizi uko kwenye WMA ya Makao ambapo TGTS, ikishirikiana na Kampuni ya Mwiba Holdings, wamejenga kambi kwa ubabe kwenye kitalu ambacho kimemilikishwa kihalali kwa kampuni ya Fereck Safaris Ltd.
- Kampuni ya Mwiba Holdings ilishindwa kwenye mchakato wa maombi ya kitalu cha Makao ambapo ilipata alama 50 wakati washindani wao Fereck walipata alama 92. Hata hivyo, Kampuni hii haikusajiliwa kama Kampuni ya uwindaji na kwa hiyo haikustahili kuomba kitalu cha uwindaji.
- Kampuni ya TGTS kupitia Mwiba Holdings inaendesha utalii wa picha katika kitalu hicho na zinajihusisha na uwindaji haramu. Kampuni hii haina kibali cha kufanya shughuli hizo. Mbaya zaidi wanalindwa na Askari wa Jeshi la Polisi (ushahidi mwingine kuwa wanatumia pesa kununua baadhi ya watumishi wa Serikali wasio waaminifu ili kufikia malengo yao).
- Tayari Wizara imepokea barua kutoka Kampuni ya Fereck Safaris ikilalamikia kupoteza safari mbili na hivyo kudaiwa kulipa fidia.
Aidha, Serikali, ambapo Nyalandu alikuwa Naibu Waziri, ililishauri Baraza la Congress kufanya yafuatayo:
- Baraza la Congress lijue kuwa limepotoshwa na kwamba tuhuma zilizotolewa na FCF ni za uwongo na uzushi.
- Baraza la Congress liunde tume huru kuchunguza na kupata ukweli juu ya madai ya Makapuni ya FCF ili haki iweze kutendeka
- Lijue kwamba tabia za ubabe zisizokubalika zinazoendeshwa na makampuni ya FCF.
- Isaidie kuyashauri Makampuni ya FCF (TGTS na WWS) kutii sheria na kuondoka mara moja katika vitalu ambavyo hayakumilikishwa kihalali na yatakiwe kuacha ubabe.
- Kwamba, FCF imewekeza nchini na inachangia maendeleo ya jamii, isiwe sababu ya kufanya watakavyo na kuvunja Sheria za nchi na haki za binadamu wengine.
- Kwamba, Tanzania ni nchi huru (sovereign state) na kwamba makampuni ya kigeni hayana kinga pale yanapovunja sheria za nchi kwa makusudi.
- Makampuni ya FCF yaonywe kuwa kitendo cha kuwatumia wananchi kufanya fujo kwa manufaa yao kibiashara hakikubaliki na ni uvunjaji wa Sheria za nchi.
- Katika kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa kila upande na kudumisha uhusiano mzuri kati ya Marekani na Tanzania, Baraza la Congress liombwe kuitaka Kampuni ya FCF kuiomba radhi Serikali ya Tanzania na wale wote ambao wameathiriwa na ubabe na tuhuma za uwongo zilizotokana na watendaji wa FCF. Hili lifanyike sambamba na kampuni husika kuahidi kuwa wataendesha biashara zao kistaarabu
Nyalandu alikuwa sehemu ya Wizara, tena Naibu waziri. Na malalamiko yote haya yametolewa na Wizara ambayo yeye alikuwa anaiongoza. Leo miezi michache tu anaposimama Nyalandu na kuwazawadia watu hawa waliokuwa wanaonekana wasumbufu, akidai kuwa wana sifa kutokana na mchango mkubwa katika uhifadhi inabidi kumshangaa sana. Je; yeye kama Naibu Waziri na kama anaamini kuwa walikuwa na haki mbona hakushauri vinginevyo? Kama msimamo wa Serikali ulikuwa kuchukizwa na ubabe wa TGTS na WWS, yeye Nyalandu anapowazawadia Leseni za Rais, tuseme kuwa alikuwa anatumikia Serikali ipi? Mara nyingi Nyalandu ametajwa kumhujumu aliyekuwa Bosi wake, Balozi Kagasheki, na hata kuondoka kwake inasemekana ni kutokana na hujuma za Nyalandu. Je, huu hautoshi kuwa ushahidi juu ya hujuma hizi?
Vibali vilivyotajwa na Gazeti la Jamhuri la tarehe 19/08/2014, Toleo la 150 vilitolewa kwa familia ya Freidkin ya watu wanane (8) kwa ajili ya uwindaji kuanzia tarehe 1 hadi 21 Agosti 2014 kwenye vitalu vya Lake Natron, Makao open na Makao Wildlife Management Area (WMA), Maswa Kimali na Maswa Mbono kupitia kampuni ya Tanzania Game Trackers Safaris Ltd
Maeneo hayo yaliyowindwa hayahusiani na ugawaji wa vitalu kama ilivyoelezwa na gazeti la Jamhuri ya kuwa Waziri Nyalandu amegawa vitalu zaidi ya vitano kwa kampuni moja.. Leseni ya Rais inatuma kuwinda katika sehemu yoyote ile itakayoonekana inafaa kisheria bila kujali idadi ya vitalu husika kwa vile ni shughuli ya mara moja tu.
Kuna kila sababu kuamini kuwa Nyalandu kagawa vitalu hivyo kinyemela kwa rafiki zake wa FCF. Kwanza, kwa kuwa vitalu hivyo vilikuwa vinamilikiwa kihalali na m8akampuni mengine na Nyalandu kuyataka makampuni hayo kuviachia ili vimilikiwe na Makampuni ya FCF. Makampuni ya FCF yamekuwa yakivitaka na kufikia kufanya fujo na kutishia maisha ya wageni wa makampuni yaliyomilikishwa vitalu hivyo kihalali.
Kitalu cha Makao WMA: Kampuni ya Ferreck Safaris ilikubali kuachia kitalu cha Makao WMA baada ya kushindwa kuwinda kwa mwaka mzima kutokana na fujo za Mwiba Holdings anbayo hata hivyo haikusajiliwa kama Kampuni ya Uwindaji. Nyalandu ndiye aliyesimamia makubaliano ya kuachia kitalu hicho na baadaye kuagiza kuwa Mwiba wapatiwe kitalu hicho kwa kisingizio cha kuongezeka vitendo vya ujangili kwa kuwa kitalu hakikuwa na mtu. Leo hii wanapoonekana watu wale wale, rafiki zake Nyalandu, waliokuwa wanawahujumu wenzao ndio wanawinda kwa nini isiaminike kwamba kitalu kimetolewa kinyemela?
Kitalu cha Lake Natron GCA (East): Nyalandu alimtaka mmiliki wa Kitalu hiki kukiachia baada ya mgogoro wa muda mrefu uliosababishwa na WWS (Kampuni ya FCF). Mmiliki huyu ambaye ni Green Mile Safaris (GMS) alikataa na ndipo Nyalandu alipomtishia kwa kusema ‘wewe ni jeuri sana, this will cost you’ (itamgharimu). Kilichofuatia ni barua ya tarehe 11 March 2014 na DVD kutoka Dallas Safari Club ya Texas (makao makuu na FCF) ikimtaka Nyalandu ainyang’anye Kampuni ya GMS vitalu kwa kile kilichodaiwa kukiuka sheria za uwindaji mwaka 2012 huko Selous. Inaaminika kuwa Nyalandu alishiriki katika kuandaa barua na DVD husika. DVD hii ikaibukia Bungeni tarehe 13 na 14 Mei ambapo Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Peter Msigwa, aliituhumu GMS kwa ujangili na kumtaka Nyalandu kuinyang’anya GMS vitalu. Cha kushangaza, Nyalandu akijifanya kuwa hana taarifa na DVD tajwa! Tarehe 16 Juni, TGTS wakaomba Leseni ya Rais na moja ya eneo waliloomba kuwinda ni Kitalu cha Lake Natron (East). Huhitaji akili nyingi sana kujua kwamba ili Nyalandu aweze kuruhusu uwindaji ufanyike katika kitalu hiki ilikuwa lazima akinyang’anye kutoka kwa GMS. Ili kuuzuga umma akamtumia Msigwa ambaye aliita waandishi wa habari Serena Hotel na kujifanya kwamba anamtaka Nyalandu kuichukulia hatua Kampuni ya GMS. Nyalandu naye akaifutia GMS Leseni zote mara moja na siku iliyofuata kukimbilia Marekani kuripoti juu ya alichofanya. Awali, Mwezi Juni Mfalme wa Emirates ambaye tayari aliwasili nchini na ujumbe wake kwa safari ya uwindaji alilazimika kurejea nyumbani baada ya Nyalandu kumzuia kuwinda katika kitalu hicho kwa kile alichodai kuwa kitalu hicho kina mgogoro na kwamba kesi iko mahakamani kwa hiyo kuruhusu uwindaji katika kitalu hicho kungeingilia uhuru wa mahakama. Lakini Nyalandu huyu huyu mara akasahau na kumruhusu Friedkin na familia yake kuwinda kwenye kitalu alichodai siku chahce kabla kwamba kina mgogoro na kwamba hawezi kuingilia uhuru wa mahakama! Je, hatua hii haitoshi kuonyesha kuwa Nyalandu kagawa kinyemela kitalu hicho kwa watu ambao wamekuwa wanakidai kiasi cha kufikia kutishia maisha ya wageni wa kampuni nyingine?
