Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Mhandisi Deusdedit Kakoko amefanya mageuzi makubwa katika Bandari ya Dar es Salaam, sasa magari yanaruhusiwa kutolewa kwa saa 24.
Taarifa zilizolifikia JAMHURI zinasema Mhandisi Kakoko ametoa maelekezo mahususi kwa watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam kufanya kazi za wateja wote watakaofika Bandarini hapo kila siku kutoa mizigo yao hadi ziishe ndipo waende nyumbani.
“Ni kweli. Nimesema wafanyakazi wanaopitiliza muda wa kazi walipwe mafao ya ziada, ila kama kuna mfanyabiashara anayesubiri kutoa mzigo bandarini na amefika hapo hata kama amefika saa 5 usiku aweze kulipa ushuru na kuwezeshwa kuchukua mzigo wake,” Mhandisi Kakoko ameliambia JAMHURI.
Amesema amebaini wateja wengi walikata tamaa kupitisha mizigo yao katika Bandari ya Dar es Salaam, kutokana na kusumbuliwa hivyo ameamua kudhibiti usumbufu.
Katika kuthibitisha hilo, Idara ya Uhusiano ya Mamlaka ya Bandari imetoa Tangazo linaloeleza kuwa benki zenye matawi yake katika eneo la Bandari zitalazimika kufanya kazi hadi saa 6 usiku.
“Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inapenda kuwatangazia wateja wake, wadau, watumiaji wa Bandari ya Dar es Salaam na umma kwa ujumla kwamba; muda wa kulipia ankara za forodha katika ofisi za TRA na matawi ya benki ya CRDB na NMB yalipo ndani ya bandari sasa umeongezwa hadi saa sita (6) usiku ili kuongeza kasi ya utoaji wa magari bandarini.
“Tayari utaratibu huu umeshaanza kutumika na Mawakala wa Forodha wanashauriwa kutumia fursa hii kikamilifu. Endapo itaonekana kuna mahitaji ya huduma za Forodha na za kibenki baada ya saa sita usiku, muda huu utaongezwa.
“Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania inachukua fursa hii kuwashukuru wadau wote kwa ushirikiano wenu katika kuhakikisha bandari za Mamlaka zinatoa huduma zenye ufanisi na za gharama stahiki kwa watumiaji,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Habari kutoka kwa wafanyabiashara walioomba wasitajwe majina, zinasema wamefurahia utaratibu huo ila kabla ya kupongeza wanajipa muda kuona kama utaendelea au ni nguvu ya soda. Hadi sasa bandari imepewa lengo la kuzalisha Sh trilioni moja na kwa mwaka wa mapato ulioisha walifikia asilimia 68 ya lengo.
Bandari sasa imeanza kupata wateja baada kupiga marufuku mizigo ya wateja kwenda kwenye Bandari Kavu kabla ya eneo la Bandari kujaa mizigo, hali iliyokuwa inaongeza gharama za kusafirisha mizigo kupitia Bandari ya Dar es Salaam kweni wenye ICDs walikuwa wanatumia mwanya huo kukamua wafanyabiashara.