‘Kutegemea kubaya kupita kote ni kutegemea mtu mwingine kwa mawazo

Katika sehemu iliyopita, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alisema hata angekuwa anafuata sera za kibepari, angejenga viwanda. Anasema mabepari ndiyo walioanza kujenga viwanda, na viwanda vyenyewe havikuwa na sera. Ifuatayo ni sehemu ya hotuba ya Mwalimu aliyoitoa katika kilele cha Sherehe za Mei Mosi, mwaka 1995 mkoani Mbeya.Juzi juzi, wakati nipo pale Dodoma , vijana walinikumbusha. Mwalimu, ulipotoka, uliacha viwanda vya nguo vya umma kumi na viwili. Kati ya viwanda hivyo kumi na viwili, kumi vimefungwa na viwili vilivyobaki kimoja hatujui hata kama kitapata pamba. Tusipoangalia, vyote viwili vilivyobaki vitafungwa.

Juu ya Mashirika ya Umma

Nataka kusema kidogo juu ya hiki kitu kinachoitwa mashirika ya umma. Sijui yananuka? Hata hivyo, hata kama yananuka, nataka kujua kwa nini yananuka. Lazima tujiulize kwa nini yananuka. Sababu ya kusema hivi ni kwamba mimi nilikuwa sijui, lakini vijana walinikumbusha wakaniambia “Mwalimu, ulipondoka, uliacha kumi na mbili”, Mimi kitu kimoja nilichokuwa nakifikiria ni kwamba sasa viwanda vyetu vya nguo vilikuwa vinafikia shabaha ile tuliyokuwa tunataka ya kuweza kutumia asilimia themanini na tano (85%) ya pamba hapa nyumbani.

Nilipowauliza vijana kwa nini viwanda kumi vimefungwa na viwili vilivyobaki vipo katika hatari ya kufungwa, nilielezwa kwamba kuna sera inayoitwa sera ya ubinafsishaji. CCM wasiogope sana , na ninyi mniwie radhi kwa kusema CCM, maana ndiyo yenye serikali inayotawala.

 

Sasa mimi nifanyeje? Wala CCM wasije wakaninung’unikia, maana ndicho chama kinachotawala, na wale wa vyama vingine wasije wakasema “mbona Mwalimu umesema kama unaipendelea CCM? Aka! Kama wanataka niwabomoe, naweza kuwabomoä, lakini sitaki.

 

Mimi nataka kueleza hali yetu ilivyo hivi sasa na nataka kusema; mosi, tunatoka wapi, tuko wapi na tunataka kwenda wapi. Pili, kama tunataka kwenda huko, tufanye nini tusije tukashitukia tunapelekwa mahala ambako siko tunakokusudia kwenda. Na hiyo ndiyo shabaha yangu.

 

CCM imebadili sera ya Azimio la Arusha

CCM imebadili sera ya Azimio la Arusha. Mimi sina ugomvi hata kidogo. Naweza kusema nina ugomvi wa kiitikadi, ingawa sijasema “mbona mnaacha sera yetu ina ubaya gani?” Aidha, sina ugomvi wa msingi wa kitaifa kwa sababu mnaweza mkaacha Azimio la Arusha na baadaye mkajenga uchumi imara tu kwa manufaa ya wananchi. Ziko namna nyingi za kufanya hivyo na si lazima kufuata Azimio la Arusha.

 

Sera za CCM

Sasa CCM wanazo sera ambazo zimefafanuliwa katika kakitabu haka kanakoitwa Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka ya Tisini. Hii imetengenezwa na ndiyo marekebisho ya Azimio la Arusha. Ndiyo sera yao mpya baada ya kusahihisha Azimio la Arusha. Kuna sehema ninayotaka kuitumia kueleza hayo ninayotaka kuyaeleza ambayo inahusu mashirika ya umma.