Ni wazi kuwa Nyalandu aliinyang’anya Kampuni ya Green Miles Kitalu ili akigawe kwa rafiki zake TGTS. Tunajiuliza, Hivi Dereva akiangusha gari, yeye anasalimika na adhabu? na hasa kama alithibitishwa kuwa ni dereva na kupewa leseni na mamlaka husika? Uwindaji wa kitalii unasimamiwa na Mwindaji Bingwa (Professional Hunter) nay eye ndiye anayeelekeza watalii mambo ya kufanya na yale ambayo hayastahili kufanywa (dos and don’ts). Aidha, kuna maafisa wa Wanyamapori wanaosimamia zoezi zima la uwindaji. Unapokuwa na watu hawa si lazima Mkurugenzi wa Kampuni husika awepo. Leo hii unapofungia Kampuni na kumwacha Mwindaji Bingwa na maafisa wa wanyamapori nani ataelewa kuwa hapa Nyalandu hakuwa na nia ovu ya kumuonea mzawa ili kutekeleza matakwa ya maswahiba wake na kutimiza kile kitisho alichotoa kwa GMS kwamba ‘It will cost you?’
Makao Open Area: Eneo hili ndilo ambalo limekuwa likiitwa Mwiba Wildlife Ranch. Jina la Makao Open Area limetumika kupotosha watu ili wasijue kilichokuwa kinaendelea. Nyalandu anadanganya kwamba eti Leseni ya Rais inaruhusu uwindaji kufanyika popote! Si kweli, uwindaji wa kitalii unafanyika katika vitalu vilivyotengwa kisheria tu. Mwiba Holdings wamekuwa wanaliita Eneo hilo Mwiba Wildlife Ranch na wamekuwa wakitaka haki ya matumizi (user rights) ili kulitumia eneo hilo kwa ajili ya uwindaji na utalii wa picha. Awali walimwandikia Balozi Kagasheki ambaye aliwajibu kuwa isingewezekana kupata user rights kwa kuwa kanuni za ranchi zilikuwa bado hazijatoka. Baada ya kukwama kwa Waziri, wakarudi kwa Mkurugenzi, lakini sababu zikawa hizo hizo huku wakiahidiwa kufanya subira kwani tayari zilikuwa zimefikia hatua nzuri. Kwa kuelewa kuwa walikuwa hawakidhi vigezo, walimtumia mmoja wa washauri wao kumshawishi Mkurugenzi kutoa vibali lakini wakakwaa kisiki. hapo ndipo walipomtafuta Nyalandu ambaye alimwita Mkurugenzi na kushinikiza kuwa atoe vibali kwa rafiki zake hao. Mkurugenzi alimkatalia Nyalandu na kueleza madhara ya kutoa vibali hivyo. Aidha, alimshauri Nyalandu awasiliane na Waziri ambaye tayari alikataa ombi hilo. Leo hii Nyalandu, baada ya kupata Uwaziri kamfukuza Mkurugenzi na Msaidizi wake. Zaidi, katoa kibali uwindaji ufanyike katika eneo hili ambalo halina sifa kama kitalu cha uwindaji. Je, sio kweli kwamba karuhusu uwindaji ufanyike katika eneo ambalo si kitalu?
Uchambuzi wa makala ya gazeti hili ulitaja vipengele kama:-
a) Gazeti la Jamhuri liliandika taarifa potofu yenye kicha cha habari; KASHFA IKULU
Gazeti la Jamhuri liliandika taarifa potofu kuwa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ametumia Leseni ya Rais kuwaruhusu marafiki zake Wamarekani wanane kuua wanyamapori 704 bila kulipa hata shilingi moja serikalini.
Tuhuma hizi si za kweli.
Ukweli ni kuwa, Pamoja na leseni hii kuitwa Leseni ya Rais kwa Mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 273 la mwaka 1974, leseni hiyo haitolewi na Ikulu bali hutolewa na Mkurugenzi wa Wanyamapori baada ya kupata ridhaa ya Waziri mwenye dhamana ya kusimamia Maliasili na Utalii na leseni hiyo haikutolewa bure.
Hamna aliyedai kuwa Leseni hiyo inatolewa na Ikulu. Lakini mradi jina la Rais limetajwa ni wazi kuwa ina uhusiano mkubwa na Ikulu. Ina heshima yake na si Leseni ya kufanyiwa mchezo kama mtu anavyotaka. Leseni alizoorodhesha Nyalandu, ukiacha hiyo ya rafiki yake, zilitolewa kwa maagizo ya Rais mwenyewe. Mchakato mzima hupitia Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje. Kitendo cha Nyalandu kutoa Leseni hiyo bila sababu za msingi, tena kwa mfanyabiashara, ni matumizi mabaya ya madaraka. Ni uporaji wa mamlaka ya Rais.
Kama Nyalandu anataka tuamini kuwa Friedkin alikuwa mgeni wa nchi mwenye hadhi ya kupata leseni za Rais, angetueleza bila kuficha kwamba ni kwa nini mchakato huu haukuratibiwa na Foreign Affairs.
b) Tuhuma zilizotolewa na gazeti la Jamhuri dhidi ya Waziri Nyalandu ya kuwa ametoa leseni ya Rais kwa rafiki zake Freidkin na familia yake pia si za kweli.
Nyalandu anataka umma kuamini kuwa hana uhusiano wa kimaslahi na makampuni ya FCF. Si vizuri kumtaja Marehemu, lakini inapobidi tunalazimika kufanya hivyo. Wakati wa uhai wake na hata leo, huwezi kumtenganisha Marehemu Nyaga Mawala na makampuni ya Friedkin. Alikuwa mwanasheria wao na mtetezi waliyemwamini sana. Kwa bahati mbaya yeye pia alitumiwa na makampuni haya kuiyumbisha tasnia ya uwindaji wa kitalii nchini. Nyaga Mawala, alikuwa mtu wa karibu sana wa Nyalandu na James Lembeli. Na wote walikuwa miongoni mwa watu waliohudhuria mazishi yake Nairobi. lazima Mtu makini atahoji chimbuko la urafiki huu.
Leseni ya Rais ilitolewa kwa familia ya Freidkin na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kwa kuzingatia utaratibu kama walivyopewa watu wengine ambao wamekidhi vigezo kama ilivyoelezwa hapo juu.
Utaratibu haukufuatwa. Friedkin ni mfanyabiashara na sheria inasema kuwa leseni hiyo isitolewe kwa maslahi binafsi na kwa malengo ya biashara. Nyalandu amekuwa anafadhiliwa na Makampuni ya FCF kwa kupatiwa ndege kwa matumizi ya binafsi. Wakati anazunguka nchi nzima kuuzuga umma kuwa yeye ndiye anayefaa kurithi mikoba ya Kagasheki, wafadhili wake wakubwa walikuwa makampuni ya FCF ambayo yalithubutu kumpatia ndege kila alipohitaji. Kwa hiyo, hamna ubishi kwamba Leseni tajwa ilitolewa ili kulipa fadhila.
Tuhuma zilizotolewa na gazeti la Jamhuri dhidi ya Waziri Nyalandu ya kuwa ametoa leseni la kuwinda wanyamapori 704 bila malipo pia si za kweli.
