Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (9)

Katika sehemu ya nane, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alisema Rais ndiye aliyekiri kosa la Zanzibar kuingia katika OIC na pili ndiye aliyelazimika kukiri kule Dodoma kwamba utaratibu wa kushughulikia hoja ya Utanganyika ulikosewa lakini mawaziri wake mara zote mbili walitulia tu nakumuacha Rais ndiye akiri kosa na kubeba lawama. Ifuatayo ni sehemu ya kitabu cha Mwalimu Nyerere alichokiandika mwaka 1994 cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania. Endelea…

 

Katiba ya nchi yetu, na utaratibu tunaojaribu kujenga, vinataka kuwa katika hali kama hiyo, Mawaziri ndiyo wawajibike, na hivyo kumlinda Rais, si Rais awajibike, na kuwalinda Mawaziri wake, na tena  kwa kosa ambalo si lake. Watu walioshindwa uongozi Bungeni, hata tukafikishwa hapa tulipo leo, ni Waziri Mkuu na Katibu Mkuu wa CCM.

Hawawezi kukwepa matokeo ya kusarenda kwao Bungeni, na wamtupie Rais ati kwa sababu Rais wetu ni Rais Mtendaji na walipomshauri kusarenda kama wao, alikubali. Tukikubali hoja hiyo hakuna Waziri yeyote atakeyetakiwa kuwajibika kwa kosa lolote; maana kila wakati Rais atatakiwa awajibike badala yake.

Kosa kubwa la Rais (na ni kosa kubwa), ni kule kukubali kushirikishwa kosa, badala ya kuwafukuza wale waliomshauri ashiriki kosa lao. Waziri Mkuu aliposhindwa kupinga hoja ya Utanganyika alipaswa kujiuzulu; lakini aliposhindwa kufanya hivyo, na badala yake akamshauri Rais naye akubali kuwa geugeu, Rais angemfukuza pale pale na kuteua Waziri Mkuu mwingine. Rais hakufanya hivyo; na badala yake Rais naye akakubali kweli kuwa geugeu na kushiriki kosa la washauri wake.

Lakini kosa hilo la Rais, pamoja na ukubwa wake wote, haliwezi kufuta kosa la awali la washauri wake na hoja ya kuwataka wawajibike kwa kosa hilo. Na sasa wanalo kosa la nyongeza la kumfikisha Rais katika hali ngumu na ya fedheha; na kuiingiza nchi yetu katika mabishano ya chuki zinazoweza kuigawa.

Pengine inafaa niseme kwamba inashangaza na kutisha kidogo kuona kuwa kujiuzulu kwa Waziri yeyote kunafanywa kuwa ni jambo la kuvutana au kubembelezana.

Ndugu Ali Hassan Mwinyi aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Muungano. Makosa fulani yalifanyika katika Wizara yake. Hakuwa ameyafanya yeye; yalikuwa yamefanywa na watendaji fulani waliokuwa chini ya Wizara yake. Alilazimika kubeba lawama, akajiuzulu.

Nadhani kuna wengine waliolazimika kujiuzulu kutokana na mkasa huo huo.

Wala kubadili Waziri Mkuu si jambo la ajabu. Ndugu Rashidi Mfaume Kawawa alikuwa Waziri Mkuu wangu kwa muda mrefu. Hakuwa amefanya kosa lolote; lakini nilitaka kumbadili na kuteua Waziri Mkuu mwingine. Nilimwita, nikamwambia hivyo. Tukakaa pamoja, mimi na yeye, tukashauriana na kukubaliana ni nani anafaa kushika nafasi yake. Nikamteua hayati Edward Moringe Sokoine.

Najua kuwa watu wa aina ya Rashidi Kawawa ni adimu sana duniani, hawazaliwi kila siku. Lakini, hata hivyo ni jambo la kushangaza kidogo kwamba viongozi wetu wa mageuzi hata bado hatujafa, wanaona kuwa ni kosa kuwakumbusha kuwa vyeo walivyo navyo ni dhamana. Wanadhani kuwa uwaziri ni usultani: ukisha kuwa sultani utakufa sultani! Nadhani wanakosea. Nchi hii imewahi kung’ oa masultani wa kila aina.

Tukianza kuvumilia masultani wa kuchaguliwa tutapanda mbegu ya masultani wa kuzaliwa. Narudia: kumbadili Waziri, hata Waziri Mkuu, si jambo la ajabu. Anaweza kujiuzulu, anaweza kufukuzwa na nchi isitikisike. Lakini huwezi kumtikisa Rais wa nchi bila kuitikisa nchi yenyewe. Ni vizuri jambo hili likatamkwa wazi wazi na likaeleweka sawa sawa. Maana watu wengine wananong’onanong’ona kuwajibika kwa Rais kana kwamba ni jambo la mchezo mchezo tu. Ni vizuri jambo hili likatamkwa wazi wazi na likaeleweka sawa sawa. Maana watu wengine wananong’onanong’ ona kuwajibika kwa Rais kana kwamba ni jambo la mchezo mchezo tu.

