Kilichotokea kwa fedha hizo
Hadi jana wakati tunakwenda mitamboni, kuna hundi zenye thamani ya Sh 259,697,003 bado ziko Hazina ambazo wahusika hawakujitokeza kuzichukua. Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa hundi hizo zimedoda kwa sababu moja ya msingi.

Wakubwa walikuwa wamechomeka majina hewa, na baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (wakati huo) Lukuvi kuanzisha utaratibu wa mtu anayechukua malipo kupigwa picha na kuchukuliwa alama za vidole, maofisa wa Serikali wameziona fedha hizo ni za moto hivyo kuzisusa.

Kinachoivunja kichwa Serikali ni fedha hizo sasa itazifanyia nini. “Hatujui kama zibadilishwe matumizi na kuingizwa kwenye shughuli nyingine za Serikali au tuzifanyeje, maana tangu 2009 hadi leo mtu hajajitokeza kudai unadhani huyu yupo kweli? Tulichobaini ni kuwa watumishi wasio waaminifu walichomeka majina hewa, lakini baada ya kubaini utaratibu unalazimisha mtu afahamike kwa kupigwa picha, wameamua kutojitokeza,” kilisema chanzo chetu.

Nyaraka mbalimbali za Serikali zinakiri kuwa wananchi wa Mbagala waliolipukiwa na mabomu walipunjwa fidia. “Waathirika 111 walipunjwa malipo ya fidia kwa Sh 1,050,862,900,” inasema sehemu ya waraka mzito wa Serikali kwa wabunge.

Taarifa ya Serikali inakiri kuwa wapo waathirika 41 waliolipwa zaidi kwa Sh 183,883,000. Hili lilifanyika kwa wengine kupokea malipo mara mbili hadi tatu na wengine kupewa thamani kubwa kuliko uhalisia wa mali iliyoharibika.

Pia hadi sasa kiasi cha Sh 48,780,000 kimelipwa lakini haijulikani nani alilipwa fedha hizo ingawa hazikuwa kwenye orodha ya watu wa kufidiwa. “Huu ndiyo wizi wenyewe,” chanzo chetu kiliongeza.