Leo Tanganyika ni nchi masikini. Hali ya maisha ya umma iko chini kiasi cha kuaibisha. Lakini kama kila mtu katika nchi, mke kwa mume, atatambua hayo na kufanya kazi ukomo wa nguvu zake, kwa faida ya nchi nzima, basi Tanganyika itaendelea; na maendeleo hayo kila mtu atayapata. Lakini mafanikio haya lazima yagawanywe kwa watu wote. Mtu mwenye kuamini Ujamaa kikwelikweli hawezi kuwanyonya wenzake. Kwa hiyo, ikiwa kikundi cha watu katika nchi yetu watasema kuwa kwa kuwa wanaleta faida kubwa zaidi katika uchumi wa nchi, basi wajichukulie sehemu kubwa zaidi ya mazao haya kuliko hata wanavyohitaji; na kama waking’ang’ania kufanya hivyo watapunguza sehemu yao katika uchumi wan chi, na hivyo watapunguza hatua ya maendeleo yatakayoufaidia umma, basi kikundi hicho kinanyonya, au kinajaribu kunyonya, binadamu wenzao. Kinaonyesha mawazo ya kibepari.

Lazima yatakuwako makundi fulani ambayo kwa sababu ya thamani ya mazao wanayolima au vitu wanavyotengeneza, watatia mali nyingi zaidi katika uchumi wan chi kuliko wengine. Lakini wale wengine pia wanaweza wakawa wanatengeneza vitu na wanalima mazao kiasi kile kile, au pengine zaidi, lakini kwa bahati mbaya haina bei kubwa kwa wakati huo. Kwa mfano: chakula anachokilima mkulima kina manufaa zaidi kwa watu kuliko almasi inayochimbwa Mwadui. Lakini mchimba almasi Mwadui anaweza akadai, kwa haki kabisa, kwamba kazi yake inaingiza feha zaidi katika nchi kuliko mkulima. Lakini kama wakiendelea kudaia kwamba wapate faida yote wao peke yao, na hata sehemu isitumike kumsaidia mkulima, basi hao wana mawazo ya kibepari! Hapo ndipo tabia ya mtu inapohesabiwa katika Ujamaa. Shabaha moja ya kuwa na VyamaVya Wafanya kazi ni kuhakikisha kwamba wafanya kazi wanapata malipo ya haki ya kazi zao. Lakini ujira wa haki lazima uwe wa haki kwa nchi nzima.

Kama ujira huo ni mkubwa kuliko kiasi ambacho nchi inakimudu bila ya kuwapatisha taabu wananchi wengine, basi ujira huo si wa haki. Viongozi wa Vyama vya Wafanya Kazi, na wanachama wao, kama wanaamini Ujamaa kweli, hawatakuwa na haja ya kulazimishwa na Serikali kuweka madai yao ya mishahara katika kima ambacho haja za umma zitakiweka. Lakini kama kuna wenye mawazo ya kibepari miongoni mwao, basi Serikali ya Ujamaa italazimika kuingilia kati na kuwazuia wasiyatumie mawazo yao ya kibepari.

Kama ilivyo katika vikundi, ndivyo ilivyo kwa watu binafsi. Kuna utlaamu au ujuzi fulani ambao kwa sababu fulani unawafanya wale walio nao wapate mshahara mkubwa zaidi kuliko watu wengine. Lakini hata hapo mtu mwenye kuamini Ujamaa kweli kweli atadai ujira kwa kazi yake ambao anajua kuwa ni wa haki kwa kulinganisha na utajiri au umaskini wa nchi yake ambamo yeye anaishi. Hata kulazimisha nchi yake kumlipa mshahara sawa na ule unaopatikana katika nchi tajiri zaidi, isipokuwa kama mawazo yake ni ya kibepari. Ujamaa wa Ulaya ulitokana na mapinduzi ya kilimo, na mapinduzi ya viwanda yaliyokuja baada ya hapo. Mapinduzi ya kilimo yalileta tabaka za makabaila na wasio ardhi; na yale ya viwanda yalileta bepari na mfanya kazi wa viwandani.