 

Kulazimika kumchukulia hatua Rais wa nchi ni mkasa na balaa kwa nchi yoyote ile. Ndiyo maana tunatakiwa kuwateua na kuwachagua marais wetu kwa uangalifu mkubwa; na ndiyo maana wakisha kuchaguliwa, wanatakiwa wajiheshimu na kuwa waangalifu sana.

 

Ni jambo muhimu kabisa, kwa kweli la kufa na kupona, kufanya kila jitihada ili kujenga na kuimarisha utaratibu na mazoea ya kuchagua na kubadili Rais wa Nchi yetu kwa njia ya kupigiwa kura, baada ya Rais anayetoka kumaliza kipindi chake kimoja au viwili kwa mujibu wa Katiba.

 

Utaratibu mwingine wowote haufai, na ni lazima tufanye kila lililo ndani ya uwezo wetu kuuzuia. Mnapolazimika kuutumia, ni jambo la kufanyaje, si jambo la kurukia.

SURA YA KUMI

Katika suala hili lililotutikisha hapa tulipo watu wa kuwajibika ni Waziri Mkuu, kwa sababu zilizoelezwa kwa kirefu kabisa; na Katibu Mkuu wa CCM kwa sababu hizo na zaidi, maana yeye ndiye aliyekuwa Kiongozi na Mchochezi wa chini chini wa hoja ya Utanganyika. Waziri Mkuu alisarenda ili wenzake wakiongozwa au kuchochewa na Katibu Mkuu, wasije wakamwacha katika mataa.

 

Waheshimiwa wawili hawa walikwisha kuambiwa kuwa watamsaidia Rais wao kama wakijiuzulu. Aliyewaambia ni mimi, kwa niaba ya Rais. Katika kikao cha mwisho nilichofanya na Rais kabla ya kuondoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam, nilimwarifu kuwa nimeufikisha ujumbe wake kwa Washauri wake waheshimiwa.

 

Nilimwambia kwa mdomo na kwa maandishi, kwamba nilihisi kuwa viongozi hao watafanya mshikamano wa kukataa kujiuzulu. Kama watafanya hivyo nilisema, tatizo litakuwa lake. Lakini kwa sababu tatizo halitakuwa lake kama Ali Hassan bali litakuwa lake kama Rais Mwinyi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mimi kwa upande wangu sitakubali liishie hapo.

 

Na kama nilivyohisi, kweli walifanya mshikamano na mkakati wa kukataa kujiuzulu na Rais akawakubalia! Nimeambiwa kuwa ama wao wenyewe au wajumbe wao walitoa kwa Rais sababu mbili kubwa” za kukataa kujiuzulu:

 

(i) Kwanza, Waziri Mkuu akijiuzulu katika hali hii, na Rais akalazimika kuteua Waziri Mkuu mwingine kwa kufuata Katiba ya sasa ati Wabunge, hasa wale “55” watakataa kumpa kibali Waziri Mkuu mpya huyo! Wabunge hawa sasa wanatumiwa kama chaka la kufichia madhambi ya kila namna! Mimi katika ujinga wangu nilidhani kuwa tatizo moja la Rais katika uhusiano wake na Wabunge linatokana na kutokuwa na Waziri Mkuu aliyechaguliwa kwa utaratibu mpya; na akapata kibali cha Wabunge.

 

Kumbe Rais akijaribu kusahihisha hali hii ya sasa, ili achague Waziri Mkuu atakayetaka kibali chao, Wabunge hao hao, hasa “Kikundi cha 55”, watamgomea kwa kutaka kuwaondolea Saulo wao aliyekwisha kuona mwangaza! Naendelea kuwa Toma!

(

ii) Sababu ya pili ya kukataa kujiuzulu, Waheshimiwa wahusika waliyanong’ oneza magazeti na Magazeti yakatangaza, kwamba ujumbe wa kuwanong’ oneza wajiuzulu ulifikishwa kwao na Mwalimu Nyerere: ati wakijiuzulu, itaonekana kuwa Mwalimu Nyerere anaendesha nchi kichini chini kutoka Butiama.

 

Mtu ye yote aliyesoma maelezo haya mpaka hapa atatambua kuwa sikuwa na sababu ya kusita kwenda kuwanong’oneza waheshimiwa hawa ujumbe wa Rais. Nataka wajiuzulu, kwa sababu nilizozieleza.

 

Katika masuala ya nchi mimi si mpole kama Rais Mwinyi, ndiyo maana tulikubaliana nikamfanyie kazi hiyo. Lakini kisiasa mtu mbaya wako hakunong’ onezi kujiuzulu: hupiga baragumu! Pengine anayekunong’oneza kujiuzulu anakutatakia mema, na unaweza kujidhuru mwenyewe kwa kufanya ukaidi.

