Mkutano wa matajiri wakubwa duniani ulifanyika mjini Davos katika milima ya Uswisi tarehe 20 hadi 23 Januari mwaka huu. Takriban matajiri 2,500 walishiriki, pamoja na wakuu wa kampuni za kimataifa, wakuu wa serikali na watu mashuhuri. Huu ni mkutano wa 45 ambao unafanyika kila mwaka. Wenyewe wanauita ‘ulingo wa uchumi duniani’ (World Economic Forum – WEF).
Mabepari hawa na wakuu wa kampuni zao waliwasili katika ndege zao za kifahari, na kufikia katika hoteli za anasa ambako sahani moja ya mlo ni dola 1,000 za Marekani. Lengo lao wanadai ni kuzungumzia maendeleo na hali ya uchumi duniani. Pia walikuwapo waandishi 500 wa habari pamoja na waajiriwa 600 wa WEF.
Miongoni mwa ajenda zao ni uchafuzi wa hali ya hewa duniani, bila ya kujali kuwa wachafuzi wakubwa ni hao hao waliowasili Davos kwa mamia ya ndege binafsi zilizokuwa zikimimina hewa ya kaboni angani. Hawakutaka kusafiri kwa ndege za kawaida. Matokeo yake viwanja vya ndege vya Uswisi vilifurika.
Miongoni mwa walioshiriki ni wamiliki na wakuu wa kampuni kama Goldman Sachs, JPMorgan Chase, GM, Google, Alibaba, Microsoft na Facebook. Pia walikuwapo wakuu wa serikali kutoka Marekani na Ulaya.
Mkutano wa Davos ulihudhuriwa pia na asasi za kiraia ambazo ziliamua kutoa mawazo mbadala. Mojawapo ni Oxfam, asasi ya kimataifa kutoka Uingereza. Wao kama ilivyo kawaida yao, walifanya utafiti wa kina na wakatayarisha ripoti inayoonyesha jinsi tofauti kati ya matajiri na masikini inavyoongezeka ulimwenguni – yaani matajiri kuzidi kutajirika na masikini kuzidi kudidimia.
Mwaka 2010, kwa mfano, mabilioea 388 walioongoza duniani walimiliki zaidi ya nusu ya mali zote duniani. Mwaka huu ni matajiri 62 wanamiliki nusu ya mali zote. Yaani hawa matajiri 62 tu mali wanazomiliki zimeongezeka kwa asilimia 44 katika muda wa miaka sita. Sasa wanamiliki jumla ya dola trilioni 7.6. Hii inaonesha jinsi mali inavyozidi kushikwa na matajiri wachache.
Maana yake utajiri wote duniani unahodhiwa na asilimia moja ya watu wa duniani. Hawa wanatumia nguvu zao za kiuchumi kujilimbikizia siyo tu mali, bali pia uwezo wa kuamua jinsi uchumi wa kimataifa utakavyoendeshwa kwa faida yao. Mbinu moja wanayotumia ili kuzidi kujitajirisha ni kukwepa kulipa kodi. Wanafanya hivyo kwa kuficha mali zao katika benki za siri (off-shore) ambako wanaweka hizo trilioni 7.6.
Mkuu wa Oxfam, Mark Goldring amesema ulimwengu hautakubali kuona sehemu kubwa ya utajiri wa dunia umo mikononi mwa matajiri wachache ambao hawawezi hata kujaza basi.
Akaongeza kuwa hii ni hali isiyokubalika, mamilioni ya watu kukosa mlo mmoja kwa siku wakati matajiri wachache wanazidi kujitajirisha.
“Ni lazima tuhakikishe kuwa tunateketeza mfumo huu wa mabenki ya siri ambako kampuni za kimataifa na matajiri wanaficha fedha zao wasizozilipia kodi. Kwa njia hii wanakwepa wajibu wao kwa jamii,” anasema Goldring, akiongeza kuwa njia moja ya kupunguza umasikini ni kuondokana na huu msururu wa benki za siri (off shore).
Kuhusu hizi benki za siri, asilimia 90 ya matajiri na kampuni zao ziliyohudhuria mkutano wa Davos wameficha fedha huko. Na kima hiki kinaongezeka. Kuanzia 2000 hadi 2014 idadi ya fedha walizoficha ziliongezeka mara nne. Matokeo yake nchi masikini zinapoteza takriban dola bilioni 100 za Marekani kila mwaka.
