Wakati kampeni za urais, ubunge na udiwani zikiendelea nchini, joto la uchaguzi limepamba moto kiasi cha kumponza Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Geita, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Joseph Konyo.
Taarifa za uhakika kutoka Jeshi la polisi Dar es Salaam, zinasema kuwa ACP Konyo ameondolewa eneo hilo la kazi na kurejeshwa Makao Makuu ya Jeshi hilo jijini, atakakopangiwa majukumu mengine.
Nafasi ya Konyo kwa mujibu vya vyanzo vyetu vya habari, imechukuliwa na Latson Mponjeli ambaye kabla alikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa kipolisi wa Tarime/Rorya kulikofumuka mapigano hivi karibuni.
Taarifa za Polisi zinasema kwamba uhamisho huo ni wa kawaida katika utendaji wa jeshi, hata hivyo unaacha maswali mengi kwa sababu ya umelanga kwa kamanda mmoja tu, wa polisi.
Mara nyingi mabadiliko kama hayo, hutokea kwa kugusa makamanda wengi, lakini hadi tunakwenda mitamboni gazeti hili lilithibitishiwa kuwa safari hii ameguswa RPC wa Geita pekee.
Sababu za kuondolewa kwa ACP Konyo zinasema kwamba ni vuguvugu la mabadiliko mkoani humo kwani wananchi wengi hususani vijana wamekuwa ni mashabiki wa mabadiliko na RPC ameshindwa kuwadhibiti.
Taarifa zinasema kwamba hali kama hii imepata kutokea huko mwaka 2010 ambako Kamanda wa Polisi wa Mwanza wakati huo, Simon Siro alihamishwa baada ya kuzidiwa nguvu na vijana walioshinikiza matokeo ya Uchaguzi Mkuu yatangazwe huku chama tawala kikiwa katika hali mbaya ya kushinda.
Matokeo yake, majimbo ya Ilemela na Nyamagana yalinaswa na upinzani, na sasa inatokea tena Geita baada ya ACP Konyo kudaiwa ‘kugoma’ kufanya kazi aliyotumwa na chama tawala huku Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Joseph Musukuma akitajwa kuwa sababu.
Chanzo cha JAMHURI kimeeleza kuwa, sababu za Musukuma kuandaa zengwe hilo ni kutokana na ACP Konyo kuonekana akisimamia majukumu yake kwa haki na si kuibeba CCM kama wao wanavyotaka jambo lililowakera viongozi hao na kuamua kumchongea kwa wakubwa zake.
Musukuma alizungumza na JAMHURI baada ya kupatikana taarifa hizo na mara moja akasema, “Huo ni uongo. Mimi si IGP naomba muulize IGP au Msemaji wa Jeshi la Polisi ambao watakujibu kwa ufasaha. Ila najua kweli amehamishwa.”
Alipobanwa ukweli upi anaoufahamu wa kuhamishwa, alijibu: “Nasema tayari tumeshamuondoa huyo amekwenda kupanga mafaili makao makuu, sasa ushindi ni wetu anakuja RPC mwingine ukitaka zaidi muulize IGP.”
Taarifa zinasema uhamisho wa ACP Konyo aliyekuwa akisifika kwa kufanya kazi zake kwa haki na weledi ndani na nje ya Mkoa wa Geita ulitumwa kati ya Septemba 25, mwaka huu na anatarajia kukabidhi ofisi yake muda wowote ndani ya wiki hii.
‘’Mimi Konyo ni rafiki yangu sana na mara nyingi nimekuwa nikimshauri akubali tu kutii matakwa ya Musukuma ya kupiga mabomu vijana wanaodai ni wapenda mabadiliko, kukamata na kuweka selo vijana wanaoishabikia Chadema. Lakini akawa anataka haki.
“Lengo ni kuwatisha wengine wasiendelee kushabikia chama hicho, maana mimi Musukuma namfahamu akiamua jambo haijalishi wewe ni nani na kama hukufukuzwa kazi basi utahamishwa,” anasema mtoa habari.
“Kuna watu walikuwako hapa, wamehamishwa kwa sababu ya Musukuma,” anasema mtoa habari na kutaja majina ya wahusika waliohamishwa ambao gazeti hili linashindwa kuwataja kwa sababu juhudi za kuwapata kuzungumza nao zilikwama.
“Nikamwambia Konyo akibebe chama chetu kwa sababu tuna hali mbaya kwenye jimbo la Geita, yeye anazubaa,” anasema mtoa habari na kuongeza: “Matokeo yake ameondoka na analetwa kamanda mwingine.”
JAMHURI lilipomtafuta Kamanda Konyo, aliyehamishiwa kwenye mkoa wa Geita Aprili, mwaka jana akitokea Mwanza alikokuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, alikiri kurudishwa makao makuu.
