Mabadiliko makubwa ya maendeleo ya kiuchumi yanatarajiwa kuonekana Afrika, amesema Katibu Mtendaji wa Baraza la Uchumi Afrika, Dk. Carlos Lopes.

Dk. Lopes ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, katika mazungumzo na Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo.

 

Amefafanua kuwa mpango huo unawasilishwa kwa wadau mbalimbali barani Afrika ili kujadili namna ya kuleta mapinduzi hayo kuinua uchumi wa Afrika.

 

Kwa upande wake, Waziri Muhongo ameahidi kutoa ushirikiano wa dhati katika kuleta mabadiliko hayo yatakayobadili mtazamo wa baadhi ya Waafrika wanaojiona hawawezi.

 

Kwa mujibu wa Muhongo, Tanzania inaweza kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa madini licha ya kukabiliwa na tatizo la idadi ndogo ya wataalamu wa sekta hiyo.

 

“Wataalamu wengi waliopo wamefikia umri wa kustaafu na hivyo kuacha pengo kubwa katika sekta za nishati na madini,” amesema Waziri Muhongo.

 

Ameongeza kuwa wizara hiyo inaendelea kutafuta wafadhili watakaogharimia masomo ya masuala ya petroli na gesi, na kwamba hadi sasa kuna wanafunzi 20 wanaotarajiwa kujiunga na hayo.

 

“Lakini pia vyuo mbalimbali nchini kikiwamo Chuo Kikuu cha Dodoma na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam vitatoa mafunzo juu ya masuala ya mafuta na gesi,” amesema waziri huyo.