Inakisiwa kuwa matajiri wa ulimwengu wameweka katika benki hizi takriban dola trilioni 7.6. Kama fedha hizi zingelipiwa kodi, basi serikali zetu zingeingiza mapato ya dola bilioni 190 za Marekani ambazo zingesaidia katika utoaji huduma za kijamii.
Benki nyingi ziko katika maeneo ya Carribean. Mfano mmoja ni visiwa vya British Virgin Islands ambavyo vinatawaliwa na Uingereza. Wakazi wake ni 24,000 tu, lakini kuna kampuni bandia 800,000 zilizoandikishwa huko (shell companies). Hizo zinatumiwa na mabepari katika kuficha mabilioni ya fedha zisizolipiwa kodi au zilizopatikana kwa njia haramu. Wanatumia kampuni bandia zenye majina bandia ili kuepuka kutambulika.
Mfano mmoja ni benki ya Barclays ya Uingereza. Mnamo mwaka 2012 mkuu wake alihojiwa na wabunge wa nchi hiyo. Katika mahojiano hayo ilijitokeza kuwa benki hiyo ina kampuni tanzu 30 katika kisiwa cha Isle of Man, 38 katika kisiwa cha Jersey na 181 katika Cayman Islands. Kwa ujumla benki hiyo ina kampuni tanzu 300 katika visiwa vya off-shore duniani kote.
Miaka mitatu iliyopita Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, aliahidi kuwa atachukua hatua thabiti dhidi ya wanaoficha fedha huko bila ya kulipa kodi. Hadi leo hakuna hatua alizochukua.
Mabepari wa kimataifa waliokutana Davos wanadai wanazungumzia maendeleo ya kimataifa, na ndio maana huwaalika marais kutoka nchi za Afrika. Na marais wetu huwa wanachangamkia sana mialiko ya kwenda kupeana mikono na mabepari na kuwaalika kuja kuwekeza hapa kwetu!
Kisichozungumzwa ni kuwa lengo halisi la mkutano huu ni kufinyanga na kubuni mfumo wa utawala ili badala ya uamuzi kuchukuliwa na serikali zetu, uwezo huo uwe mikononi mwa wale wanaojiita wadau.
Kwa maneno mengine, sisi raia tunazichagua serikali za “kidemokrasia” ambazo zitakuwa zinaingia mikataba na wawekezaji na wafadhili wa kimataifa ambao ndio watakaotuamulia sera!
Huko ndiko nchi zetu zinakoelekea au tunakoburuzwa. Mashirika ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa (UN) yatakuwa na kazi ya kuidhinisha tu uamuzi utakaochukuliwa na “wadau”. Uhuru wa kujiamulia mustakabali wetu utapotea.
Haya yamesemwa hata na mwanzilishi na mkuu wa WEF, Klaus Schwab. Ndio maana WEF imeunda mabaraza 40 yatakayojadili ajenda za kimataifa (Global Agenda Councils). Ni mabaraza haya ndio yatakayotoa mipango ya “maendeleo” yetu ambayo yatakuwa mikononi mwa kampuni za kimataifa.
Chini ya mfumo huu, serikali zetu zitatakiwa zishirikiane na sekta binafsi kwenye utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa na mabaraza. Tayari wameunda mabaraza yanayoshughulikia masuala ya maji, usafiri wa majini, mtandao wa intaneti na kilimo.
Hii inadhihirisha kuwa mabepari wa kimataifa wanapokutana huko Davos nia yao ni kuunda mfumo mpya wa utandawazi utakaodhibiti uchumi na uzalishaji wa ulimwengu.
Ndio maana Oxfam ilishauri mbinu za kujikwamua kutoka umasikini duniani. Njia ya kwanza ni kuwachukulia hatua za kisheria na kiutawala mabepari wanaokwepa kulipa kodi. Njia ya pili ni kuwekeza mitaji yetu zaidi katika huduma za kijamii kama elimu, matibabu na maji. Njia ya tatu ni kuongeza mishahara ya wafanyakazi na mapato ya wakulima.
