Nchini Senegal, kuelekea uchaguzi wa wabunge siku ya Jumapili, muungano wa mashirika 46 ya kiraia unaonya kuwepo kwa ongezeko la machafuko ya kisiasa katika kipindi hiki cha kampeni..
Mashirika ya kiraia yanayofuatilia mwenendo wa kampeni hizo katika maeneo mbalimbali ya nchi, yanasema kuna matumizi makubwa ya rasilimali za umma kama maafisa wa usalama, kuwahangaisha wanasiasa wa upinzani wanapoendelea kuomba kura.
Aidha, Mashirika hayo yametoa mfano wa Waziri wa afya aliyeamua kupelekea vifaa vya kutoa tiba katika eneo la Podor Kaskazini mwa nchi hiyo, kuwashawishi wapiga kura kumuunga mkono, kitendo ambacho kimetajwa ni matumizi mabaya ya rasilimali za umma kufanya kampeni.
Asilimia 26 ya vitendo hivi vilishuhudiwa ndani ya siku 10 ya kampeni, huku asilimia 20 ya vitendo vya rushwa vikiripotiwa kwa waangalizi hao.
Ofisi za vyama vya upinzani, zimeteketezwa moto jijini Dakar huku vipeperushi na mabango ya wagombea hao yakiharibiwa.
Licha ya changamoto hizi, waangalizi wa uchaguzi huo kutoka mashirika ya kiraia wanasema wameridhika namna Tume ya uchaguzi ilivyojiandaa kusimamia uchaguzi huo.