Huu ni Mwaka Mpya. Nawatakia Watanzania wote heri ya Mwaka Mpya wa 2016. 

Kawaida Wahaya wana jadi ya kuupa jina kila mwaka unaokuja. Mwaka huu wameupa jina la ‘yangua’ lenye maana ya harakisha. Jina hilo limetungwa na Filbert Kakwezi, kijana ninayeweza kumuita mwandishi mkongwe  japo yeye hajawa mkongwe kiumri.

Ni imani yangu kuwa katika kutunga jina hilo, Kakwezi alilenga kuihimiza nchi yetu kufanya haraka katika kuirudisha hadhi yake ambayo kwa miongo kama miwili imeporomoka kwa kasi ya kutisha. Kwa maana hiyo jina hilo ni kama limeambatana na kauli ya Rais wa Awamu mpya ya Tano ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Joseph Magufuli, ya hapa kazi tu. Ni lazima Magufuli kalisema hilo kwa kusukumwa na aliloliona kuwa haliendi sawa.

Neno hapa kazi tu kwa namna moja au nyingine linaainisha au kuhimiza kufanya haraka. Sababu muda wote Watanzania wanafanya kazi tangu wajipatie uhuru wao. Kwa hiyo, kwa kuhimizwa kufanya kazi tu, hapa kazi tu, moja kwa moja ni kuhimizwa kufanya haraka, ‘yangua’. Inawezekana kazi ilikuwa ikifanyika lakini ikikosa uharaka unaotakiwa.

Bila shaka wito huo wa Rais unawahimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii na haraka ili kuirudishia nchi  hadhi yake ambayo ilikuwa imeanza kuyoyoma kwa kasi. Kama siyo hivyo sidhani kama Rais Magufuli angeona ulazima wa kuanzisha wito huo wa hapa kazi tu, au ‘yangua’.

Tujaribu kutafakari, Tanzania, nchi iliyokuwa kimbilio  la wanyonge waliokuwa wakiporwa haki zao duniani kote, nchi iliyogeuzwa mahali pa kujengea mikakati ya kurudisha haki na hadhi ya utu, mara hii inageuzwa nchi ya kutolea mifano ya dharau na kebehi ya ‘usiwe kama Tanzania’, kwa maana ya nchi isiyothamini utu na haki za binadamu kama ilivyowahi kuwa nchi ya Uganda wakati wa utawala wa Idi Amin Dada na mataifa mengine ya aina hiyo, hilo ni jambo la aibu sana ambalo hakuna aliyelitarajia.

 Fikiria mambo ambayo Tanzania ilikuwa mstari wa mbele katika kuyapiga vita, sasa yanaigeukia yenyewe na kuisakama kama luba afanyavyo anapojibana kwenye mwili wa binadamu!

Kwa mantiki hiyo, huu mwaka mpya wa ‘yangua’ au hapa kazi tu,  unatakiwa uyabadilishe hayo yote ili kuirudishia Tanzania hadhi yake iliyoporomoka kwa kasi ya kutisha. Inabidi kujiuliza hadhi hiyo ilitengenezwaje mpaka ikawapo, ilitengenezwa na viumbe wa aina gani? Hata kama siyo hawa waliopo ila ni binadamu kama hawa waliopo. Kwa hiyo inaweza kurudishwa, suala ni  hapa kazi tu au ‘yangua’.

 Uharaka na bidii ya kazi ndiyo dawa pekee ya kuutibu ugonjwa huu ulioipata nchi yetu. Kupona inawezekana iwapo kila mwananchi atatimiza wajibu wake kama alivyowahi kuhimiza Baba wa Taifa mwanzoni mwa miaka ya uhuru wetu.

Kinara wetu kwa wakati huu, Rais Magufuli, anatakiwa ahakikishe kasi aliyoanza nayo na kuwafanya Wahaya walikubali jina la mwaka la ‘yangua’, kwa maana ya fanya kasi, anaiendeleza kasi hiyo ili, pamoja na mambo mengine, aielekeze katika kuirudishia nchi yetu hadhi yake mbele ya macho ya jumuiya ya kimataifa. Tanzania irudi kuwa tishio la kutolea mfano kwa ubora wake, isiwe tena nchi ya kutolea mifano ya kebehi.

