Waathirika 2,575
Baada ya malalamiko haya kufanyiwa kazi kwa kina na kufanya tathmini mara tatu, bado kama inavyoelezwa, kuna watu 2,575 waliojitokeza kudai fidia ama kwa kupunjwa au kwa maelezo kuwa awamu zote tatu walirukwa katika uthamini.
Kati ya hao 1,900 wanasema walipunjwa fidia, 596 wanadai walirukwa katika tathmini, 25 wanalalamika kusababishiwa maumivu mbalimbali kutokana na milipuko, na 54 wanadai kuharibikiwa na samani zao.
Ingawa Serikali inasema ilikwishafunga malipo kwa mabomu ya Mbagala, wale waliolalamika wana kila sababu ya kuwa na matumaini baada ya Serikali kutoa taarifa rasmi Mei 22, 2012 kwa wabunge kuwa inatafuta fedha za kuwalipa.
“Ofisi ya Waziri Mkuu ikishirikiana na Hazina inaendelea na juhudi za kupata fedha ya malipo haya,” inasema taarifa hiyo bila kutaja malipo hayo ni kiasi gani, ila kwa idadi hiyo na mtiririko wa malipo lazima itakuwa sh bilioni moja kwenda juu.
Hitimisho
Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI baada ya kusoma nyaraka mbalimbali, umebaini kuwa watu walio wengi walipunjwa stahiki zao katika fidia; baadhi ya maofisa wa Serikali walitumia fursa hiyo kujitajirisha na kibaya zaidi kwa sasa hakuna msukumo wa kutafuta fedha hizo za nyongeza kwa hawa waathirika 2,575, kutokana na udhibiti mkali unaowafanya maofisa wa Serikali kuona haina tija kufuatilia malipo haya.
Hadi sasa Serikali imeshatoa Sh 10,908,802,310 kwa ajili ya fidia hizo, na Sh 10,528,640,792 zimetumika kulipa fidia au kutoa huduma isipokuwa kiasi cha Sh 259,697,003 ambacho kipo Hazina hadi leo wenyewe hawajitokezi kuzichukua.