Mapinduzi haya yalipanda mbegu za uhasama katika nchi, na uhasama huo ndio ulizaa Ujamaa wa Ulaya. Si hivyo tu, ndio pia uliofanya mashahidi wa Ujaa wa Ulaya wautengeneze Ujamaa katika mawazo yanayokubalika. Vita havikuonekana tena kuwa kitu kibaya, au mkasa, lakini vilihesabiwa kuwa faida, na vya lazima. Kama sala ilivyo kwa Mwislamu au Mkristo, vivyo hivyo ndivyo ilivyokuwa ikihesabiwa vita kwa wale waaminio Ujamaawa Ulaya. Shabaha ya kuleta usawa. Kila kimoja katika hivyo kinakuwa msingi wa maisha yote ya Ujamaa. Mtu mwenye kuamini Ujamaa wa Ulaya hauwezi kuufikiria Ujamaa wake bila ya kufikiria baba ya Ujamaa huo, yaani Ubepari! Lazima nisema kuwa mimi niliyelelewa katika Ujamaa wa Kiafrika naona kuwa upinzani huu ni wa ovyo kabisa. Unaujenga ubepari na kuupa hadhi ambayo ubepari wenyewe hauidai wala hauistahili. Maana maneno yenyewe karibu ni sawa na kusema, ‘Bila Ubepari, na uhasama unaoleta katika nchi, hakuwezi kuwako Ujamaa!’ Narudia tenakusema kwamba watu wanaoamini Ujamaa wa Ulaya kuutukuza ubepari namna hii ni jambo la ovyo.

Lakini kwa upande mwingine Ujamaa wa Kiafrika haukupata faida ya Mapinduzi ya Kilimo au Mapinduzi ya Viwanda. Haukuanzishwa na kuwapo na uhasama wa tabaka za watu katika nchi.

Na kwa kweli, wala sidhani kuna neno linafanana na ‘tabaka’katika lugha zetu za makabila, maana lugha hueleza tabia za wale wanauoisema, na tabia ya ‘tabaka’ haiku katika makabila ya Kiafrika. Shabaha ya msingi wa Ujamaa wa Kiafrika ni ukoo.Mtu mwenye kuamini Ujamaa wa Kiafrika kwelikweli hawaoni watu wa tabaka fulani kama ndugu zake na tabaka nyingine kuwa adui zake. Haungani na wale anaowaita ndugu zake ili awateketeze wale ambao si ndugu zake. Afadhali awahesabu watu wote kuwa ndugu zake: kama watu wa ukoo wake. Ndiyo sababu kifungu cha kwanza cha Imani ya TANU kinasema,’Binadamu wote ni ndugu zangu, na Afrika ni Moja’.

Kwa hiyo ‘Ujamaa’ unaeleza mawazo yetu. Unapinga ubepari, ambao shabaha yake ni kuunda nchi zenye raha kwa msingi wa kunyonyana. Vile vile unapinga aina ya Ujamaa unaotarajia kujenga nchi zenye raha, katika msingi wa uhasama baina na mtu na mtu. Sisi tulio katika Afrika hatuna haja ya kufundishwa Ujamaa, kama vile vileunapinga aina ua Ujamaaunaotarajia kujenga nchi zenye raha, katika msingi wa uhasama baina ya mtu na mtu.

Sisi tulio katika Afrika hatuna haja ya kufundishwa Ujamaa, kama vile vile ambavyo hatuna haja ya kufundishwa demokrasia. Yote hayo tunayo katika jadi zetu, katika makabila yetu yaliyotulea. Ujamaa wa Kiafrika leo unaweza kujifunza kutoka jadi zetu za kutambua umuhimu wa umma, kama vile vile ambavyo zamani tulitambua umuhimu wa ukoo.

Lakini sasa haiwezekani kuufikiria Ujamaa katika mipaka ya ukoo, au ya kabila, au hata ya taifa peke yake. Maana Mwafrika anayeamini Ujamaa hawezi akachora mstari katika ramani akasema ‘Watu walio upande huu ni ndugu zangu, lakini walio upande ule hawana haki na mimi’. Kila mtu katika ulimwengu huu ni ndugu yake.

Wakati tulipokuwa tunapigania kumwondoa mkoloni, tulijifunza faida za Umoja. Tulitambua kwamba mawazo yale yale ya Kiujamaa ambayo katika siku za zamani za makabila yalimpa kima mtu usalama kwa sababu ya kuwa sehemu ya ukoo fulani, lazima yahifadhiwe na kutumiwa katika ukoo mkubwa zaidi wa taifa zima. Lakini tusiishie hapo. Kutambua kwetu kwa faida ya umoja katika ukoo lazima kuelekezwe mbali zaidi: zaidi ya kabila, zaidi ya taifa, au zaidi ya bara zima: mpaka wamejumlishwa binadamu wote. Hilo ndilo lengo lililo dhahiri la Ujamaa wa kweli.