Mabilionea wakubwa kumi nchini Marekani wana utajiri wa pamoja unaofikia dola nusu trilioni na athari za utajiri huo tayari zimekwisha kuanza kuonekana katika uchaguzi wa nchi hiyo.
Matajiri hao wamejihusisha kwa namna moja au nyingine na uchaguzi huo, huku mmoja wao, Michael Bloomberg, ambaye anashika nafasi ya sita katika orodha ya matajiri wakubwa Marekani akiomba kuteuliwa na Chama cha Democrat kuwa mgombea urais.
Wakati Bloomberg akiomba nafasi hiyo, mabilionea wengine wamekuwa muhimu kupitia michango yao ya fedha kwa vyama vya siasa nchini humo.
Bloomberg tayari amekwisha kutumia mamilioni ya dola katika kampeni zake kiasi cha kuanza kushambuliwa na wagombea wenzake kuwa anatumia utajiri wake kununua urais.
Mwanzilishi mwenza wa Kampuni ya Oracle (ORCL), Larry Ellison, ambaye anatajwa kuwa tajiri namba nne akiwa na utajiri unaofikia dola za Marekani bilioni 62.5, aliandaa hafla ya uchangishaji fedha hivi karibuni, akimkaribisha pia Rais wa sasa wa nchi hiyo, Donald Trump, ambaye naye yumo kwenye orodha ya matajiri hao.
Kwa mujibu wa mialiko iliyokuwa imetolewa, watu waliohudhuria hafla hiyo walipaswa kuchanga kati ya dola 100,000 na 250,000 kwa ajili ya kumsaidia Trump katika kampeni zake za awali na kampeni za uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.
Fedha hizo pia zitatumiwa na Chama chake cha Republican katika kuendesha shughuli za uteuzi wa mgombea na baadaye kampeni za uchaguzi.
Ellison amejiunga na kambi ya Trump hivi karibuni. Katika uchaguzi wa mwaka 2016 alitoa mamilioni ya dola kwa Marco Rubio. Kwa miaka mingi, Ellison amekuwa na tabia ya kutoa fedha kwa vyama vyote lakini akikipendelea zaidi Republican.
Miaka ya nyuma amewahi kutoa fedha kwa wagombea wa Democrat kama vile Joseph Crowley, wakati akiwania nafasi ya Congress kupitia Jimbo la New York, ambaye hata hivyo aling’olewa mwaka 2018 na Alexandria Ocasio-Cortez. Ellison pia amewahi kutoa fedha kwa Seneta Harry Reid wa Nevada na Ron Wyden wa Oregon.
Rekodi zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, Ellison alikuwa hajatoa mchango wowote wa kifedha kwa Trump.
Charles Koch, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Koch Industries, mwenye utajiri wa dola bilioni 50.5, ni bilionea mwingine ambaye pamoja na kaka yake David, wamekwisha kutoa michango mikubwa ya fedha kwa vyama vya Republican na Libertarian kwa miaka mingi.
Hata hivyo, wanafamilia hao mara kwa mara wamekuwa wakikosana na Trump, wakimkosoa kwa masuala mengi, hasa masuala ya biashara.
Kwa upande wake, Trump, akiandika kupitia twitter, amekwishawahi kueleza kuwa hana haja na fedha za wanandugu hao matajiri.
“Sikuwahi kuwaomba waniunge mkono kwa sababu sizihitaji fedha zao au mawazo yao (kwenye biashara),” anaandika Trump.
Hadi hivi sasa Charles Koch hajaonyesha iwapo atamuunga mkono Trump, na iwapo atafanya hivyo atachangia kiasi gani cha fedha. Hadi hivi sasa wanandugu hao wameshatoa fedha kwa ajili ya wagombea wa viti vya seneti.
Tajiri mwingine ni Jim Walton, mmoja wa wamiliki wa Walmart. Yeye anatajwa kuwa na utajiri unaofikia dola bilioni 44.6 na yuko namba 10 katika orodha ya matajiri wakubwa Marekani.
Si mtu anayependa kujionyesha sana katika masuala ya kisiasa, lakini anaonekana kuwa ameshatoa fedha kwa makundi kadhaa ya Republican, akiwamo Trump.
Wapo matajiri wawili ambao wanahusishwa na Chama cha Democrat.
Mark Zuckerberg (tajiri namba 5 akiwa na utajiri wa dola bilioni 62.3) amekwisha kuonyesha dhamira ya kuchangia kampeni za Meya Pete Buttigieg. Zuckerberg alitembelea eneo la meya huyo, South Bend, mwaka 2017 na akafanya mkutano uliorushwa moja kwa moja kupitia facebook akiwa na meya huyo wa zamani.
Zuckerberg pia amekwisha kuwachangia wagombea wengine wa Democrat.
Taarifa zilizovuja zilimnukuu akisema kuwa Elizabeth Warren, ambaye hivi sasa anachuana na wengine kuwania kuteuliwa kuwa mgombea urais, atakuwa hatari kwa facebook iwapo atateuliwa.
Zuckberg pia amewahi kukutana na Trump mwaka jana.