Uthamini wa kwanza
Baada ya mabomu kuwa kulipuka huko Mbagala Aprili 29, 2009, uthamini wa kwanza ulifanyika kati ya Aprili 30 na Juni 4, 2009. Wathamini walikuwa na vigezo lakini kwa bahati mbaya vigezo havikufuatwa kwa sababu ya urafiki na ulafi wa kutaka kupata fedha za dezo.

Walikamilisha ripoti iliyoonekana wazi ni ya hovyo, ambayo haikuonyesha idadi sahihi ya waathirika walioharibiwa vyombo (samani) vyao ikilinganishwa na uharibifu uliotokea. Takwimu zilikuwa hazijaainisha idadi ya nyumba zilizoharibika kabisa, nyumba ambazo hazifai kuishi na nyumba zilizohitaji kufanyiwa ukarabati.

Ukiacha upungufu huo, malalamiko ya wananchi yalikuwa mengi kupita kiasi, ambapo baadhi ya maofisa wa Serikali walikuwa wameamua kufanya ubabe na kuwaruka baadhi ya watu walioathirika huku zikivuma taarifa kuwa vitendo vya rushwa vilijipenyeza miongoni mwa wathamini.