Kwa wiki nzima sasa nchi yetu imekumbwa na mgogoro mkubwa unaohusisha madaktari na serikali kwa upande mwingine.

Mgogoro huu umeingia doa zaidi baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk. Stephen Ulimboka, kutekwa na kupigwa na kuumizwa na watu ambao hadi sasa hawajafahamika. Hukumu inayotolewa na wengi hata kabla ya uchunguzi kukamilika ni kwamba suala hili limetendwa na vyombo vya dola.

Kwanza tunapenda kueleza masikitiko yetu juu ya tukio hili la kinyama bila kujali aliyelitenda ni serikali au la. Tunalaani vikali matendo ya aina hii kwa sababu mtu yeyote aliyetenda tukio hili amechukua mkondo usio sahihi. Katika dunia hii hakuna tofauti zisizomalizwa hata kama mmehitilafiana. Tunajua madaktari wameeleza kutokuwa na imani na Tume iliyoundwa na tunadhani nao wanaweza pia kuunda Tume mbadala wakaja na matokeo ya uchunguzi wao.

Pili tunapenda kuwasihi Watanzania kuheshimu utawala wa sheria. Kuchukua hatua ya kumpiga na kumuumiza Dk. Ulimboka kwa kiwango hicho ni unyama uliokithiri – usio na tofauti na uharamia.

Kwa upande mwingine, sisi tunadhani nchi yetu sasa ipime utamaduni mpya tuliouingia. Tukio hili baada ya kutokea tumepitisha hukumu moja kwa moja dhidi ya Serikali. Tunadhani tunapaswa kusubiri uchunguzi kisha tujue hasa nani aliyehusika. Kwa bahati inasemekana kuwa kuna baadhi ya hao waliofanya hivyo Dk. Ulimboka aliwatambua.

Baada ya kueleza masikitiko yetu, turejee katika hoja ya msingi inayodhaniwa kuzaa hata utekaji wa Dk. Ulimboka. Tunajua kuwa nchi hii inatafunwa. Wapo watu wanajenga maghorofa kila kukicha ilhali sisi tunashindwa kumalizia hata vibanda vya nyasi. Wanasiasa wamegeuka wala rushwa wakubwa hadi wengine wanatiwa mbaroni.

Wabunge ndiyo wamekuwa chimbuko la yote haya. Spika wa Bunge Anne Makinda alipolitangazia taifa kuwa maisha yamekuwa magumu hivyo kila mbunge anastahili kulipwa posho ya Sh 200,000 kwa siku, ndipo na madaktari walipoona kumbe nao wanastahili mishahara minono.

Maana ni ukweli ulio wazi kuwa wapo watu tumesoma nao walikuwa  wanapata maksi namba za viatu darasani leo ni wabunge, wanatembelea magari mazuri na wana uhakika wa maisha.

Tuliwahi kusema siku za nyuma kuwa kwa tofauti kubwa iliyopo ya pato inayozidi kuongezeka kati ya wabunge na kada nyingine za utumishi wa umma, ipo siku itazaa maafa kwa taifa hili. Mgomo wa madaktari ni matunda ya kutosikiliza ushauri wetu. Kama wabunge wangeendelea kulipwa fedha kidogo, hata wapigakura wasingeongeza kasi ya kuwaomba fedha.

Kwa vyovyote iwavyo, tunasema katika hili pamoja na kwamba kesi tayari iko mahakamani, kwa vitisho vya kuwafukuza madaktari pande husika zirejee kwenye mazungumzo na upatikane ufumbuzi wa kudumu. Mgomo huu ni hatari kwa ustawi wa jamii. Tusipoziba ufa, tutajenga ukuta.