“Ni uhamisho wa kawaida. Kwani wewe umesikia nini?” alihoji ACP Konyo na alipoelezwa kuwa ni masuala ya siasa, akajibu: “Hapana bwana.”
Licha ya Konyo kukataa kuzungumzia kwa undani sakata hilo, taarifa ambazo gazeti hili limezipata zinasema kwamba askari huyo ambaye ni mwanasheria kitaaluma, kilichomponza ni hulka yake ya kufanya kazi kwa haki na weledi.
Taarifa zinasema baadhi ya matukio ambayo kama si busara za ACP Konyo kutumika yangeleta maafa makubwa, ni pamoja na lile lililotokea Septemba 16, mwaka huu pale alipoagiza polisi kuzuia msafara wa vijana wa bodaboda zaidi ya 30 waliokuwa wamevalia magwanda ya CCM huku wakipeperusha bendera za chama hicho kuelekea Uwanja wa Magereza ulipokuwa mkutano wa mgombea wa Chadema, Edward Lowassa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, vijana hao wanaodaiwa kukodiwa na Musukuma kwenda kufanya fujo kwenye mkutano huo kabla ya kuzuiwa na polisi waliokuwa wametanda kwenye barabara zote zinazoingia uwanjani hapo baada ya kupata taarifa za mpango huo siku moja kabla ya mkutano huo kufanyika.
Tukio jingine lilitokea siku hiyo majira ya asubuhi wakati Musukuma akielekea kwenye kampeni zake Tarafa ya Bugando, Jimbo la Geita Vijijini anakogombea nafasi ya ubunge, alipofika katika kijiji cha Bugulula na kuwaamuru walinzi wake wawashambulie wananchi waliokuwa wakionyesha alama ya vidole viwili huku yeye na kundi lake wakionesha dole gumba inayotumiwa na chama chake.
Kutokana na hali hiyo wakazi wa kijiji hicho walishindwa kuvumilia hali hiyo baada ya mwenzao kuumizwa kwa kipigo na walinzi hao na kuamua kujibu mapigo kwa kupiga makelele kuwakusanya wanakijiji ili waanze mashambulizi hali iliyomlazimu dereva wa basi lililokuwa limebeba msafara wa Musukuma na wapambe wake kuliondosha kwa kasi eneo hilo baada ya kuona wanakijiji wamechachamaa.
Hata hivyo, ili kujihami siku iliyofuata Musukuma alifika ofisi za RPC Geita na kuonana na Kaimu RPC, Peter Kakamba na kutoa taarifa za msafara kuvamiwa na watu kwenye kijiji hicho na kuchana mabango ya mgombea wao wa urais, Dk. John Magufuli.
Kakamba alikiri Musukuma kutoa taarifa juu ya uvamizi wake na askari wake kwenda eneo la tukio na kukamata vijana waliotuhumiwa na Musukuma kuchana mabango hayo.
Hata hivyo, Musukuma akapingwa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Kata ya Rwezera, Joseph Mpondi anayedai: “Si kweli kwamba Musukuma amevamiwa.”
Badala yake, alilaani kitendo cha Musukuma kuruhusu walinzi wake kupiga wananchi kwa kuwalazimisha kuunga mkono CCM jambo alilodai halikubaliki.
Akizungumzia vurugu hizo za walinzi wake kupiga raia, Musukuma anakiri kulitambua tukio hilo huku akijitetea kuwa alichokifanya siku hiyo ni kuzuia wafuasi wa upinzani kuchana picha za Dk. Magufuli.
Septemba 23, mwaka huu katika mkutano wa mgombea urais wa CCM, Dk. Magufuli ulikumbwa na sintofahamu baada ya wananchi kuinuka na kumzomea Abdallah Bulembo – Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi taifa.
Bulembo alizomewa kutokana na hatua yake ya kuanza kuhubiri ukanda na kujenga chuki hususani kitendo chake cha kuanza kuwataja viongozi wa Chadema akidai wote wanatoka kanda moja hatua iliyowafanya wananchi hao wa Geita kuonyesha hasira dhidi ya hatua hiyo.
Haikuishia hapo, mkutano wa Magufuli ulipomalizika majira ya jioni umati wa wananchi waliokuwa kwenye mkutano huo uliofanyika Uwanja wa Kalangalala mjini Geita waliamua kujipanga kando ya barabara na kuonyesha alama ya vidole viwili, huku wakiimba: “Lowassa Rais.”
Wakati msafara wa mgombea huyo wa CCM ukipita hali iliyozidisha hasira kwa vigogo hao wa chama na serikali na kuamua kukaa kikao kupanga namna ya kumtoa kafara Kamanda Konyo baada ya kuona hakuna polisi aliyethubutu kuwatawanya vijana wale hata kwa mabomu ya machozi.