Na Munir Shemweta
“Sekta ya ardhi ni nyeti kuliko sekta yoyote na iwapo itasimamiwa vizuri basi itaiingizia Serikali
mapato makubwa kuliko sekta nyingine’’. Hiyo ni kauli ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, wakati akikagua Mfumo wa Ukusanyaji Kodi ya Ardhi
kwa njia ya kielektroniki (GEPG) katika mikoa ya Mara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.
Katika ziara hiyo iliyohusisha pia ukaguzi wa mpaka wa Tanzania na Kenya, Mabula alibaini
upungufu mkubwa katika ufuatiliaji na ukusanyaji mapato ya ardhi kwa halmashauri mbalimbali
nchini; jambo alilolieleza kuwa linaikosesha mapato makubwa Serikali.
Alishangazwa na halmashauri kupitia idara za ardhi kushindwa kufuatilia madeni kwa wadaiwa
kodi ya ardhi huku idara hiyo ikiwa imewaingiza katika mfumo wa malipo kwa njia ya
kielektroniki ambao unasomeka pia wizarani.
“Mnahangaika na fedha ndogondogo za kudai ushuru huku mnawaacha watu mnaowadai pesa
nyingi katika kodi ya ardhi, kitu kinachoikosesha Serikali mapato mengi,” amesema Mabula.
Halmashauri zote za wilaya na miji alizotembelea Mabula zimekuwa na shida ya kufuatilia
madeni ya wadaiwa kodi ya ardhi huku baadhi wakiwa hawajalipa kodi ya ardhi kwa miaka kumi
bila kuchukuliwa hatua.
Halmashauri alizotembelea Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni Bunda,
Musoma, Butiama na Tarime mkoani Mara; Monduli, Longido, Arumeru na Arusha mkoani
Arusha; Rombo, Hai, Mwanga na Moshi mkoani Kilimanjaro; na Lushoto, Korogwe, Muheza,
Mkinga na Tanga mjini mkoani Tanga.
Imebainika kuwa halmashauri hizo zimejiwekea malengo madogo ya ukusanyaji kodi ya ardhi,
ikilinganishwa na kiasi halisi cha madeni inayodai kwa wamiliki wa ardhi huku zikijinasibu kuwa
zimevuka lengo wakati kuna madeni makubwa.
Kwa mfano Halmashauri ya Wilaya ya Monduli katika kipindi cha mwaka 2016/2017
imekusanya milioni 35 huku ikidai bilioni 2.475; Bunda ilikusanya Sh milioni 328 wakati ikidai Sh
bilioni 1.2.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ameagiza wadaiwa sugu wa kodi ya
ardhi kupelekewa hati ya mwito ya madai ya miezi mitatu na iwapo watashindwa kulipa madeni,
wapelekwe katika Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya ambako huko ni kulipa au kunyang’anywa
ardhi.
Ameahidi kutoa msaada wa wanasheria kwa halmashauri zitakazohitaji kusaidiwa.
Anasema Serikali imekuwa ikipigia kelele ukusanyaji maduhuli ya kodi ya ardhi, lakini suala hilo
halifanyiwi kazi ipasavyo hivyo amezitaka halmashauri kila robo mwaka katika vikao vyao
kuhakikisha zinabaini wadaiwa sugu wote na kuwapa hati za madai kwa lengo la kuisaidia
Serikali kukusanya maduhuli ya kodi ya ardhi.
“Mnachotakiwa sasa kufanya kwa yule mdaiwa sugu asiyeonekana ni kwenda katika eneo lake
na kuweka bango linaloonesha kuwa eneo hilo linauzwa na halmashauri na nina imani mhusika
atakapoona hivyo lazima atajitokeza na hapo ndipo mtaanza kushughulika naye,’’ amesema
Mabula.
Naibu Waziri ameshangazwa na sekta ya ardhi kutopewa kipaumbele na wakurugenzi wa
halmashauri kwenye bajeti ya kuendeshea ofisi kiasi cha kuwalazimu maafisa katika sekta hiyo
wakati mwingine kutumia fedha zao.
Baadhi ya Watumishi katika sekta ya ardhi kwenye halmashauri alizozuru Mabula
wamemweleza kuwa wanakabiliwa na upungufu wa vitendea kazi vya intaneti, karatasi, wino na
usafiri.
