*Wakubwa walitumia (msiba huo) kutengeneza utajiri binafsi
*Ofisi ya Pinda yahaha kutafuta zaidi ya bilioni fidia mpya
*Waliopunjwa kucheka, hundi hewa milioni 260 zadoda

Miaka mitatu baada ya mabomu kulipuka katika Kambi ya Jeshi Mbagala nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, siri nzito zimeanza kuvuja jinsi wakubwa walivyotumia msiba huo kujitengenezea utajiri binafsi.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na ofisi mbalimbali za Serikali ikiwamo Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke umebaini kuwa viongozi walioshughulikia fidia walitumia mwanya huo kuzoa mabilioni.

Wakati baadhi ya waathirika wakipunjwa malipo yao, majina mengi hewa yalichomekwa kwa matumaini ya watu fulani kuvuta fedha hizo, lakini baada ya Serikali kushitukia dili hilo, maofisa waliohusika na suala hilo wakaona fedha hizo zitawatokea puani, wakazisusa.

Nyaraka mbalimbali kutoka serikalini zinaonyesha kuwa wananchi wengi wa Mbagala walioathirika walilipwa fidia ndogo ikilinganishwa na uhalisia wa mali zilizoharibika, hali iliyowalazimu kuibana Serikali na uthamini ukafanywa mara tatu.