 

Inawezekana kabisa kwamba Ndugu AIi Hassan Mwinyi, Waziri wa Mambo ya Ndani aliponong’onezwa alijiuzulu hakushangilia. Lakini sina hakika kama angekuwa hapo alipo leo, kama baada ya kunong’onezwa hivyo angetafuta hila za kutojiuzulu. Nchi yetu bado changa; bado inajenga misingi na mazoea yatakayowaongoza viongozi wetu katika kutuongoza na wananchi wetu katika kuwahukumu viongozi wao. Jitihada za kujaribu kusaidia kujenga maadili ya viongozi wetu lazima ziendelee.

 

Waziri Mkuu si mpishi wa Rais, hata tuseme kuwa maadamu Rais mwenyewe anayapenda mapishi yake, sisi wengine tusipoyapenda si kitu. Waziri Mkuu ni Mpishi Mkuu wa Tanzania nzima. Kama hatupendi mapishi yake au kuanza kutupakulia vyenye sumu, au kachoka, au kashindwa kupika, ni wajibu wetu kumwambia mwajiri wake ateue mpishi mwingine.

 

Narudia: sababu peke yake nilizoambiwa za kutojiuzulu kwa viongozi wahusika ni hizo mbili nilizozitaja Lakini sikusikia wala sijasikia kwamba ama wao wenyewe au wajumbe wao, walimwambia Rais kuwa hawastahili kujiuzulu au kufukuzwa ikiwa watakataa kujiuzulu. Na hilo ndilo muhimu; mengine yale ni hila tu za kuwatia watu kiwi na kiini macho.

 

Hatuwezi kujijengea utaratibu wo wote ambao utazuia kabisa makosa yasifanyike, hasa makosa makubwa; lakini tunatazamia kuwa yakifanyika wanaohusika watawajibika. Na katika makosa makubwa ya maadili na utendaji mwenye jukumu la wazi wazi la kuwadhibiti wahusika ni Rais.

 

Mawaziri wake wanapofanya makosa makubwa, na badala yake kujiuzulu waanze kufanya hila na kutafuta visingizio vya kutofanya hivyo, ni wajibu wa Rais kuwafukuza; na tunamtazamia kufanya hivyo. Ni kazi yake mwenyewe, asiyoweza kusaidiwa na mtu mwingine. Mtu anaweza kumsaidia Rais kumnong’oneza Waziri wake kujiuzulu; lakini hawezi kumsaidia kufukuza Waziri wake. Hiyo ni kazi ya Rais peke yake. Asipoifanya kosa ni lake peke yake.

 

Rais alikuwa na nafasi kadhaa za kumfukuza au kumshauri Waziri Mkuu kujiuzulu. Kwanza, ni wakati Waziri Mkuu alipomshauri akubali hoja ya Utanganyika. Nilisema awali kwamba Waziri Mkuu huyo huyo huwezi kumshauri Rais wako akubali hoja, ambayo jana tu ulimshauri apinge, na badala ya kujiuzulu uendelee na kazi yako. Lakini pia Rais huyo huyo huwezi kukubali ushauri fulani leo, na kesho ukubali kinyume cha ushauri huo, kutoka kwa Waziri Mkuu huyo huyo, bila kumfukuza au kumtaka ajiuzulu. Hata kama yeye ndiye angekuwa mkuu wako ungepaswa kujiuzulu, badala ya kukubali ushauri wake. Lakini si mkuu wako, ni mshauri wako tu. Kosa la kukushauri vibaya ni lake; lakini kosa la kukubali ushauri wake mbaya badala ya kumfukuza au kumtaka ajiuzulu ni lako. Rais analo kosa hilo.

 

Rais alipata nafasi ya pili baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa kukataa pendekezo la Serikali la kuitaka ikubali sera ya Serikali Tatu. Azimio la Serikali Tatu lilifanya Bunge la Muungano na Serikali ya Muungano viwe na sera moja na Chama Cha Mapinduzi kiwe na sera nyingine katika suala muhimu kabisa. Halmashauri Kuu ya Taifa ilipokataa pendekezo la Serikali la kukubali hoja ya Utanganyika, Rais alipaswa kutumia nafasi hiyo kukipa Chama na serikali uongozi mpya wenye msimamo. Rais hakutanya hivyo. Alifanya kosa.

 

Nafasi ya tatu ni wakati wa kikao mchanganyiko cha Dodoma kilipokubali kuwa utaratibu wa kutaka kubadili sera ya Chama ulikuwa umekosewa na kikapendekeza lipelekwe kwa wanachama wa CCM.


Inaendelea wiki ijayo