“Tumewawekea mfumo kuwarahisishia kazi na kuwapa mafunzo namna ya kutumia mfumo,
sasa mnataka hata vifurushi vya intaneti navyo tuwanunulie?’’ Amehoji Mabula.
Amewataka wakurugenzi wa halmshauri kuzingatia maelekezo ya fedha zinazotumwa katika
halmashauri zao kwa kuzitumia kwa masuala ya ardhi kwani baadhi yao wamekuwa

wakizitenga idara na fedha kuingizwa kwenye kapu la mkurugenzi.
Amesema Serikali imebadilisha utaratibu wa kurejesha fedha zinazopatikana kutokana na
makusanyo ya kodi ya ardhi ambako badala ya kutumia ule utaratibu wa asilimia 30, sasa
halmashauri zinapatiwa fedha kulingana na kiasi inachokusanya. Wizara imetengewa na
Serikali Sh bilioni 10 kwa halmashauri zote.
Pamoja na changamoto hizo, Mabula amebaini sekta ya ardhi katika halmashauri kutopewa
umuhimu kiasi cha baadhi yake kuongozwa na watu wasiokuwa na taaluma inayoendana na
masuala ya ardhi.
Imebainika kuwa baadhi huongozwa na maofisa misitu au maafisa nyuki; jambo ambalo
amesema limemshitua.
“Hii sekta inaonekana inadharaulika sana, yaani anayeongoza ni afisa misitu mbona idara
nyingine haziongozwi na watu wasiokuwa katika sekta husika? Ndiyo maana wakati mwingine
hamna uchungu na sekta hii,” amesema.
Mabula amebaini upungufu mkubwa katika utunzaji majalada ya ardhi usivyozingatia taratibu na
hivyo kutoa mwanya wa ‘kuchezewa’ majalada hayo na kuleta mkanganyiko.
Majalada mengi ya ardhi katika halmashauri yamebainika kutozingatia taratibu – mengi yakiwa
hayana maelekezo kutoka kwa afisa mmoja kwenda kwa mwingine na wakati mwingine
yanakuwa na risiti za malipo wakati risiti zilitakiwa ziwe kwa mtu aliyelipia.
Kuna baadhi ya majalada hata wamiliki halali hawafahamiki. Ameikuta hali hiyo katika
Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) kushughulikia suala hilo.
Katika ziara yake amewaambia watendaji kuwa Serikali imeamua kushughulikia kero za
wananchi katika sekta ya ardhi ikiwa ni pamoja na kurasimisha maeneo yaliyojengwa holela na
kuwapatia hati wamiliki wake, kupima maeneo mbalimbali na kutwaa maeneo kwa ajili ya
mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Amepiga marufuku kuchukua maeneo ya wananchi bila ya kuwalipa fidia na kama halmashauri
haina fedha, amesema inachotakiwa ni kuzungumza na mhusika au wahusika kwa lengo la
kukubaliana katika mfumo wa ‘barter trade’.
Katika kile kinachoonekana Mabula amepania kuhakikisha Serikali inapata mapato kupitia kodi
ya ardhi na wananchi kupata hati bila ya usumbufu, ameagiza Makamishna wa Kanda wa Ardhi
kuwapelekea hati wananchi katika halmashauri walizopo badala ya wananchi kuzifuata katika
kanda.
“Wakurugenzi muwasiliane na Makamishna wa Kanda ni siku gani aje katika eneo lako na
atakaa kwa siku ngapi kwa ajili ya kuwapatia hati wananchi na hati hiyo hakuna kutuma mtu
kumchukulia, anatakiwa aje mwenyewe,’’ ameagiza Mabula.
Anasema hati hiyo siyo tu itakuwa imepunguza kero kwa wananchi, bali itairahisishia Serikali
kutambua wananchi wenye hati na hivyo kuwa rahisi kupata mapato kupitia kodi ya ardhi.
Ameeleza faida kadhaa za wananchi kuwa na hati za ardhi kuwa ni kukopa kwenye taasisi za
fedha na hata kuweka dhamana pale inapohitajika kufanya hivyo kwenye mashauri mbalimbali
kwenye vyombo vya sheria.
Ziara hiyo imemsaidia Mabula kuona picha halisi ya baadhi ya watendaji wa Serikali katika
halmashauri nchini, kwani pamoja na kurejea katika maeneo aliyozuru awali na kutoa maagizo,
utekelezaji umekuwa hafifu na hivyo kuhitaji msaada wa wakuu wa wilaya na wakurugenzi.