Ukweli ni kuwa, si kweli kwamba familia ya Freidkin ilipewa leseni bila malipo kwani familia hiyo ilipewa Leseni ya Rais baada ya kulipia ada ya vibali (permit fee), ada ya nyara (trophy handling fee) na ada ya uhifadhi (conservation fee) na ada ya wanyamapori watakaowindwa ambayo ingelipwa baada ya uwindaji kufanyika kama ilivyo kwenye Kanuni za Uwindaji wa Kitalii (GN No. 243 Kanuni 21 (1),
Leseni husika ilikuwa na sehemu iliyotakiwa kujazwa kiasi cha fedha zilizolipwa. Sehemu hii haikujazwa. Nyalandu angeueleza umma kwa nini sehemu hii haikujazwa. Kama kuna malipo yoyote yaliyofanyika basi ni dhahiri kuwa malipo hayo yamefanyika baada ya gazeti hili kufichua hujuma hii. Ni juu ya Nyalandu kuuthibitishia umma kuwa kwa kutokujaza kiasi kilicholipwa hakuwa na nia ya kuhujumu uchumi wa nchi ili kuwafurahisha marafiki zake hawa.
Utaratibu huu unatumika kwa wawindaji wote wa kitalii.
Kama Friedkin na familia yake walitakiwa kufuata utaratibu unaofuatwa na wawindaji wote wa kitalii, kulikuwa na sababu gani ya kumpatia leseni nane za Rais? Si kweli kwamba kuna agenda iliyojificha hapa?
Idadi ya wanyamapori wanaotolewa kwenye leseni yoyote kupitia kampuni za uwindaji wa kitalii hutolewa kwa kufuata “Safari Package” na siyo wote wanaowindwa kwa kuwa uwindaji ni wa kuchagua kwa kuzingatia ukubwa na ubora wa nyara, umri, jinsia na iwapo wamepatikana eneo husika. Hivyo kama mwindaji anashindwa kupata mnyama mwenye sifa hizo ni kwamba hatawinda mnyama husika hata kama ameandikwa kwenye leseni. Hii ndiyo tasfiri ya kisheria ya kulipia wanyama watakaowindwa tu na siyo wanaoandikwa kwenye leseni/kibali.
Aidha, kulingana na sheria, mwindaji anatakiwa kuandika kila mnyama anayewindwa nyuma ya leseni mara tu baada ya kuwinda kwa kuonesha tarehe mnyama alipowindwa, aina ya mnyama, idadi, jinsia, umri na mahali alipowindwa. Kazi hii huhakikiwa na Afisa Wanyamapori na Mwindaji Bingwa (Profesional Hunter) wa eneo husika kwa mujibu wa Kanuni za Uwindaji wa Kitalii.
Haieleweki. Maelezo haya yanamuondoa vipi Nyalandu kwenye matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa leseni ya Rais kwa mtu asiye na sifa? Anataka kukataa kwamba hakuruhusu wanyama 704 kuwindwa?
c) Tuhuma kuhusu idadi ya wanyama walioruhusiwa kuwindwa ikiwemo kuuwa tembo wanane (8)
Pamoja na familia ya Freidkin kupewa leseni ya Rais kuwindia, hakuna tembo yeyote wala Simba aliyewindwa. Tuhuma kwa Familia ya Freidkin kuwinda Tembo wanane na simba si za Kweli. Tuhuma hizo zilikuwa na nia ovu ya kumchafua, kumdhalilisha Mheshimiwa Waziri Nyalandu pamoja na familia ya Freidkin.
Ukweli ni kwamba pamoja na kuwa idadi ya wanyama hao walikuwa wameandikwa kwenye leseni iliyotolewa, lakini wanyama hao hawakuwindwa kwa sababu hawakuwa wamefikia ubora wa Nyara inayotakiwa kuwindwa kisheria.
Hapa hoja sio kwamba tembo wanane na simba wanane waliwindwa au la. Lakini ni uhalali wa kutumia Leseni ya Rais kuruhusu mauaji ya wanyama hao adimu, hasa katika kipindi hiki ambapo idadi yao imepungua sana. Je, ingetokea wanyama hao alioruhusu Nyalandu wakawindwa angejitetea vipi wakati karuhusu? Inawezekana vipi mtu anayeratibu na kufadhili mipango ya mauaji akajitetea eti kwa kuwa tu aliowatuma kuua hawajafanikiwa kufanya hivyo? Lakini pia, ukweli kwamba Serikali ya Marekani imepiga marufuku nyara za tembo kuingia nchini humo, Kina Friedkin walikuwa wanamwindia nani? Kama Nyalandu amekuwa akituhumiwa kuwa jangili na leo anatoa leseni ya kuuawa tembo wanane, hatujui zinapokusudiwa kupelekwa hizo nyara, atatutoa vipi wasiwasi kuwa hapakuwa na mpango wa yeye kutumia nafasi hiyo kujipatia meno kwa ajili ya biashara haramu anayotuhumiwa kujihusisha nayo?
Kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za uwindaji nchini, mnyama tembo anaruhusiwa kuwindwa kwa ajili ya matumizi binafsi na siyo ya kibiashara.
Friedkin ni mwekezaji na ni mwindaji wa nyara. Ndiye anayemiliki makampuni ya Wengert Windrose Safaris (WWS) na Tanzania Game Trackers and safaris (TGTS). Ni vema Nyalandu akawa wazi kuwa ni matumizi yepi binafsi anayoyakusudia hapa. Rafiki yake alitaka kuua tembo wanane ili wawatumie kwa kazi gani? Na aeleze kuwa nyara ambazo zingepatikana zingeenda wapi, hasa ikitiliwa maanani kuwa Marekani imepiga marufuku uingizaji wa nyara za tembo kutoka Tanzania.
Kufuatana na Mkataba wa CITES, Tanzania imekuwa ikiwinda tembo 50 kwa miaka ya 1990 na baadaye kwenye miaka 2000 tembo 200 idadi ya tembo ilipoongezeka.
Hata hivyo, mwezi Juni 2014 Mhe. Waziri wa Maliasili na Utalii alipunguza idadi hiyo kwa asilimia 50% kutokana na kupungua kwa idadi ya tembo wenye ubora wa kuwindwa. Aidha, uwindaji huo unazingatia viwango vilivyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za Uwindaji wa Kitalii. Endapo tembo aliyeandikwa kwenye kibali au leseni hajafikisha viwango stahiki hatawindwa.
Nyalandu anajitapa kupunguza idadi ya tembo wanaowindwa kwa asilimia 50 (yaani tembo 100). Anakiri kuwa hii inatokana na kupungua kwa idadi ya tembo wenye ubora wa kuwindwa. Wakati huo huo anaruhusu familia moja iwinde tembo wanane. Maana yake ni kwamba ingetokea watu wengine wakaomba kuwinda idadi hiyo hiyo, basi ni familia 12 tu zingemaliza mgawo huo. Hapa busara iko wapi? Ina maana mamia ya wawindaji wengine wasingeweza kupata haki hii ya kuwinda tembo kwa kuwa idadi kubwa imetolewa kwa familia moja yenye urafiki na Nyalandu!
d) Tuhuma ya Kuruhusu wageni kuwinda katika vitalu ambavyo siyo vya kampuni husika
Tuhuma hizi si za kweli.
Tuhuma hizi zina nia ovu ya kudhoofisha kasi ya kupambana na ujangili.
Ukweli nu kuwa, Freidkin na familia yake waliruhusiwa kuwinda kwenye vitalu vya Lake Natron, Makao open na Makao Wildlife Management Area (WMA), Maswa Kimali na Maswa Mbono kwa sababu hii ndiyo maana Freidkin na familia yake walipewa Leseni Maalum/Leseni ya Rais kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 243 la mwaka 2010 Kanuni ya 19(2) ambalo linaeleza kuwa mwenye Leseni ya Rais anaruhusiwa kuwinda eneo lolote kama atakavyoelekeza Mkurugenzi wa Wanyamapori. Kwa mantiki hii, si kweli kwamba Mheshimiwa Waziri Nyalandu alikiuka sheria na kugawa zaidi ya vitalu vitano vya kuwindia kwa familia ya Freidkin.
Hivyo, tuhuma ya kuwa Waziri Nyalandu amekiuka kifungu kinachoweka ukomo wa idadi ya vitalu ambavyo ni vitalu vitano kwa kampuni si za kweli.
