Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (3)
Huu ni mtiririko wa maandishi yaliyo katika kitabu cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania kilichoandikwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka 1994. Sehemu iliyopita Mwalimu alieleza kuzuka kwa suala la Zanzibar kujiunga OIC, na viongozi wakaliombea bungeni mwaka mmoja wa kulitafakari. Endelea…
BUTIAMA 2: 8:1993
Masuala mawili hayo, (i) msimamo wa Zanzibar kuhusu utaratibu wa kuchagua Makamu wa Jamhuri ya Muungano, na (ii) Zanzibar kuingia katika OIC ndiyo yaliyokuwa sababu ya ujumbe wa mara kwa mara kati yangu na Rais wa Jamhuri ya Muungano; na ndiyo Rais na mimi tulikuwa tukiyazungumza Butiama, tarehe 2 Agosti, 1993. Baada ya kuyazungurnza kwa muda mrefu na kuelewana nini la kufanya, Rais akanifahamisha kwamba Waziri Mkuu kamletea habari kwamba:
(a) Wabunge 44 wamejiandikisha kupeleka Bungeni hoja ya kudai Serikali ya Tanganyika ;
(b) Kwa maoni yake hoja hiyo ikijadiliwa Bungeni, baadhi ya Mawaziri wataiunga mkono, na yeye mwenyewe atapata tatizo la kuipinga au kuiunga mkono;
(c) Anapendekeza ifanywe Semina ya Wabunge wote na Viongozi wa Zanzibar , ikiwamo Serikali ya Mapinduzi na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, ili hoja hiyo izungumzwe na ipingwe nje ya Bunge, na
(d) Rais aniombe nikubali kushiriki katika Semina hiyo.
Nilimwambia Rais kwamba niko tayari kushiriki katika Semina iliyopendekezwa na Waziri Mkuu. Lakini kwa kuwa tunakubaliana kwamba hoja ya Wabunge ni matokeo ya msimamo wa Zanzibar kuhusu masuala mawili hayo, itafaa tuyamalize kabla ya kukabiliana na Wabunge. Sikusema kuwa tusipoyamaliza vema sitapinga hoja ya Wabunge; nilisema, nadhani kwa kusisitiza, kwamba hoja hiyo kwa vyo vyote mimi nitaipinga; lakini “hali ya hewa” itakuwa ni tofauti kama hoja inapingwa baada ya Z:mzibar kukubali, au kukataa kubadili msimamo wake, na Selikali ya Muungano itakuwa imeonyesha msimamo gani katika masuala hayo.
DAR ES SALAAM 5:8:1993
Kikao tulichofanya Dar es Salaam kuendeleza mazungumzo haya tulikuwa na Rais na Makamu wake wote, na Waziri Kiongozi na viongozi wengine wa Zanzibar , na Manaibu wa Katibu Mkuu wa CCM. Katibu Mkuu hakuwapo. Pamoja na kwamba mazungumzo hayo yalikuwa magumu, lakini tulikubaliana katika kikao hicho:-
(i) Zamzibar itoke katika OIC;
(ii) Tukubali mapendekezo ya Kamati ya Bomani kuhusu utaratibu mpya wa kuchagua Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano;
(iii) Hoja ya Serikali Tatu ipingwe, na mimi nisaidie kuipinga; na
(iv) Kamati Kuu iitwe ili itoe uamuzi wake rasmi kuhusu masuala haya.
Siku hiyo baadhi ya Wabunge, Viongozi wa hoja ya Serikali Tatu, waliomba kuja kuonana nami Msasani. Tulizungumza kwa muda mrefu; na wote walisema; wakieleza sababu zao za kudai Serikali ya Tanganyika. Nilisisitiza kwao kwamba zote zilikuwa ni sababu za kuwataka wawadhibiti Viongozi wetu na kuwataka watuongoze kwa kufuata sheria na, Katiba ya Nchi yetu. Hapakuwa na sababu hata moja ya kuwafanya wadai Serikali ya Tanganyika , maana hata ukiwa na Serikali ya Tanganyika bado Viongozi wetu wanaweza kukiuka sheria na Katiba ya Nchi, na dawa haitakuwa ni kuigawa nchi tena na kuongeza Serikali, bali ni kuwadhibiti viongozi wahalifu. Baadaye hoja hizi nilizirudia Bungeni.
Siku iliyofuata, tarehe 6:8:1993, mirni niliondoka kwenda Brussels , Ubelgiji, kumwakilisha Rais katika mazishi ya Mfalme wa nchi hiyo. Huku nyuma Kamati Kuu iliitwa. Niliporudi tarehe 9:8:1993 Kamati hiyo ilikuwa inakutana Dares Salaam. Ilipokwisha kufikia uamuzi wake, Viongozi waliotumiwa kuja kunieleza uamuzi huo walikuwa ni Waziri Mkuu, Katibu Mkuu wa CCM, na Waziri Kiongozi. Msemaji wao alikuwa Katibu Mkuu.
