Na Mwandishi Wetu
WACHEZAJI watatu bora wa mashindano ya gofu ya Lina PG Tour 2024 wapo katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) jijini Dubai kwa ajili ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya Clutch Tour Tier 1 yanayoanza kutimua vumbi kesho.
Mashindano hayo yataanza kesho Machi 18 hadi 20, 2025 yamewaleta pamoja wachezaji wa gofu waliobobea na mahiri kutoka kote ulimwenguni.
Tanzania itawakilishwa na wachezaji wawili wa kulipwa wa gofu ambao walichukua nafasi ya kwanza kwenye mashindano ya Lina PG Tour 2024 ambao ni Nuru Mollel na Fadhil Nkya pamoja na bingwa kwa upande wa wachezaji wa ridhaa Isiaka Dunia.

Safari ya wachezaji hao kwenda katika mshindano hayo imeandaliwa chini ya Lina PG Tour kama sehemu ya mfululizo wa Safari ya Dubai, ambayo inalenga kutoa jukwaa shindani kwa wachezaji wa mchezo wa gofu.
Mkurugenzi wa mashindano hayo ya Lina PG Tour, Yasmin Chali amesema wachezaji wote watatu wapo katika hali nzuri ya ushindani na wanajiamini hivyo anaimani kuwa watafanya vizuri katika mashindano hayo yanayoanza kesho.
Amesema wachezaji wa Tanzania wanajitahidi na tangu wamefika jijini Dubai wanafanya mazoezi ya kutosha na kwamba hali ya kujiamini kwao imeongezeka, wanahamu na mashindano hayo.
“Maandalizi yapo vizuri kwa wachezaji wetu, huku kuna wachezaji wa gofu wa kulipwa zaidi ya 130 na baada ya siku mbili kutakuwa mchujo na watabaki 50 ambao ndio wataendelea na mashindano, tunaimani kubwa kuwa tutafanya vizuri na kusonga mbele hatimaye kuleta taji nyumbani,” amesema Chali
Mchezaji Nkya ndio nahodha wa timu ya Tanzania, akiwaongoza wenzake wawili katika michuano hiyo ambao waliibuka washindi katika mashindano ya Lina PG Tour msimu wa kwanza uliofanyika mwaka jana.

Nkya anatoka katika klabu ya Gymkhana ya Dar es Salaam, Nuru Mollel klabu ya Gymkhana ya Arusha na Isiaka Dunia klabu ya Gofu ya TPDF Lugalo ambapo kwa pamoja wamesema wako tayari kuonyesha vipaji vyao kwenye mashindani hayo ya kimataifa.
Itakumbukwa kuwa mashindano ya Lina PG Tour ndio yaliyowawezesha wachezaji hao kwenda jijini Dubai yanafanyika kila mwaka hapa nchini kwa lengo la kumuenzi mchezaji gofu wa zamani wa timu ya wanawake marehemu Lina Nkya.