Kwa kuzingatia maelezo hayo hapo juu, kutolewa kwa leseni ya Rais kwa familia ya Freidkin kulizingatia sheria, kanuni na taratibu zote za uwindaji.
Tuhuma zote zilizotolewa dhidi ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Mheshimiwa Waziri Nyalandu kuhusu utoaji wa Leseni ya Rais ya kuwindia kwa familia ya Freidkin, zilikuwa na nia ovu ya kuchafua, kudhalilisha na kushusha heshima ya Wizara ya Maliasili na Utalii, na Mheshimiwa Waziri Nyalandu na familia ya Freidkin
e) Tuhuma kuwa Waziri Nyalandu ameruhusu Tanzania Game Trackers Safari (TGTS) kumilikishwa vitalu vinane pamoja na eneo la wazi na hivyo kukiuka kifungu cha 38(7) cha sheria ya wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 pia si za kweli.
Ukweli ni kuwa kampuni ya Tanzania Game Trackers Safari (TGTS) ndiyo iliyotumika kuwindisha familia ya Freidkin kwenye maeneo matano yaliyotajwa juu na si vitalu vinane kama ilivyoandikwa na gazeti la Jamhuri.
Vilevile kama ilivyoelezwa hapo juu kisheria, mtu mwenye leseni ya Rais ya uwindaji anaruhusiwa kuwinda eneo lolote linalofaa kuwinda kisheria bila kujali ukomo wa idadi ya vitalu.
Tuhuma hizi zilikuwa na nia ovu ya kuchafua, kudhalilisha na kushusha heshima ya Wizara ya Maliasili na Utalii, na Mheshimiwa Waziri Nyalandu na familia ya Freidkin
f) Tuhuma ya kuwa Waziri Nyalandu ameruhusu uwindaji wa kitalii kufanyika eneo la Makao, sehemu ambayo haijatengwa kama kitalu pia si za kweli.
Tuhuma hizi zinalenga kuchafua jina zuri la Mheshimiwa Waziri na kumpunguzia dhamira, Hari na kasi ya kupambana na ujangili.
Ukweli ni kuwa, eneo la Makao pamoja na kwamba halijatengwa rasmi kama kitalu cha uwindaji, lakini kisheria linaruhusiwa kufanyika shughuli za uwindaji (yaani kwa lugha iliyozoeleka – kuwindwa) kama ilivyo kwa maeneo mengine ya mapori tengefu na mapori ya wazi. Hii ndiyo maana familia ya Freidkin haikugawiwa vitalu bali ilipewa kibali cha kuwinda katika maeneo yaliyotajwa.
Makao Open Area: Eneo hili ndilo ambalo limekuwa likiitwa Mwiba Wildlife Ranch. Jina la Makao Open Area limetumika kupotosha watu ili wasijue kilichokuwa kinaendelea. Nyalandu anadanganya kwamba eti Leseni ya Rais inaruhusu uwindaji kufanyika popote! Si kweli, uwindaji wa kitalii unafanyika katika vitalu vilivyotengwa kisheria tu. Mwiba Holdings wamekuwa wanaliita Eneo hilo Mwiba Wildlife Ranch na wamekuwa wakitaka haki ya matumizi (user rights) ili kulitumia eneo hilo kwa ajili ya uwindaji na utalii wa picha. Awali walimwandikia Balozi Kagasheki ambaye aliwajibu kuwa isingewezekana kupata user rights kwa kuwa kanuni za ranchi zilikuwa bado hazijatoka. Baada ya kukwama kwa Waziri, wakarudi kwa Mkurugenzi, lakini sababu zikawa hizo hizo huku wakiahidiwa kufanya subira kwani tayari zilikuwa zimefikia hatua nzuri. Kwa kuelewa kuwa walikuwa hawakidhi vigezo, walimtumia mmoja wa washauri wao kumshawishi Mkurugenzi kutoa vibali lakini wakakwaa kisiki. hapo ndipo walipomtafuta Nyalandu ambaye alimwita Mkurugenzi na kushinikiza kuwa atoe vibali kwa rafiki zake hao. Mkurugenzi alimkatalia Nyalandu na kueleza madhara ya kutoa vibali hivyo. Aidha, alimshauri Nyalandu awasiliane na Waziri ambaye tayari alikataa ombi hilo. Leo hii Nyalandu, baada ya kupata Uwaziri kamfukuza Mkurugenzi na Msaidizi wake. Zaidi, katoa kibali uwindaji ufanyike katika eneo hili ambalo halina sifa kama kitalu cha uwindaji. Je, sio kweli kwamba karuhusu uwindaji ufanyike katika eneo ambalo si kitalu?
2. Katika gazeti Jamhuri la tarehe 30 machi 2014 toleo namba 129 ilichapishwa taarifa potofu yenye kichwa cha habari NYALANDU ’ AUZA’ HIFADHI
· Yeye na lembeli waenda afrika kusini kukamilisha mpango
· Katibu mkuu njia panda alazimishwa kuidhinisha safari, posho
· Hifadhi nyingine nazo mbioni kutolewa kwa wawekezaji
Taarifa hiyo potofu ilielezea kuwa Waziri Nyalandu alikwenda nchini Afrika ya Kusini na kufanya mazungumzo na kampuni ya African Parks Network (APN) kwa ajili ya kuikabidhi uendeshaji wa Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu ikiwemo kuuza hifadhi ya Katavi.
Tuhuma hizi si za kweli.
Tuhuma hizi zililenga kuchafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na kumchafua mheshimiwa Lazaro Nyalandu, Waziri wa Maliasili na Utalii.
Ukweli ni kuwa Safari ya Waziri Nyalandu kwenda Africa kusini ilikuwa rasmi na ilifuatia maagizo ya Serikali kuhudhuria mkutano wa African Parks Network (APN) wa uhifadhi ulioandaliwa na asasi hiyo kwa lengo pia la kuhakiki uwepo, utendaji halisi wa taasisi hiyo na kufanya majadiliano kuhusiana na mapendekezo yao.
Huu ni utaratibu wa kawaida wa utendaji serikalini ambapo taarifa ya safari hiyo iliwasilishwa Serikalini kwa hatua zaidi.
Katika mkutano huo, hakukuwa na mikataba yoyote iliyowekwa na Waziri Nyalandu au maamuzi yoyote ya kukabidhi hifadhi za Taifa kama ilivyoelezwa na gazeti la Jamhuri.
Tuhuma hizo zilizolenga kuchafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na Mhe. Nyalandu.
Tunasisitiza kwamba huu ulikuwa mpango mchafu wa Lembeli na Nyalandu kukabidhi hifadhi zetu kwa makaburu wa Afrika Kusini. Nyalandu alikana kuwa hakwenda kukabidhi Katavi bali alitumwa na Waziri Mkuu kukutana na African Parks Network (APN) kujua jinsi wanavyofanya kazi! APN ndio hao hao wanaotaka kukabidhiwa mbuga zetu!
Tunajua kuwa tarehe 24 Machi Nyalandu alikutana na wataalamu bingwa wa uhifadhi nchini wakamtahadharisha juu ya matatizo ambayo APN imeleta kwenye nchi nyingine. Tunajua kwamba Nyalandu hakutaka kusikia habari za wataalamu hawa na kwamba ni Katibu Mkuu aliyesisitiza kwamba lazima waitwe wam-brief kabla hajaenda huko Afrika Kusini. Pamoja na mawasilisho mazuri na ya wataalamu waliopewa kazi ya kufanya uchambuzi na kutoa mapendekezo, Nyalandu aliondoka na rafiki zake akiwemo Lembeli kwenda huko Afrika Kusini.
Hili lilipojitokeza Bungeni akadai kuwa eti alitumwa na Waziri Mkuu. Hivi kama kweli alithamini kazi nzuri iliyofanywa na wataalamu, baada ya kujua matatizo ya APN isingetosha yeye kumshauri Waziri Mkuu juu ya utata wa asasi hii? Je, kulikuwa na uhalali gani kusafiri na msafara mkubwa wa watu sita kwenda huko kwa siku nne eti kujua tu mfumo wa utendaji wa APN? Je, kulikuwa na sababu gani kumlipia Lembeli ambaye ni mjumbe wa Bodi ya APN kwenda huko kama mmoja wa wajumbe wa Tanzania? Mgogoro wa maslahi uliachwa wapi hapa? Je, Lembeli naye hajui utendaji wa Asasi hii ambayo yeye ni mjumbe wa Bodi?