 

Sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya Umma

Kuhusu mashirika ya umma, sera yake inasema. “Mashirika ambayo ni ya msingi na nyeti kwa maendeleo ya taifa kama bandari, reli, posta ma simu, nishati na mabenki ya umma yaliyopo, yaendelee kumilikiwa na dola. Hata hivyo, wananchi wataweza kuuziwa sehemu ya hisa katika mashirika hayo yote na mashirika haya yanaweza kuingia ubia na makampuni binafsi, mradi tu kwa uwiano unaolifanya shirika kuendelea kuwa la dola”. Mimi nilipokuwa nasoma jana nikaafiki na kukubali. Sina ugomvi na hilo na sina ugomvi kabisa kwani ndivyo tulivyosema katika Azimio la Arusha. Lakini mambo haya lazima yabadilike. Sasa sina ugomvi na hili.

Pili: “Mashirika ya umma ambayo yanaendelea kwa ufanisi lazima yaendelee kuwa ya dola kwa lengo la kuendelea kuwashirikisha wananchi katika umilikaji. Mipango itaandaliwa ya kuwawezesha wananchi kununua hisa katika mashirika hayo. Pia mashirika ambayo yanahitaji mtaji au kupenyeza sayansi na teknolojia ya kisasa yataweza kuingia katika ubia ili kutimiza azma hiyo. Aidha, kwa mashirika ambayo serikali italazimika kumiliki, mashirika haya itabidi yaendeshwe kibiashara”. Mimi nakubali mia kwa mia, sina maneno na wala sioni tatizo na hilo .

Tatu: “Kwa upande wa mashirika ambayo yanaweza kufanya shughuli zake kwa faida lakini yana matatizo mbalimbali kama ya ukosefu wa mtaji, madeni makubwa katika mabenki, menejimenti mbovu na kadhatika, dola itachukua hatua ya kulazimika kuondoa menejimenti mbovu, kuimarisha mtaji kwa kuwauzia wananchi hisa na kuingia ubia na vyombo vingine vya kiuchumi au kuyakodisha kwa mteja mwenye uwezo wa kuyaendesha kwa faida”. Mimi hiyo bado naikubali na sina matatizo.

Nne: “Mashirika yaliyo sugu [“mashirika yaliyo sugu” tena Kiswahili kizuri sana ] kwa kufanya shughuli kwa hasara yatakodishwa, ama kuuzwa au kufungwa kwa kutilia maanani zaidi jawabu ambalo ni la maslahi zaidi kwa taifa”. Sasa mimi nasema hilo bado nalikubali kwani shughuli hii imekuwa inaendelea. Nimesikia kwamba shirika, halikuwa ni shirika la umma, lilikuwa ni Benki ya Ushirika na Maendeleo Vijijini (CRDB), peke yake ndicho chombo cha namna hiyo ambacho kimepitapita kuuza hisa. Mengine sijayasikia, yanaweza kuwa yapo.

Uuzaji wa mashirika ya umma

Uuzaji wa mengine, ambayo sivyo sera inavyosema [sera haisemi mashirika yanayoendeshwa kwa faida yauzwe hata kidogo], sijui yanavyouzwa. CRDB wamepita kwangu pale wameniomba ninunue hisa. Nitapata wapi mimi? Hata hivyo, wamepitapita wanaomba watu wanunue hisa; wanakwenda kwenye vyama vya ushirika na wanawaomba watu binafsi. Angalau, hicho ni kitendo cha kushirikisha watu ambacho wamekifanya na watu wametumia fursa hiyo kama sera inavyosema.

 

Mengine tunasikia yanakwenda tu. Eti sasa ni kwamba, kwa mfano, kile Kiwanda cha Sigara, ni cha umma ni chetu wote pamoja. Najua wewe huna hisa, mimi sina hisa na wala hakuna mtu mwenye hisa. Lakini ni cha umma na kinafanya shughuli zake kwa faida.

Tofauti kati va shirika ya umma na shirika/kampuni binafsi

Nimechukua mfano wa kiwanda ambacho kinafanya shughuli zake kwa faida. Kama kinafanya shughuli zake kwa faida, wote tunapata faida. Chukua mfano wa viwanda viwili vinavyoendeshwa vizuri na vinapata faida. Kimoja kama kile cha sigara na cha pili ni cha watu binafsi. Sasa tofauti yake ni nini? Hiki cha watu binafsi kinalipa kodi ya serikali na hiki cha umma kinalipa kodi ile ile na kwa mujibu wa sheria ile ile. Kwa hiyo, hivyo vyote vinalipa kodi ile ile juu ya faida kwa asilimia ya faida zao kwa mujibu wa sheria. Baada ya kodi, pato lililobaki linagawanywa kwenye hisa. Kile cha umma pato lake linakwenda kwa serikali: kwa umma. Hiki kingine, faida yake inakwenda kwa watu binafsi wachache.