Kuhusu kuwabana wakwepaji kodi, Oxfam inasema ni pamoja na kuwafungia mabenki ya siri ili kuziba mianya ya utoroshaji wa fedha chafu.
Tumeona jinsi miaka mitatu iliyopita Waziri Mkuu wa Uingereza alivyoahidi kuchukua hatua dhidi ya benki za siri katika visiwa kama Cayman na Virgin vilivyo chini ya himaya ya Uingereza. Alisema kuwa atalazimisha akaunti hizo za siri zifichuliwe ili kubaini uvunjifu wa sheria. Hiyo ilikuwa ahadi hewa, kwa hivyo nchi zetu zinaendelea kuporwa.
Kwani kwa mujibu wa ripoti ya Oxfam, asilimia 30 ya fedha za Afrika zinakisiwa kufichwa katika benki za off-shore. Kama fedha hizi zingelipiwa kodi, basi nchi zetu zingepata dola bilioni 14 za Marekani. Hii ndio kodi inayoporwa na matajiri kutoka bara hili. Fedha hizi zingetosha kuwapatia kina mama na watoto wao matibabu. Zingetosha kuokoa maisha ya watoto milioni nne wanaokufa kila mwaka. Zingetosha kulipa mishahara ya walimu wote ili kumpatia kila mtoto elimu bila malipo.
Katika mkutano wa Davos, asasi ya Oxfam ilishirikiana na asazi zingine za kimataifa kama vile ActionAid, Christian Aid, Amnesty International, Greenpeace na ushirika wa vyama vya wafanyakazi duniani (International Trade Union Confederation). Wengine ni umoja wa haki za wanawake katika maendeleo (Association for Women’s Rights in Development), mshikamano wa asasi za kiraia duniani (CIVICUS) na mtandao wa asasi za kidini kama ACT na CIDSE.
Katika risala yao ya pamoja walionya kuwa kuongezeka kwa tofauti baina ya matajiri na masikini kunaathiri maendeleo ya kijamii, mazingira, haki za wanawake na haki za binadamu.
Risala ikaongeza: “Jitihada za kuboresha maisha zinashidikana kutokana na tofauti hii ya tajiri na masikini ambayo inaongezeka kila kukicha. Ulimwenguni kote tunaona hali hii ambayo haijawahi kuonekana katika karne nzima.”
Ili kupambana na hali hii asasi hizi zimeazimia kushirikiana siyo tu miongoni mwao tu, bali na asasi nyingine duniani zinazojitahidi kuboresha maisha ya mwananchi masikini. Lengo ni kuunda vuguvugu la kimataifa ili kupambana na mabepari wa kimataifa wanaotumia utajiri wao ili kuzuia maendeleo. Kisha risala ya pamoja ikasema:
“Tunataka tuwe na dunia iliyo bora kuliko ilivyo sasa, ambako haki za kila raia zinalindwa, kuheshimiwa na kutekelezwa. Tuna hakika kuwa binadamu ana uwezo na umahiri wa kuunda dunia bora ambako maslahi ya walio wengi inawekwa mbele. Na tunaamini kuwa wakati umefika sasa kuunganisha nguvu zetu na kupigania dunia hiyo”
Haya pia yalisemwa na kiongozi mashuhuri wa watu weusi nchini Marekani, marehemu Martin Luther King. Yeye aliwahi kusema kuwa misaada au sadaka si kitu kibaya, ila ni vizuri tukauliza ilikuwaje mpaka watu wakalazimika kuomba hiyo misaada. Tuulize vipi tunaweza kuepukana na mfumo unaosababisha masikini kuomba sadaka kutoka kwa tajiri. Hili ni suala la kubadili mfumo.
Huu ndio mkutano wa mabepari wakuu duniani uliofanyika Uswisi. Ilibidi serikali ya nchi hiyo itumie askari wake zaidi ya 5,000 ili kuwalinda waheshimiwa hawa “wasihujumiwe” na waandamanaji. Ndio maana eneo zima la mkutano lilizungushwa seng’enge.
Pia waliwekwa makomando juu ya kila jengo, wakiwa na silaha nzito. Hatuambiwi serikali ya Uswisi iligharimia kiasi gani mbwembwe zote hizo za mabepari. Lakini tunachojua ni kuwa nchi hiyo ndiyo inayoongoza kwa mabenki ya siri.