Lakini pia ukweli kwamba APN ndio waliokuwa wanataka Hifadhi zetu kwa udi na uvumba, na hifadhi zenyewe ziko Tanzania; kulikuwa na uhalali gani kutumia mamilioni ya walipa kodi kuwafuata huko? Hapa ndipo tulipowahi kuhoji, inakuwaje baba wa binti kugharamika kusafiri kumfuata mchumbiaji kwake, eti kumwambia tu kwamba hataki binti yake aolewe naye?
Tunaelewa kuwa Nyalandu bado hajakata tamaa. aliporejea akaanza mbinu za kutuma watu wakiwemo wabunge kutembelea nchi mbalimbali ambapo APN imewahi kufanya kazi. Hivi hapa inatumika akili au matope? APN walishindwa wakafukuzwa huko, anatuma wanasiasa waende kujifunza ili kuhalalisha kusudio la kuwakabidhi APN mbuga zetu! Hapa hamna uhuni? Kwa nini tusihoji!
Suala zima la APN ni ufisadi. Nyalandu anafanya akijua kwamba atafaidika yeye na rafiki yake Lembeli ambaye alikanusha kwamba hakwenda Afrika Kusini kiasi cha kufikia kwenda mahakamani. Hata hivyo, baada ya JAMHURI kuonyesha vielelezo kwamba alikuwa huko Lembeli akafunga mdomo na kesi aliyofungua imekufa kifo cha kawaida.
3 Gazeti la Dira jumatatu, Machi 31 – April 6, 2014, liliandika habari yenye kichwa cha habari “Kashfa za Nyalandu zatikisa. Na vichwa vidogo vya habari vilivyosomeka, Adaiwa kumiliki vitalu, kampuni ya “tours”, Aificha chini ya mwamvuli wa Wachina.
Tuhuma hizi si za kweli.
Tuhuma hizo zina nia ovu ya kuchafua jina la Mheshimiwa Waziri Nyalandu na kupunguza kasi yake ya kupambana na ujangili.
4 Taarifa ya kuwa Waziri Nyalandu anatuhumiwa kurefusha msimu wa muda wa uwindaji kuanzia Julai Mosi hadi Machi 30 ambapo ni sawa na muda wa miezi tisa kila mwaka tofauti na muda wa kisheria ambao ni kuanzia Julai Mosi hadi Decemba 31 sawa na miezi 6 kwa mwaka si za kweli.
Ukweli ni kwamba Waziri Nyalandu alitangaza kusudio la kuongeza msimu wa uwindaji kutoka miezi sita kwenda tisa na hii iko ndani ya mamlaka ya waziri kisheria kama ilivyo kwenye Sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 na kanuni zake.
Hii siyo mara ya kwanza kwa mawaziri wenye dhamana ya Maliasili na Utalii kurefusha au kufupisha msimu wa uwindaji.
Hapa ndipo Nyalandu anapokosea. Kuwa na dhamana maana yake si kujifanyia mambo unavyojisikia. Dhamana maana yake ni kuhakikisha kuwa mambo yana fanyika kwa kuzingatia weledi na misingi sahihi. Nyalandu anatakiwa aje na hoja za kisayansi kwa nini alitaka kufanya hivyo, tena kwa kiburi hata baada ya kushauriwa na wataalamu wake. Kama dhamana maana yake ni waziri kujifanyia anavyotaka basi hatuna sababu ya kuwa na watendaji, wataalamu, bodi na mamlaka za kisayansi kama vile TAWIRI. Ukweli unabaki pale pale kwamba Nyalandu anatumiwa vibaya na kwa maslahi yake binafsi na wafanyabiashara, hasa kwa kuwa wafanyabiashara hawa wa tasnia ya uwindaji wamekuwa wakishinikiza muda mrefu kurefushwa msimu wa uwindaji. Mtangulizi wake, Balozi Kagasheki, ndiye aliyefupisha msimu wa uwindaji kufuatia ushauri wa kitaalamu. Nyalandu, alikuwa naibu wake lakini hakuthubutu kushauri juu ya hili kwa kuwa hakuwa na hoja za msingi. Hapa huhitaji digrii ya uzamili kujua kwamba, wakati Balozi Kagasheki anaongoza wizara kwa kuzingatia matakwa ya kisheria na kisayansi, Nyalandu alikuwa na wenye makampuni wakipanga namna ya kumhujumu Kagasheki na kumkwamisha kiutendaji.
5 Tuhuma ya kuwa Waziri Nyalandu ni mmoja wa wafanyabiashara wa Uwindaji na yuko karibu kabisa na wawindaji wenye vitalu nchini hazina ukweli wowote.
Waziri Nyalandu ni waziri mwenye dhamana ya kusimamia masuala yote ya Maliasili na Utalii na anapaswa kuwa karibu na wadau wote wa maliasili na Utalii ili kuweza kusimamia vema sekta hiyo. Huwezi kuisimamia vema Sekta husika kwa kuwakwepa wadau husika.
Ni kweli waziri hatakiwi kuwakwepa wadau. Hata hivyo, kuna ukaribu na ukaribu. Ukaribu wa kufadhiliwa ndege kwa matumizi binafsi ni ukaribu gani? Ukaribu wa kupokea amri ili kuvunja sheria za nchi ni ukaribu gani? Ukaribu wa kulazimishwa kufukuza kazi watendaji waadilifu na kuweka watu watakaotii amri za matajiri ni ukaribu gani? Ukaribu gani wa kulazimishwa kukiuka kwa makusudi haki za wawekezaji wengine?
Lakini la kustaajabisha zaidi ni pale Nyalandu anapodai kuwa hawezi kusimamia vema sekta bila ukaribu na wadau wakati anawakwepa watendaji wizarani kwake. Anasahau kuwa watendaji hawa ndani ya wizara ni wadau pia. Nyalandu anataka kutuaminisha kuwa anaweza kusimamia vema Sekta kwa kufunga ndoa na TGTS bila kuongea na Katibu Mkuu wa Wizara? Mfano ni taarifa hii anayoiita rasmi. Je, awe mkweli aseme ni nani Wizarani aliyehusika kuiandaa kama sio yeye na rafiki zake. Je, Nyalandu ana Wizara nyingine na kitengo cha Mawasiliano kingine zaidi ya pale Mpingo House?
6 Tuhuma ya kuwa Waziri Nyalandu anakabiliwa na kashfa ya kujihusisha na ujangili mkoani Singida pia si za kweli
Ukweli ni kuwa tuhuma hizo zina nia ovu ya kuchafua jina la Waziri Nzyalandu, kumshushia heshima na hadhi yake kwa lengo la kupunguza na kukwamisha jitihada zake za kukabiliana na ujangili uliokithiri hususan mauaji ya tembo na faru.
Jitihada zilizofanywa na Waziri Nyalandu hadi sasa ni pamoja na kutafuta fedha na vifaa ndani na nje ya nchi ikiwemo helikopta moja na kuwezesha kuanzishwa kwa mfuko maalum wa kukusanya fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo chini ya uratibu wa shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ofisi ya Tanzania.
Nyalandu analazimisha umma kuamini kuwa utendaji bora ni pamoja na kuwa omba omba. Angetusaidia sana kama angetufahamisha kiasi cha fedha za umma anachotumia na kile anachopata kutokana na kuombaomba. Anatumia shilingi ngapi kwa uzururaji nje ya nchi? Safari za Arusha na Dar es Salaam kila siku akiwa nchini zinagharimu shilingi ngapi? Na vyumba vya kudumu alivyo navyo kwenye hoteli za nyota tano vinalipiwa shilingi ngapi na nani? Huwezi kupoteza mabilioni na kuzalisha milioni kadhaa halafu ujinadi hadharani kwamba umeleta mafanikio.
Nyalandu atufafanulie juu ya ule usanii ulioripotiwa na vyombo kadhaa vya habari kwamba alipokea hundi hewa na ndege iliyochakaa kutoka kwa marafiki zake kama njia ya kuonesha kuwa yuko makini katika kupambana na majangili. Je; tulitarajia hundi hewa na ndege chakavu vipunguze ujangili kwa kiwango gani? Usanii huu ulikuwa na nia gani kama siyo hadaa ili aonekane kama mchapakazi.