UAMUZI WA KAMATI KUU: 10:8:1993
(i) OIC: Zanzibar itoke;
(ii) MAKAMU WA RAIS: Mapendekezo ya Kamati ya Bomani yakubaliwe;
(iii) HOJA YA SERIKALI TATU: Ipingwe;
(iv) SEMINA: Isifanyike; badala yake mazungumzo yafanyike katika Kamati ya Chama ya Bunge.
Baadaye Rais alinifahamisha kwa simu kwamba yeye sasa alikuwa hakusudii kwenda kusema na Wabunge, lakini akanitaka mimi niende. Inaelekea kuwa baadhi ya viongozi waliona kuwa Rais akienda kusema atawazuia wabunge wenye hoja kutoa dukuduku zao hila hofu. Kwa kuwa nilikuwa nafahamu kwamba baadhi ya viongozi wa Chama na Selikali walikuwa na maoni hayo hayo kuhusu kushiriki kwangu, nilimwambia Rais kwamba hata na mimi nisiende kusema Bungeni. Na kwa vyo vyote vile kushiriki kwangu kulitegemea kushiriki kwake; lakini kama yeye haendi kusema na Wabunge, mimi nitakwenda kama nani na kutafuta nini?
Kwa hiyo yafaa wote wawili tusiende. Tukakubaliana hivyo.
NYUMBANI KWA RAIS: 13:8:1993
Baadaye Rais akanipigia simu tena na kuniambia kuwa Waziri Mkuu alipoelezwa makubaliano yetu ya kutokwenda kusema na Wabunge amechachamaa. Nikamwomba Rais amwambie Waziri Mkuu asiondoke ili niende, wote watatu tuzungumze la kufanya. Nikaenda; tukazungumza kwa muda mrefu. Waziri Mkuu akanisihi sana sana, niende Bungeni, nikasaidie kupinga hoja ya Serikali Tatu. Nikakubali, nikisisitiza mambo mawili:
(i) Rais awe ndiye msemaji mkuu, na rnirni niwe msaidizi tu; na
(ii) Uamuzi wa Zanzibar kutoka katika OIC; na wa kukubali utaratibu wa kuchagua Makamu uwe urnekwisha kutangazwa.
Nilisisitiza kwarnba itafaa uamuzi wa Zanzibar kutoka katika OIC uelezwe wazi wazi, na bila kuvunga vunga, ili rnakali ya Wabunge, kama ikiwezekana, yawe yamepunguzwa kabla hatujapinga hoja ya Serikali Tatu. Tulipokwisha kukubaliana hivyo Waziri Mkuu alifurahi sana na kusema kwa Kiingereza: “I could not take no for an answer! Nisingekubali jibu la Hapana! Tukaachana
BUNGENI: 14:8:1993
Kesho yake tarehe 14:8: 1993 tulikwenda Bungeni.
(i) Nadhani jana yake Waziri Mkuu alikuwa amekwisha kutanga uamuzi wa Zanzibar kutoka katika OIC, na wakubali mapendekezo ya Kamati ya Bomani kuhusu utaratibu wa kuchagua Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Na kwa upande wa Zanzibar , Rais wa Zanzibar alikuwa amekwisha kufanya vivyo hivyo. Bungeni Waziri Mkuu alieleza sababu za kutuomba tusema na Wabunge.
(ii) Rais alieleza historia ya kisa cha OIC na uamuzi wa Zanzibar kujitoa. Akapinga hoja ya Serikali Tatu.
(iii) Mimi nilieleza kwa kirefu sana ile rnigogoro miwili ya awali, na kupinga hoja ya Serikali Tatu. Katika kufanya hivyo nilieleza historia ya Muungano wa Serikali Mbili, badala ya
Muungano wa Serikali Moja au Shirikisho la Serikali Tatu.
MFUMO WA SERIKALI MBILI:
Kisanduku 1
Nchi mbili zinapoungana na kuwa Nchi moja mifumo ya kawaida ya miundo ya Katiba ni miwili: Muungano wa Serikali Moja, au Shirikisho la Serikali Tatu. Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta Serikali yake na nchi mpya inayolizaliwa itakuwa ni nchi moja yenye Serikali moja. Katika mfumo wa pili kila Nchi itajivua madaraka fulani ambayo yatashikwa na Serikali ya Shirikisho, na itakuwa na Serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki. Mambo yatakayoshikwa na Serikali ya Shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika mamlaka ya Nchi zilizoungana, basi kwa kweli nchi hizo zita hazikuungana kuwa Nchi Moja, bali zinaendelea zinaendelea kuwa Nchi Mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo fulani fulani.