Inatakiwa Rais Magufuli atambue kwamba kubaki kwenye historia ya nchi, kwamba aliwahi kuwa Rais wa Tanzania ni jambo moja na kubaki katika historia ya marais bora, siyo kwa Tanzania peke yake bali hata duniani kote, ni jambo jingine. Na hilo ndilo jambo linalotafutwa na watu kote duniani.

Mfano wa karibu ni wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Mwalimu huyo hahesabiki tu kama aliyekuwa kiongozi wa Tanzania, bali dunia nzima inamuenzi kama aliyepata kuwa kiongozi mzuri  na jasiri. Hiyo ni heshima aliyojitafutia Nyerere bila kutumia uwezo mkubwa kiuchumi, bali akili na busara  tu.

Juhudi hizo binafsi za Mwalimu ndizo zilizomfanya akaenziwa duniani kote kiasi cha kuwafanya waumini wa Kikatoliki katika mataifa mbalimbali waanze kufanya mchakato wa kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili amfanye mtakatifu kupitia madhehebu hayo. Ikumbukwe kwamba Nyerere hakuwa kiongozi wa kidini bali wa kisiasa. Ila alichokifanya katika siasa ndicho kinachompa sifa zote hizo.

Mfano mwingine ni wa nchi ya Marekani. Nchi hiyo imeishakuwa na marais  44 mpaka sasa, lakini marais wanaokumbukwa na kuenziwa katika nchi hiyo  hawazidi watano. Wengine wanabaki tu kwenye historia ya nchi hiyo kwamba nao walikuwa marais lakini bila kuenziwa kwa namna yoyote ile kana kwamba hawajawahi kuwapo. Ni kwamba juhudi walizozifanya hao wanaokumbukwa ndizo zilizowafanya wawe hivyo.

Kwa hiyo, jambo ambalo Magufuli anaweza kulifanya ili si tu  abaki kwenye  historia ya Tanzania bali abaki akienziwa kama kiongozi mpendwa, ni kuhakikisha anairudishia nchi hii hadhi yake iliyopotea. Ahakikishe haki za wananchi zinawarudia, uamuzi wao unaheshimiwa,  kwa maana wao ndiyo wenye nchi na mambo kama hayo.

Tanzania ambayo muda wote huko nyuma ilipigana kufa na kupona kuhakikisha wazalendo wa Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia  wanapata haki zao za uraia  wakati nchi hizo tayari zilishajitangaza kama nchi huru, iwe ni Tanzania ileile linapokuja suala la Zanzibar. Haiwezekani kwamba Tanzania iliona hitilafu kwenye uongozi wa nchi hizo lakini ishindwe kuiona hitilafu hiyo katika uongozi wa Zanzibar,  ilhali yanayolalamikiwa na Wazanzibari yakiwa ni sawasawa na yaliyolalamikiwa na wazalendo  katika nchi hizo.

Tuelewe kwamba kebehi ninazozisema hapa zilizoligubika jina la Tanzania kwa kiasi kikubwa zinatokana na mgogoro wa Zanzibar. Inaeleweka kwamba Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kama ni hivyo kwa nini wao wanachagua rais wao wa Zanzibar  wakati Mkoa wa Kagera hawachagui rais wa Kagera wala mikoa mingine kufanya hivyo?

Kwa mantiki hiyo, inaonekana kwamba pale kuna hitilafu, na kama Tanzania iliiona hitilafu ya aina hiyo katika nchi nyingine na kuamua kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha hitilafu hizo zinamalizwa katika nchi hizo, basi inapaswa izione na hizi za Visiwani Zanzibar, vinginevyo kitabaki ni kitendawili kwa Tanzania kuirudisha hadhi yake iliyopotea.

Jambo jingine ni kuhusu Upinzani hapa nchini. Upinzani unatakiwa upewe heshima yake kama ilivyo katika nchi zote zinazoheshimu kitu hicho. Lakini Upinzani ukiendelea kuwa kama wa kina Mandela nchini Afrika Kusini enzi za makaburu, heshima ya Tanzania haiwezi kurudi tena kwenye nafasi yake. Itaendelea kuporomoka hata kuipita ya makaburu.

Huu ni Mwaka Mpya, tujitahidi kuirudisha Tanzania kwenye nafasi yake itakayoonekana ni mpya kutokana na kupotea kwa nafasi hiyo kwa miongo kadhaa. Inabidi tufanye kama walivyosema Wahaya, ‘yangua’, au ‘hapa kazi tu’ ya Mheshimiwa Magufuli.

 

[email protected]    

0784 989 512