Nyalandu anajivunia kutafuta vifaa na helikopta kwa ajili ya kupambana na ujangili. Tunataka kujua kuwa vifaa hivi mpaka sasa vimetumika wapi na lini kupambana na ujangili.
Misaada ya Buffet ina utata mkubwa sana na mambo yaliyojificha. Kwanza ni juu ya jaribio la kuweka kipengele kwenye Mkataba na Mfadhili huyu kwamba misaada itatolewa endapo tu NYALANDU AENDELEE KUWA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII. Je, huku siYo kuuza nchi? Mfadhili huyo ana nguvu na jeuri kiasi gani hadi afikie hatua ya kumuamuru Rais juu ya nani anamtaka yeye kuwa waziri? Ana maslahi gani hasa na Nyalandu? Nyalandu alifahamiana wapi na huyu Mmarekani? Baba wa Taifa alikataa katakata misaada yenye masharti. Leo Nyalandu anatuletea Mzungu anayemlazimisha Rais la kufanya juu ya uteuzi! Kamwe hatuwezi kukubali.
Aidha, tunahitaji maelezo kuhusu Binti wa Kitanzania ambaye Nyalandu alimtambulisha kwa Howard Buffet kuwa anafanya kazi ofisi ya Rais, Ikulu. Hata hivyo, Nyalandu huyu huyu amekuwa akimtambulisha binti huyu kuwa ni mwajiriwa wa Howard Buffet anayeratibu misaada ya tajiri huyo hapa nchini. Kuna nini kimejificha hapa? Ama, kuhusu hiyo helikopta, tunajua kuwa kulikuwa na fursa za watumishi wa Idara kwenda kujifunza urubani Marekani. Matokeo yake Nyalandu alikataa katakata kuwaendeleza watumishi na kuamua kupeleka watoto watano wa rafiki zake wakiwamo wawindaji Marekani. Watoto hawa hawajaajiriwa. Je, kwa nini tusiamini kuwa nafasi hizo zimeuzwa na kwamba hiyo inatumika kama mbinu ya kuwapatia ajira watoto wa rafiki zake? Tunaomba Nyalandu akanushe habari hizi pia.
7 Kashfa za kumhusisha Waziri Nyalandu na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwanyonye, Rehema Manji kudai kuwa alitishiwa bastola ni kosa kisheria kwani. Waziri Nyalandu hakuwahi kutenda kosa hilo.
Kutajwa kwa mmiliki wa gari namba T 505 BKM kuwa ni la ndugu Lazaro Samwel Nyalandu, mwenye utambulisho wa mlipa kodi (Tin: 105-059-701) si uthibitisho ya kuwa Waziri Nyalandu alihusika kumtishia bastola Rehema Manji. Kashfa hizo zililenga kumchafua, kumshushiaa hadhi Waziri Nyalandu.
Huu ni ubabaishaji. Hivi gari, tena ya binafsi, inaweza kutenda kosa yenyewe bila mhusika? Ofisa Mtendaji alitishiwa kwa bastola na kizuizi kilivunjwa. Gari iliyohusika ilitambuliwa na kwamba alitoka mtu ndani akamtishia mhusika kwa bastola. TRA wakathibitisha kuwa mwenye gari ni Lazaro Samwel Nyalandu. Baadaye kesi ikamalizwa kwa mazingira ya kutatanisha, pengine rushwa ilitumika kuizima. Na gari hiyo ilikuwa na mzigo usioeleweka na bila shaka ni mzigo haramu na ndio maana mhusika hakutaka ukaguliwe. Kama Nyalandu anadai kuwa hakuhusika ni juu yake kututajia watu aliowaazima gari lake ambao wamehusika na uhalifu uliotajwa. Kama si yeye mwenyewe basi ina maana anashirikiana au anawatuma kufanya uhalifu.
8 Katika gazeti la Jamhuri la Jumanne October 07 – 13, 2014 ISSN No. 1821-8156 Toleo No. 157, zilichapishwa taarifa zenye kichwa cha habari AUNTIE EZEKIEL ATANUA NA NYALANDU MAREKANI.
Tuhuma hizi si za kweli. Tuhuma hizi zimetolewa na watu wenye nia ovu na zimelenga kuchafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na kumchafua mheshimiwa Waziri Lazaro Nyalandu, kumshushia Heshima, kumdhalilisha kwa umma ili kumpunguzia dhamira, malengo na kasi ya kupambana na ujangili.
Ukweli ni kuwa, Waziri Nyalandu hakuhusika kwa namna yoyote ile na kile kilichoelezwa na gazeti la Jamhuri “Aunty Ezekiel atanua na Nyalandu Marekani” kichwa cha habari hiyo na vichwa vidogo vya habari vilivyoandikwa vililenga kutoa picha potofu kwa umma ili kumchafua, kumdhalilisha, na kuvuruga amani kwa Waziri Nyalandu na familia yake.
Waziri wa Maliasili na Utalii, akiwa nchini Marekani kikazi, alialikwa kuhudhuria shughuli ya kutimiza miaka minne ya blog ya Vijimambo ambayo inamilikiwa na Watanzania waishio Marekani.
Waandaaji wa shughuli hiyo iliyolenga kutangaza Utalii wa Tanzania nchini Marekani walimwalika Waziri Nyalandu kuwa mgeni rasmi. Mwaka jana kwenye sherehe kama hizo alialikwa Rais mstafu Ali Hassan Mwinyi
Wizara ya Maliasili na Utalii haikuhusika na uratibu wa safari ya Msanii Auntie Ezekiel.
Tarifa hizo zimelenga kuchafua Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Mheshimiwa Waziri Lazaro Nyalandu.
Tuhuma za ufisadi, ujangili na matumizi mabaya ya madaraka hazina ukweli wowote. Tuhuma hizo zinalenga kudhoofisha kasi ya Waziri Nyalandu katika kupambana na ujangili.
U-Miss na ujangili una uhusiano gani?? Je, huko Marekani Nyalandu alikwenda kupambana na ujangili? Awali alidai kwamba kuna watu wanamsogezea wasichana apige picha nao, halafu zitengenezwe kwa kompyuta ili kumchafua. Alipoona uongo huo haukubaliki akasema alikutana na Aunty Ezekiel usiku kwenye hafla. Habari zilipoandikwa akamzuia Aunty asizungumze na wanahabari. Ikumbukwe kuwa msichana huyo alisema safari hiyo iligharimiwa na Nyalandu, na wale wa vijimambo blog walikuwa kisingizio tu. Mwingine mwenye ziara hiyo, aliyelipiwa, Kassim Mganga, amethibitisha kuwa safari yote iligharimiwa na Nyalandu.
Mganga amenukuliwa kwenye Gazeti la Serikali la Habari Leo, Toleo Na 02864 la Oktiba 23, 2014 akisema yeye na Aunty Ezekiel walipelekwa nchini Marekani na Waziri Nyalandu. Ukweli umeshajulikana.
Lakini pia ni wakatiu wakiwa huko, Nyalandu alijificha ili asionwe na Rais Jakaya Kikwete, lakini taarifa zikamfikia mkubwa huyo wa nchi. Nyalandu akahofu na kutaka kutimka, lakini ni Waziri mmoja (tunamhifadhi) aliyemshauri amsalimu Rais kwani kutofanya hivyo ilikuwa ni utovu wa nidhamu. Rais alikasirika kumuona Nyalandu akiponda raha Marekani wakati akiwa ameagiza mawaziri wote wawepo Dodoma katika Bunge Maalum la Katiba. Baada ya kumsalimu Rais, Nyalandu aliondoka haraka haraka kurudi Dar es Salaam.Nyalandu kama si muumini mnafiki, ajitokeze ayakane haya.
9 Hoja ya kuwa waandishi wa habari wameshinda na kuwa wameokoa mamilioni ya fedha za umma ambazo zingetumika kulipia mkutano na badala yake mkutano huo ulifanyikia wizarani hazina msingi.
Hoja hizo si za kweli kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Nyalandu anatumia kumbi za wizara kufanya mikutano na wadau.