Nchi za Afrika Mashariki zilikuwa katika hali kama hiyo kabla ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Zilikuwa ni Nchi Tatu zenye ushirikiano mkubwa, lakini hazikuwa Nchi Tatu zilizoungana kuwa Nchi Moja yenye muundo wa Shirikisho. Shirikisho halisi la Nchi Mbili litakuwa ni Nchi Moja yenye Serikali Tatu, Serikali ya Shirikisho, na Serikali Mbili za awali zilizoungana kuzaa Nchi mpya moja.
Tanganyika na Zanzibar zilipoamua kuungana na kuwa Nchi Moja, tungeweza kufuata mmojawapo wa mifumo hiyo ya kawaida. Lakini tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zanzibar na ukubwa wa Tanganyika. Zanzibar ilikuwa na watu laki tatu (300,000) na Tanganyika watu milioni kumi na mbili (12,000,000). Muungano wa Serikali Moja ungefanya ionekane kama Tanganyika imeimeza Zanzibar . Tulikuwa tunapigania Uhuru na Umoja wa Afrika; hatukutaka tudhaniwe, hata kwa makosa, kwamba tunaanzisha ubeberu mpya!
Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa Serikali Moja. Shirikisho la Serikali Tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika . Zanzibar ingeendesha Serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha Serikali ya Shirikisho; na Tanganyika ingefanya vivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa Tanganyika ndio hasa ungeendesha Serikali ya Shirikisho. Kwa hiyo Tanganyika ingeendesha Serikali yake ya watu 12, 000, 000, na pia ndiyo ingetoa sehemu kubwa ya kuendesha Serikali ya Shirikisho la watu 12,300,000.
Ni Watu wanaofikiri kwa ndimi zao wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yo yote kati ya hizo ingekuwa ndogo. Gharama ya Serikali ya Tanganyika isingekuwa ndogo, (waulizeni Wazanzibari), na wala ya Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo, hata bila ya gharama za mambo yasiyo ya Shirikisho. Na gharama zote hizo kwa kweli zingebebwa na Tanganyika.
Kwa hivyo ilitupasa tujiulize kwa nini tunataka kuibebesha Tanganyika gharama zote hizo; na hasa kwa nini tunataka Serikali ya Tanganyika ? Hivi tuna hofu ya kwamba Tanganyika , bila kuwa na Serikali yake, itaoekana kuwa imemezwa na Zanzibar ? Hofu yetu ni kwamba tukiwa na Serikali Moja Tanganyika itaonekana kuwa imeimeza Zanzibar . Basi na tutafute muundo ambao utaiondolea Zanzibar hofu hii ya kumezwa, bila kuibebesha Tanganyika mzigo wa kuendesha Serikalli mbili zenye uzito unaolingana.
Hivyo ndivyo tulivyofanya, na hiyo ndiyo asili ya muundo wa Muungano wa Serikali Mbili. Badala ya kutungua mfumo uliopo kama wapumbavu, tulitazama hali halisi yetu ilivyokuwa, na tukabuni mfumo utakaotufaa zaidi.
Labda ni vizuri kukumbusha kwamba shabaha ya baadhi yetu ilikuwa ni kuziunganisha Nchi za Afrika ya Mashariki ziwe Nchi Moja.
Na wakati Zanzibar na Tanganyika zinaungana, Kenya , Uganda na Tanganyika zilikuwa katikati ya mazungumzo ya kutafuta uwezekano wa kuungana. Kama jambo hilo lingetokea, nina hakika kabisa kwamba mfumo wa Nchi mpya ambayo ingezaliwa ungekuwa ni wa Shirikisho; ama Shirikisho la Nchi Tatu zenye Serikali Nne, au Shirikisho la Nchi Nne zenye Serikali Tano.
Kwa kweli hata kesho Nchi za Afrika ya Mashariki zikiamua kuungana, na Tanzania ikawa ni mshiriki, naamini kuwa ni rahisi zaidi kushirikisha Tanzania yenye Serikali Mbili – ya Zanzibar na ya Tanganyika – kuliko Tanzania yenye Serikali Mbili, ya Tanzania na ya Zanzibar.
Wapendao Utanganyika watakuwa wazalendo zaidi, badala ya kuwa wasaliti, wakiazimia Afrika ya Mashariki iliyoungana kuwa Nchi Moja, kuliko Tanzania iliyotengana ikawa nchi mbili.