KILIMANJARO
Na Nassoro Kitunda
Hivi karibuni Chama cha ACT-Wazalendo kimetangaza waziwazi kuwa kitaendelea kunadi na kufanya ushawishi wa kudai Tume huru ya Uchaguzi na Katiba mpya kama sehemu pekee wanayoona italeta uchaguzi huru na wa haki.
Wamesema watashirikiana na vyama vingine vya upinzani wanavyoviita vyama rafiki katika kudai tume hiyo.
Pia hoja hiyo ni ya muda mrefu hasa kwa vyama vya upinzani kwamba wanaonyesha kila uchaguzi unapofanyika haukuwa huru na haki kwa sababu hakuna tume huru inayotenda haki kwa kila mtu.
Kwa hiyo ndiyo kilio kikubwa kwa vyama vya upinzani. Madai haya yalianza baada ya Tanzania kuingia katika siasa za mfumo wa vyama vingi na kuwa na dhana ya ushindani baina ya vyama.
Tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, malalamiko hayo yamekuwa ni sehemu ya siasa hizo.
Katika makala hii, nitaonyesha makosa yanayofanywa na wanaodai tume hiyo na kuacha sehemu kubwa ambayo kwa muda mrefu haizungumzwi, sehemu ya kufikiri sera gani, zitakazokwenda kugusa maisha ya walio wengi baada ya kuipata na uchaguzi kufanyika.
Tunaweka nguvu kubwa kuelekea uchaguzi kuliko maisha baada ya uchaguzi
Hoja hii imekuwa ikizungumzwa kila siku, kuwa unataka tume huru nayo ni muhimu lakini muhimu zaidi ni kufikiri baada ya kupata tume huru na uchaguzi kufanyika.
Kwa sababu vyama vya siasa vimekuwa vikitafuta upenyo wa kuingia Ikulu na njia mbalimbali lakini zimekuwa zikiipa kisogo hoja ya kutafuta sera na itikadi zitakazogusa wananchi walio wengi wanaohangaika na maisha ya kila siku.
Hili ni kosa linalofanywa kudhani kuwa tume huru pekee inatosha, bila kufikiri baadaye namna gani wananchi wanaweza kunufaika na maisha yao ya kila siku.
Vyama vya siasa vimeacha kuzungumzia masuala, muda wote vimekuwa vikizungumzia vitu vinavyowahusu wao na si wananchi.
Ndiyo maana kila miaka tumekuwa tukifanya uchaguzi lakini ile faida ya uchaguzi huo hazionekani kwa wananchi wa kawaida.
Siasa tulizo nazo zimefunga fikra za vyama vya siasa kudhani matatizo tuliyonayo yanasababishwa na siasa au utekelezaji, au masuala ya tume huru au kati na hivi, ndiyo masafa mafupi tuliyokuwa nayo.
Hili ni kosa kwa sababu shida yetu haipo katika siasa pekee, shida ipo katika mifumo ya uchumi, mifumo ya kibepari inayowaweka walalahoi pembeni wakati wote.
Lakini wanasiasa ni sehemu ya mfumo huo wa ubepari, wananufaika nao na ndiyo maana wanakubali hoja nyepesi kuwa shida ipo katika uchaguzi hivi au tume huru na kuacha sehemu pana ya shida zetu za msingi.
Uzoefu katika Bara la Afrika
Hoja ya tume huru, imepata umaarufu mkubwa katika siasa za Afrika na imekuwa ikizungumzwa. Hasa kipindi cha uchaguzi, malalamiko yamekuwa makubwa katika tume za uchaguzi.
Malalamiko haya ni ya muhimu lakini muhimu ni kufikiri kuwa na masafa marefu baada ya uchaguzi. Kwa hiyo kumekuwa na mabadiliko katika siasa za Afrika na baadhi ya vyama vya upinzani kupata nafasi ya kuongoza nchi lakini cha kushangaza hali bado zipo vilevile kama ilivyokuwa mwanzo.
Kwa hiyo, hoja si kuwa na tume huru na kuwa na uchaguzi wa haki, wananchi wanataka kuona baada ya uchaguzi na tume huru, maisha yao yanakuwa na ubora mkubwa.
Hivyo, uzoefu katika Bara la Afrika ni kwamba kuna nchi zimefanya uchaguzi na vyama vimefanikiwa kushinda vilivyokuwa muda mrefu havikushinda na madai yao yalikuwa tume huru, lakini walisahau kujadili na kuja na sera zinazowaendeleza wananchi na zimekuwa nyuma kuwanufaisha wananchi wao.
Tuna mfano wa Gambia anatoka Yahaya Jammeih anaingia Adama Barrow ni mafanikio, kisiasa chama hiki cha upinzani kushika madaraka lakini nini kimetokea baada ya hapo?
Hali ni ileile tu ya mtangulizi wake. Kwa hiyo suala si kushinda uchaguzi na kuwa na hoja ya tume huru, lakini je, umebeba falsafa ya wengi ya kunyanyua maisha ya wengi?