Mikutano ya wizara ya Maliasili na Utalii inayofanyikia kwenye kumbi za mikutano nje ya wizara, inafuata taratibu zote za Serikali na inategemeana na idadi ya washiriki wa mikutano hiyo na aina ya mkutano husika.
Utaratibu huu ni wa kawaida na hutumiwa na watendaji na viongozi mbalimbali wa Serikali na si upotevu wa fedha za umma kama inavyodaiwa na magazeti husika bila kujua uhalisia wa mikutano, idadi ya watu watakaohudhuria mkutano , na wadau wa mkutano husika.
Mikutano hii imekuwa na manufaa makubwa kwa taifa katika swala zima la kupambana na ujangili
Mikutano ambayo JAMHURI imekuwa inahoji ni ile mikutano ya mara kwa mara ambayo Nyalandu amekuwa akifanya na waandishi wa habari. Mikutano hii imekuwa ikifanyika Serena na Sea Cliff na imekuwa haina jipya zaidi ya kujitangaza yeye ili aonekane kuwa ni mchapakazi. Inapotokea mkutano mmoja tu kugharimu milioni tatu wakati ungeweza kufanyika kwenye ukumbi wa Wizara, basi hapo hamna lugha ya mbadala zaidi ya ubadhirifu na kutaka kuonesha ufahari. Sasa kama kutokana na kufichuliwa ubadhirifu huu, Nyalandu sasa ameona aibu na kufanyia Mkutano wizarani kwanini tusiamini kuwa tumechangia kuokoa mamilioni ya fedha za umma? Aeleze faida zilizopatikana kwa kumleta mwandishi wa Daily Mail, Martin Fretcher ambaye alimgharimia daraja la kwanza ndani ya ndege na kumlaza katika hoteli ya hadhi ya nyota tano, lakini mwisho wa siku ‘akaitukana Tanzania’. Tunamsema Nyalandu kwa sababu ni mtu anayetumia vibaya madaraka na fedha za umma.
10 Tuhuma ya kuwa waziri anafanyia kazi hotelini si za kweli kwa sababu kiongozi wa serikali wa ngazi za juu anakuwa kazini muda wote bila kujali yuko wizarani ama nje ya wizara.
Tuhuma hizo zinalenga kuchafua jina zuri la Waziri Nyalandu, kumkatisha tamaa na kumpunguzia heshima yake kwa umma ili kupunguza kasi yake ya kupambana na ujangili.
Haya ndiyo majibu ya kiongozi wa juu wa Serikali! Kwamba anahamishia ofisi hotelini kwa kuwa ni kiongozi wa juu wa Serikali na anaweza kufanyia kazi popote! Kwanza si sahihi kudai kuwa anafanyia kazi hotelini. Usahihi ungekuwa kwamba Waziri ni mzururaji hotelini kwa kuwa hata hiyo kazi inayodaiwa kufanyika haionekani! Kama kweli angekuwa anafanyia kazi hotelini na kazi za wizara zikawa zinaenda vizuri isingekuwa tatizo; lakini kuna ushahidi kwamba mambo pale wizarani hayaendi. Lakini pia ni vema tukajua, kwa kupenda kwake kuishi hotelini, gharama hizi analipa nani? Kama siyo Wizara, basi atakuwa analipiwa na mafisadi, ambao sitakosea kuamini kuwa ndio wanaovuruga sekta ya maliasili nchini.
Itakumbukwa kuwa Siku chache zilizopita Waziri mwenzake, William Lukuvi, alimlalamikia Nyalandu hadharani kwa kutokujibu barua na kutokuonekana ofisini. Wanakijiji kutoka Iringa wamefika mara tatu wizarani bila kufanikiwa kumuona Nyalandu. Lukuvi anadai kumtafuta kwa simu na kuandika barua nne kwake bila kupata majibu! Ni wazi kuwa Lukuvi alishindwa kumvumilia Nyalandu kutokana na shinikizo alilokuwa anapata kutoka kwa wapigakura wake. Hata hivyo, Nyalandu badala ya kumuona Waziri Lukuvi na kulielewa tatizo, aliamua kutoa majibu ya hovyo kupitia vyombo vya habari. Katika hali ya uafrika, majibu ya Nyalandu kwa Lukuvi hayakustahili kutokana na umri na uzoefu wa Lukuvi serikalini kulinganisha na Nyalandu.
Huo ni mfano mmoja tu. Je, ni wangapi wanakosa huduma ya waziri kutokana na utoro na uzururaji wa Nyalandu? Anataka tuamini kuwa yeye akiwa angani, klabuni, kwenye ngoma na hata akiwa anatanua na vimwana basi yuko kazini?
Aidha, ni wazi kuwa kitendo cha waziri kukosekana ofisini kwa muda mrefu kinasababisha uamuzi wenye athari hasi kwa sekta. Waziri anasoma lini sheria, taratibu na miongozo mbalimbali? Anapata wapi na lini ushauri wa watendaji na wataalamu wake wakati saa zote yeye ni kiguu na njia? Tumeona uamuzi wa hovyo aliyofanya na matokeo yake ni kashfa na tuhuma hizi ambazo yeye anadai kuwa si za kweli na kwamba: “zinalenga kuchafua jina zuri la Waziri Nyalandu, kumkatisha tamaa na kumpunguzia heshima yake kwa umma ili kupunguza kasi yake ya kupambana na ujangili.”
Matokeo ya Nyalandu kukosekana ofisini, ni yale yaliyotokea kwenye Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ambako wabunge walimjia juu baada ya kuwasilisha taarifa dhaifu. Ingawa rafiki yake, Lembeli alimtetea kama kawaida yake, ni wazi kuwa Nyalandu alikurupuka na hakuelewa kilichoandikwa. Ataelewa wapi wakati hayuko ofisini? Shukrani ziwaendee wajumbe makini wa Kamati ambao wameapa kutoburuzwa na maslahi binafsi ya Lembeli.
Inawezekana waziri asiwe ofisini, lakini kama katika siku 100 anaonekana ofisini kwa siku 10 tu basi hii ni hatari. Hii imekuwa tabia yake tangu akiwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara ambako alipotea na Wizara kubaki bila waziri kwa miezi kadhaa wakati waziri wake, Dk. Cyril Chami, alipokuwa kwenye matibabu nchini India. Nyalandu akaendeleza utoro huo wakati akiwa Naibu wa Balozi Kagasheki, ambako ilikuwa inapita miezi mitatu bila Waziri kujua alipo Naibu wake! Kuanzia mwezi Julai hadi Septemba, Nyalandu ametumia muda wake mrefu nchini Marekani. Ingawa amekuwa akienda na kurudi, lakini aliporejea amekuwa hamalizi wiki nchini. Ni nini hasa anachofuata huko, na kwa pesa za nani?
Hadi sasa kuna mafanikio makubwa yaliyojitokeza katika suala zima la kupambana na ujangili ikiwemo Kupungua kwa kiasi kikubwa kwa mauaji ya tembo. Idadi ya tembo katika ikolojia ya Serengeti – Maasai Mara imeongezeka, kupungua kwa matukio ya ujangili katika Pori la Akiba Selous kuanzia mwezi machi 2014 hadi sasa, wadau wengi kujitokeza katika kusaidia suala zima la kupambana na ujangili wa wanyamapori nchi kama Marekani, Ujerumani, China, Uingereza.
Ukweli ni kwamba Nyalandu ni mwepesi sana wa kusahau. Atakalosema leo silo atakalosema kesho. Kwa hiyo hicho anachokiita mafanikio hatuna uhakika nacho kwa kuwa kesho anaweza kukikana.
Kwa mfano, Septemba 9, mwaka huu, Nyalandu huyu huyu anayejivunia mafanikio makubwa katika kupambana na ujangili aliuambia Mkutano wa Wadau wa Maendeleo ya Kupambana na Ujangili uliofanyika Dar es Salaam kuwa ujangili umekithiri. Leo hii anasema umepungua. Tushike lipi?
Ni Nyalandu huyu huyu, akiwa na mteule wake Paul Sarakikya, alitangazia umma siku ya Jumatatu ya Machi 31, mwaka huu kuwa Wizara yake imefanikiwa kupunguza ujangili kwa asilimia 58, katika kipindi chini ya siku 60 tangu ateuliwe kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii. Tujiulize, inakuwaje katika siku zisizozidi 60 apunguze tatizo kwa asilimia 58 ashindwe kumaliza asilimia 42 katika siku zaidi ya 160, badala yake tatizo likithiri kama alivyotamka Septemba 9? Na inakuwaje, mwezi mmoja tu baada ya kutujuza kuwa tatizo limekithiri atuambie kuwa tatizo limepungua? Imekuwa homa ya vipindi hii?
