Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE) kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia wa Sekta za Umma na Binafsi (PPP) wanatatarajia kujenga mabweni ya wanafunzi kwa ubia utakaogharimu Sh bilioni 20.7.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa chuo hicho, Proesa Edda Lwoga, wakati akizungumza na waandishi wa habari chuoni hapo jijini Dar es Salaam.
Alisema mabweni hayo yatakayojengwa kwenye kampasi kuu ya Dar es Salaam yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,728 hivyo kupunguza pengo kubwa la malazi kwa wanafunzi.
Alisema kwa sasa kampasi ya CBE Dar es Salaam ina jumla ya wanafunzi 12,000, ambapo kwa upande wa malazi kampasi ina majengo mawili tu ya bweni yenye uwezo wa kuchukua vitanda 160 pekee vya malazi kwa wanafunzi wa kike na kiume hivyo vinakidhi uhitaji wa malazi kwa asilimia 1.3 tu.
“Mradi huo utafanywa kwa Ubia kati ya CBE na mwekezaji lakini pia naomba nitumie nafasi hii kuwafahamisha wadau, wawekezaji wa ndani na nje kuhusu fursa hii muhimu ya uwekezaji ili waweze kushiriki kwenye mkutano maalumu utakaokutanisha wadau mbalimbali katika kuupeleka mradi huu sokoni na kupeana uwelewa zaidi na mkutano huo utafanyika tarehe 20 siku ya Ijumaa,” alisema
Mkuu wa chuo alisema mradi huo utakapokamilika unatarajiwa kupunguza changamoto ya malazi kutoka asilimia 1.34 iliyopo mpaka asilimia 30 ya mahitaji ya wanafunzi kwa bweni.
“Hali iyopo imesababisha uhitaji mkubwa wa malazi ya wanafunzi kwa asilimia 98.6 hivyo wengi wanalazimika kutafuta malazi nje ya chuo kwa gharama kubwa, jambo linalosababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kumudu gharama hizo,” alisema.
Aidha, alisema chuo kimejitathmini na kuona njia ya ubia yaani PPP inatoa suluhisho la pengo hilo la miundombinu hivyo kwa kushirikiana na wawekezaji binafsi, CBE inaweza kutumia mitaji ya nje kujenga hosteli zinazohitajika bila kuathiri sana rasilimali zake za kifedha.
Kuhusu faida za mradi huo, Profesa alisema CBE imechagua njia hii ya PPP baada kujiridhisha na faida kadhaa zikiwemo, ujenzi unakamilika kwa wakati, washirika binafsi watachangia sio tu mitaji bali pia utaalamu katika ujenzi, usimamizi, na uendeshaji, hivyo kuhakikisha malazi ya ubora wa juu kwa wanafunzi.
Vilevile alisema kupitia mfumo wa (Design-Build-Finance-Operate-Maintain-Transfer), (DBFOMT) wawekezaji binafsi watasimamia mabweni hayo kwa muda maalum kama mkataba utakavyaongoza na baada ya muda huo, umiliki utarudishwa kwa CBE.
Aidha, alisema mabweni hayo yatahakikisha upatikanaji wa kutosha wa wanafunzi jambo ambalo alisema litaimarisha ufanisi wa kifedha wa mradi kwa wawekezaji.
Alisema ujenzi kwa njia ya ubia utahakikisha kuwa gharama za malazi zitakuwa nafuu ikilinganishwa na watoa huduma binafsi wa malazi nje ya kampasi.
“Kwa upande mwingine mradi huu unalenga rasmi kutekeleza malengo ya kitaifa, ikiwemo mipango ya serikali ya Kupanua Sekta ya Elimu, Sera ya uendelezaji wa biashara wa mwaka 2023 inayotoa kipaumbele kwa kuboresha ustawi wa wanafunzi na upatikanaji wa elimu ya juu,” alisema.
Alisema mradi huo unaendana na malengo ya uchumi ya kuongeza ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, kama ilivyoainishwa katika sera za ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi za Tanzania.
“Njia ya PPP ni bora na ya haraka kufanikisha mradi huu, ambayo itawanufaisha Wanafunzi na Taasisi. CBE imejikita katika kutoa mazingira bora ya kujifunzia na uboreshaji malazi ya wanafunzi ni kipaumbele muhimu kwetu nawashukuru washirika wa sekta binafsi, serikali, na wadau wote kwa mchango wao katika kufanikisha mradi huu muhimu,” alisema