Hiki kitu hatukioni huko Gambia. Nchi nyingi tu Afrika hali iko hivyo. Na hii si kwamba Jameh alikuwa bora kuliko Adama, hapana. Wote wana masilahi sawa.
Uzoefu huu unatuonyesha kuwa lazima tufikirie zaidi ya tume huru na uchaguzi, tufikirie sera na mifumo ya kiuchumi inayoleta unafuu kwa wananchi wote.
Vyama vitafute tume huru lakini vifikirie mifumo inayowafanya watu kuwa maskini
Vyama vimekuwa vikiacha na vikidhani tume huru ni jambo la mwisho, bila kuwa na tafakuri ya kina ya kutazama mifumo ya uchumi inayorudisha nyuma maisha ya walalahoi.
Vyama lazima vijue historia ya maisha ya wananchi kuwa tupo kwenye mifumo ya uchumi inayowafukarisha na waone namna ya kubomoa mifumo hiyo ya kinyonyaji. Kimsingi, vipato vya wananchi vipo chini, watu wanashindwa kumudu matibabu, wakulima wanalia na kilimo, wachimbaji wadogo wa madini wanalia na leseni.
Masuala haya hayapewi kipaumbele kwenye hoja za wanasiasa wanaodhani tukiwa na tume huru na kufanya uchaguzi basi kila kitu kimemalizika.
Si kweli, mapambano bado yanaendelea, kama tukiwa na tume huru, na bado tukiwa na fikra kuwa mifumo ya uchumi ya soko ndiyo dira yetu, tume huru hiyo haitakuwa na msadaa wowote katika maendeleo ya wananchi.
Kwa hiyo, vyama vinavyofikiria tu uchaguzi na kufanya marekebisho kuelekea uchaguzi vitakuwa vina maono ya masafa mafupi tu yasiyokuwa na tija kwa wananchi.
Kwa sababu havitakuwa vinalenga sababu ya matatizo yetu, kwanini tupo hapa? Nini kimesababisha haya yatokee? Kama vinashindwa kufikiri maswali haya na namna ya kuyajibu, basi itakuwa ni siasa za muda mfupi tu.
Ndicho kinachoendelea ulimwenguni, tumeacha kujadili tena kutazama historia yetu na sababu zilizotufikisha hapa tumekuwa watu wa kudai matukio, wala si mambo yatakayowafanya wananchi kufikiri hatima ya maisha yao.
Kwa ufupi, kama hatutaangalia kwa umakini hoja nilizoeleza hapo juu, siasa zetu zitakuwa zinalenga masafa mafupi pekee.
Kwa sababu hazijibu na wala kujiuliza kuwa haya madai ya tume huru ni ya nani? Ni kwa faida gani? Ni nani anayenufaka? Lakini nini kitatokea baada ya tume huru na kufanya uchaguzi?
Tunazo sera zitakazobadilisha maisha ya watu? Hsitoria yetu inatuambia nini juu ya hali zetu za maisha? Maswali haya ni ya kufikirisha na vyama havina budi kufikiria haya. Wakati wanadai tume huru, lazima wajadiliane na kuijua historia yetu, wapi tumetoka, kwa nini tuko maskini? Muktadha wa demokrasia yetu uweje?
Rai yangu
Madai haya kwangu ni ya msingi kabisa ya kudai tume huru kwamba si ya muhimu, la hasha!
Ni muhimu. Lakini hatuna budi kuweka nguvu zetu na maarifa yetu kumaliza mifumo ya uchumi inayowaumiza wengi, hasa walalahoi, mifumo inayofanya afya iuzwe, elimu iuzwe, maji yauzwe, umeme na mahitaji mengine muhimu ya binadamu yauzwe.
Sisikii wanasiasa wakiyanadi haya, nasikia tume huru tu lakini je, baada ya tume huru na uchaguzi, tutaendelea kuyaona haya, na kuendelea kukumbatia mifumo isiyowajali walalahoi?
Au kwetu ni masuala ya kawaida na hayana umuhimu huo kuliko tume huru? Maswali haya bado yanafikirisha na lazima tuyatafakari haya. Kwa hiyo tukiweza kujua haya, basi tutakuwa tunaelekea katika siasa za masafa marefu zinazolenga zaidi kuleta ukombozi kwa wananchi na kushirikiana nao kuleta huo ukombozi juu ya maisha ya wananchi kwa ujumla wake.
Wakati fulani tujaribu siasa za ukombozi kama ilivyokuwa wakati wa Mwalimu Julius Nyerere lakini katikati tulipoteza siasa hizo, sasa tunasema tume huru, uchaguzi, lakini hatuangalii mbele kipi kinatukabili katika maisha yetu ya kila siku.
Mwandishi wa makala hii ni Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU).
0683 961891/0659 639808 [email protected]