Itakumbukwa kuwa si mara moja wala mbili tu Nyalandu kulalamikiwa kwa kutokujua vipaumbele vya wizara yake. Nathubutu kusema bila kutafuna maneno kwamba Nyalandu haoni ujangili kama tatizo. Nyalandu anachukulia dhamana ya uwaziri kama fursa ya kutangaza utukufu wake na kujipatia ukwasi. Ndio maana hata mikakati yake na mafanikio anayotutangazia kwenye runinga kila siku ni utata mtupu Kwake yeye ni utukufu na fedha, basi.
Wizara ya Maliasili na Utalii inatoa taarifa kwa umma kwamba tuhuma zote zilizotolewa na hata zitakazoendelea kutolewa na gazeti la Jamhuri dhidi ya Wizara ya Maliasili na Utalii na dhidi ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Lazaro Nyalandu zinalenga kulichafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na pia kuchafua jina la Mheshimiwa Waziri Lazaro Nyalandu na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya gazeti la Jamhuri na chombo chochote cha habari kitakachotoa taarifa za kuchafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Lazaro Nyalandu.
Sisi kama JAMHURI tunajua kuwa kazi hii ya kuweka hadharani uovu na ufisadi ni ya hatari sana. Tunajua kuwa roho zetu ziko hatarini na kwamba mafisadi wana pesa chafu wanazoweza kuzitumia kununua wanasiasa, waandishi wa habari na hata majambazi kuwashughulikia wale wanaosema ukweli.
Tunajua kuwa Nyalandu ana fedha, tena nyingi. Lakini tunaamini kuwa pesa alizonazo ni pesa chafu. Amejitahidi, pengine kwa kutumia pesa hizo hizo chafu, kushawishi kupata madaraka aliyo nayo. Madaraka haya anayatumia kutishia watu ambao anafikiri kuwa ni tishio kwake.
Msimamo wetu, sisi kama JAMHURI, ni kwamba tumejitoa nafsi zetu kupigania maliasili na rasilimali zetu ili zisifujwe na zitumike kwa manufaa ya wote. Tutaendelea kuandika bila kuogopa vitisho vya Nyalandu. Tuko tayari kufa katika hili, ila tunaamini kuwa wapo watakaoendelea kupigania rasilimali hizi, hata kama watakuwa wachahce na mwisho ushindi utapatikana.
Aidha, tunapenda kusisitiza kuwa hatutaonea mtu. Hatumwandiki Nyalandu kwa sababu ya kuchukia kabila lake, dini yake, sura yake au utajiri wake. Tabia na mwenendo wake ambao una athari kubwa kwa maslahi ya nchi ndivyo vinavyogomba.
Tunasisitiza kuwa hatuna ugomvi na mtendaji yeyote wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Tuhuma ambazo zimekuwa zikitolewa zimekuwa za Nyalandu kama mtu binafsi na wala si za Wizara. Tunaamini kuwa ukosefu wa maadili ambao amekuwa akiufanya Nyalandu amekuwa akiufanya kama mtu binafsi na wala hafanyi kwa niaba ya Wizara. Kwa hiyo ni upotoshaji mkubwa kuudanganya umma kuwa Wizara inachafuliwa. Nyalandu ni Waziri na wala sio Wizara. Tumetumia muda kujibu porojo hizi si kwa sababu zina ukweli, bali kwa sababu zikiachwa zitaaminiwa. Aidha, tumezijibu ili kuwaonesha hao waliomwandalia (bila nembo, kumbukumbu wala sahihi ya mhusika)kuwa tunapodhamiria kuandika habari za uchunguzi, ni za uchunguzi kweli. Haya ni mapambano halali ambayo bila shaka Watanzania wengi watatuunga mkono Si mapambano dhidi ya Nyalandu, bali ni mapambano dhidi ya hujuma na uongozi mbovu wa Nyalandu ndani ya Wizara hii nyeti..
MWISHO;
Tunajua kuwa Nyalandu amelazimika kujibu tuhuma hizi za muda mrefu leo kutokana na sababu kubwa mbili:
- Kibano alichopata kutoka kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ambao walikataa kuburuzwa na Mwenyekiti wao aliyetaka kumkingia kifua rafiki yake Nyalandu. Tuwapongeze wabunge hawa kwa uzalendo.
- Woga wa kikao cha Bunge cha mwezi Novemba. Tunaamini kuwa majibu ya tuhuma hizi ni moja ya mikakati yake kuhakikisha kuwa anajisafisha kuepuka kibano cha wabunge wazalendo ambao wameapa kumshughulikia kutokana na kashfa zinazomkabili. Mikakati mingine anayofanya ni kutumia vyombo vya habari kujikweza na kuonesha kuwa ni waziri makini, mwenye busara, mcha Mungu na mchapakazi; kutuhumu watendaji wa wizara yake na hata mawaziri wenzake na wakubwa wengine serikalini kuwa wanamchafua kutokana na utendaji wake mzuri; kuzunguka nchi nzima huku akijaribu kuwaweka sawa baadhi ya wanasiasa na kuahidi misaada kwenye majimbo yao nk. Tunajua kuwa kuna wanasiasa ambao tayari wamenasa katika mtego huu wengine wakimsifu na kuapa kupambana na mbunge yeyote atakayejaribu kumsema Nyalandu. Inatia simanzi kwamba mmoja wa wanasiasa hao ni waziri na eti anaunga mkono kuwa Nyalandu anaandamwa kutokana na uchapakazi wake. Lakini ajabu ni kwamba waziri huyo ambaye anaamini kuwa kuandamwa ni kigezo cha utendaji bora bado yuko serikalini! Kama kuandamwa ni kigezo na yeye hajaandamwa kama Nyalandu kwa nini asijihesabu kama mzigo na kuachia ngazi? Hatujui kwamba Nyalandu kawapa nini, lakini ole wao wale wanaomkumbatia na kuamua kuwasaliti Watanzania, huku wakijifanya kuwa ni watetezi wao.
Pamoja na mikakati hii ya Nyalandu kujikosha, tunaomba kumkumbusha kuwa kuna tuhuma nyingine zinazomhusu ambazo Watanzania wangependa kupata majibu yake pia. Hizi ni pamoja na zile za kutumia mamilioni kugharamia ziara ya mwandishi wa gazeti Daily Mail la Uingereza na kuisababishia Serikali hasara na aibu kubwa; kujilipa posho tatu kwa safari moja; kutumia ndege ya serikali kama teksi yake kumleta Dar es Salaam na kumrejesha Arusha kila siku awapo nchini; mpango wa hujuma wa kufungua mpaka wa Bologonja; kutoa rushwa ya safari za nje kwa James Lembeli; kutumia muda mrefu na fedha za umma kwa safari za Marekani; kuwa jasusi la CIA; kushinikiza TANAPA kutoa Sh milioni 560 kugharimia Mashindano ya Miss East Africa na kutetea wakwepa kodi (Ahsante Tours) na kutaka kuingizia TANAPA hasara ya Sh bilioni 70 kutokana na mpango wake akishirikiana na wenye kampuni za utalii kushinikiza tozo iwe flat rate kwa hoteli zote bila kujali daraja. Tuhuma hizi pia zinahitaji majibu.
Aidha, Nyalandu awaeleze Watanzania sababu za jeuri na kiburi dhidi ya mamlaka za nidhamu na uteuzi akirejea sababu za kugomea na kukebehi uamuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu na yule wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma juu ya uhamisho wa watumishi aliowateua yeye. Nyalandu ana maslahi gani na watumishi hao ambao wamekuwa wanaaminika kuwa si wasafi?
TAARIFA HII IMETOLEWA NA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
Mwisho kabisa, hatuamini kama kiutengo cha mawasiliano chenye watu weledi kinaweza kutoa majibu na hoja dhaifu kama hizi. Tunashawishika kuamini kuwa haya ni maneno aliyoyaandaa Nyalandu mwenyewe na wapambe wake kwa malipo manono.