Lakini kulipa ni jambo la lazima kabisa, hakuna kusema kwamba atapata madawa ya bure, madawa ya bure yanatoka wapi? Hatuwezi tukasali misikitini na makanisani, tukamwambia , Mwenyezi Mungu, eee, tuletee kwinini, hawezi kuleta kwinini. Sasa hilo ndilo jambo moja ninalitilia mkazo katika taarifa hii kwamba kabla ya kuanza kusema tumefika kiasi gani cha elimu yenye manufaa.

Lazima ujue tumeongeza uwezo gani wa kulipa elimu hii yenye manufaa, kwa sababu tunanunua vitabu vya kusomesha Watu Wazima hawa na nitakavyoeleza huko baadaye mtaona vina idadi kubwa sana sasa hivi watu wazima wanaosoma. Lakini hatuwezi kuchukua makaratasi wala hatuwezi kuchukua majani ya miti ndiyo wakaandikia kwa makaratasi na kalamu na kadhalika.

Basi, jambo la kwanza tunalolitilia mkazo ni hilo katika taarifa hii kwamba maendeleo yetu yote yanategemea nguvu yetu ya kuyaleta maendeleo hayo na nguvu yetu ya kuyaleta maendeleo hayo ni uchumi tu. Jambo lingine ninalolitilia mkazo katika taarifa hiyo ni kwamba maendeleo yanaletwa na ziada…..

Kama nina shilingi mbili na chakula changu kinahitaji shilingi mbili hizo na nikala shilingi mbili zikesha, hakuna kilichobaki baada ya kula. Basi huna kitu utakachonikamua miye kilete kitu kinaitwa maendeleo, sina maana nguvu yangu yote nimekula. Na kama nina shilingi nne na mimi nahitaji shilingi mbili na mke wangu anahitaji shilingi mbili na tumezila, basi nyinyi kunidai nitoe kitu cha maendeleo kutokana na fedha zangu, nitakuwa sina maana nimekula na baada ya kula hazikubaki na ilikuwa lazima tule kwa kuwa zilikuwa shilingi mbili tu.

Zingekuwa shilingi sita, tungekula shilingi mbili mbili na mbili zingine hizi zikabaki zingeweza kuleta maendeleo yoyote lakini zilikuwa shilingi nne na chakula chetu kinahitaji shilingi nne hizo hizo. Basi tumefuta na wakati mwingine kusema kweli baadhi ya watu wetu chakula chao kinataka shilingi nne lakini wenyewe wanazo shilingi tatu na nusu. Kwa hiyo hula kwa mashaka na huwezi kumtizamia kwamba akabakiza chochote kuleta maendeleo. kwa hiyo na nchi yetu ndiyo hivyo.

Sasa hivi tunadhani kwamba tunao watu milioni kumi na tatu na laki saba ama ni karibu milioni kumi na nne Watanzania sasa hivi. Sasa uchumi wetu ili ulete maendeleo hauna budi kwanza uwapatie mhitaji yao jamaa hao milioni kumi na nne. Kwanza wapate mahitaji yao ya kawaida na halafu kibaki kitu na baada ya kubaki ndicho kilete maendeleo. Sasa hilo nalitilia mkazo katika taarifa hii na matumaini yangu ni kwamba Waheshimiwa mtalizingatia sana jambo hilo hamtalipuuza mkasema ni mambo ambayo yamekwisha semwa basi halafu yataachwa hapa hapa kwenye mkutano na halafu tutakwenda zetu majumbani basi.

Jitihada yetu sharti kwanza itupatie mahitaji yetu haya ya kawaida kabla ya nyongeza. Lazima uchumi wetu ili tubaki hapo hapo ili tupande ngazi kidogo lazima uchumi wetu uzidi ama sivyo hatuwezi kupanda ngazi na tutabaki hapo hapo. Sasa nasema mwaka huu nadhani Watanzania tunao milioni kumi na tatu na laki saba na nusu. Na kwamba uchumi wetu hauna budi utosheleze mahitaji yetu hayo lakini kila mwaka tunaongezeka kwa laki tatu na themanini elfu karibu laki nne. Hilo nalo linafaa likakumbukwa vile vile maana si dogo.

Kwa hiyo uchumi wetu tukitaka ubaki pale pale ama sisi tukitaka maisha yetu yabaki pale pale yaani hayapandi na wala hayashuki kwanza lazima jitihada yetu ilishe wale waliopo, iwatimizie mahitaji yao wale waliopo kila mwaka. Halafu iwatimizie hawa laki tatu na themanini elfu hawa, nayo iwatimizie ya kwao ambayo inataka juhudi zaidi kwa sababu ni lazima uongeze juhudi zaidi kwa mwakani kusudi hawa nyongeza hawa laki tatu na thelathini elfu nao wayapate mahitaji yao. Halafu maisha yetu yatabaki hapo hapo yalipo.

Sasa hawa ninaosema laki tatu na themanini elfu ndio nyongeza ni kwamba hapa Tanzania watu kila mwaka wengine wanazaliwa na wengine wanakufa. Sasa ziko hesabu, wale wanaopiga hesabu wanasema ziko zingine zinaitwa plus na zingine zinaitwa minus. Wale wote wanaozaliwa kwa mwaka, ukipunguza hesabu ya wale wote wanaokufa, tunabaki laki tatu na themanini elfu, alhamdulilah.

Hawa jamaa hawa wanaoongezeka hawana majembe, Hawa wana midomo tu! Hawa si sawa na wahaiaji kwanza wamekuja majitu mazima na majembe yao namiundu yao na wanahamia Tanzania. Wanasema Tanzania iko tupu twende kule, kwa hiyo kila mwaka wanaingia laki tatu pamoja na majembe yao na tunawaonyesha msitu wenu ule pale na nyinyi msitu wenu ule pale. Wanafyeka wanalima na wanapanda. La hasha! Waheshimiwa hawa huja na mdomo tu! (Kicheko)

Mtaniwia radhi katika kulieleza jambo hili maana yake ni jambo la msingi sana hili. Maana jamaa wengine wanalionea haya kulielez hili, Sasa mimi nikilionea haya itakuwa hatari. Mimi nitalieleza. Jamaa hawa laki tatu na themanini elfu hawa wana midomo tu na itackua muda mrefu kabla hajashika mundu huyu. Ni muda mrefu sasa kabla hajampa mundu huyu. Mama ataanza kumpa ufyagio labda kiasi ha miaka sita hivi, ndio anaweza akampa ufyagio hivi lakini kabla ya hapo hapana.

Na kitu tunachokiita maendeleo nikwamba tunwachelewesha hawa kufanya kazi. Wataingia shuleni wakae miaka saba ndio maana ya maendeleo na inapouwa hawakukaa shule ni kwa muda wa miaka saba, tunajiona kwamba hatukuendelea hata kidogo na kwa kweli miaka hii saba tunaona haitoshi, tungependa waingie shuleni na wakae miaka kumi au kumi na moja. Halafu baada ya hapo ndio tuseme sasa nyinyi mnaweza mkatoka mkashika miundu, mkashika mapanga, mkashika mashoka.

Kwa kweli wanafanya kazi lakini hawajatumbukia hasa katika jambo la kazi, shughuli yao kubwa ni kuwalea na maendeleo ni kumlea mtoto kwa muda mrefu sana na hiyo ndiyo tofauti ya binadamu na wanyama. Mnyama kitoto chake kikisha anguka chini puu kanasimama pale pale na kisha kinaanza kukimbia na mama yake. Mtoto wa binadamu huwa katika hali ya unyonge kwa muda mrefu sana.

Anaweza akaleewa kwa muda wa miaka ishirini bado unamlea tu na ndio maana ya Chuo Kikuu kile pale ni kwamba bado tunawalea vijana wale. Kuna madume pale ya miaka zaidiya ishirini katika Chuo Kikuu pale. Madume yale pamoja na akiba mama wale bado tunawalea na yale tunayaita ni maendeleo.Na kadiri utakavyojena Vyuo vil vingi sana ndio unasema Tanzania imeendelea sana maana yake sasa ina vijana wenye umri ule wanaosema malaki na hiyo ndiyo maana ya maendeleo.