 

Ndiyo maana, mpaka leo, mimi napendelea hiki cha umma zaidi kuliko kile cha watu binafsi. Vyote vinafanya biashara nzuri tu na vinalipa kodi ya serikali kama kawaida na vinawapa faida iliyobaki wenye kiwanda. Hata hivyo, hicho cha kwanza, cha umma kinawapa faida iliyobaki wenye kiwanda hicho ambao ni umma, na msimamizi wake ni serikali. Kwa hiyo, serikali ndiyo inayochukua mapato yake kwa niaba ya wananchi wake. Mimi mpaka leo, hata ninyi mngesemaje, bado nakipenda hiki cha umma.

 

Tukitaka kuongeza viwanda vya watu binafsi, tuongeze tu!

Kama tunasema sasa hivi tunataka kuongeza vile viwanda vya watu binafsi, tuongeze tu! Nani atatuzuia? Ongezeni vile vya watu binafsi. Viongezwe kwa wingi kabisa! Hata hivyo, mnapochukua hiki cha umma, kwa maana niliyoieleza, mkasema eti mnataka sasa kiwe cha wananchi moja kwa moja ili na mimi Nyerere niseme “sasa nina hisa pale”, mimi siafiki. Watu wangapi mtakuwa na hisa? Hebu niambieni, wangapi?

 

Mnachukua mali yetu wote kabisa, kiwanda cha sigara kile kina mali , kinapata faida na serikali inaitumia kuongezea fedha za kodi na tunaifanyia kazi ya umma. Mnavyosema leo ni kwamba mmegundua njia moja nzuri zaidi ya kushirikisha wananchi katika uchumi. Mimi nawambineni: ongezeni viwanda.

 

Muwashawishi wananchi wa Tanzania waongeze viwanda. Wasaidieni kuongeza viwanda. Lakini, hiki cha wote, mnataka kuwapa watu wachache, halafu mnasema ndiyo ushirikishaji? Mimi sielewi maana yake. Hii ni mali yetu wote pamoja: ni mfuko wa pamoja tunachota inatusaidia katika elimu, afya na mahitaji mengine.

 

Sasa hivi tunayo matatizo ya ukusanyaji kodi. Kiwanda hiki hakina matatizo hata kidogo. Kinaendeshwa vizuri kwa faida. Kwa hiyo, tunacho chombo ambacho kinatoa faida. Kinatusaidia. Leo shule na hospitali zina matatizo kwa sababu kodi mbalimbali hazikusanywi. Lakini kiwanda hiki kinalipa kodi yake kama kawaida. Miongoni mwa wale wanaokwepa kulipa kodi, si mmoja wao. Viwanda vya umma si mmoja wapo hata kidogo. Vinalipa kodi zake kama kawaida, havikwepi kulipa hata senti moja. Halafu, kinapopata faida, tunabaki nayo na tunafanya shughuli za wananchi. Hiki mnasema leo tukigawanye tuwashirikishe wananchi kwa kukimiliki moja kwa moja. Wangapi mtamiliki: ninyi wangapi? Itakuwa ni kuchukua fulani na fulani tu! Kiwanda ambacho ni chetu wote kabisa na faida itakapobaki, badala ya kwenda Hazina, iende kwa wewe na mimi!

 

Ndiyo tumekibinafsisha na hii ndiyo sera mpya ya kuleta manufaa Tanzania ! Hii ndiyo mbinu mpya imegunduliwa? Ujamaa mpya huo! Huo ni unyang’anyi tu wa mali yetu wote.

 

Kutegemea mtu mwingine kwa mawazo ni kubaya kupita yote kabisa

Hili ni jambo la upumbavu. Katika masuala ya uchumi wa nchi, lazima tufanye tofauti baina ya kujitajirisha wachache na kuleta manufaa ya watu wengi. Sasa, sera hii itazaa mamilionea sasa hivi na sio baadaye, lakini watakuwa mamilionea watano. Hata hivyo, wakati huo huo, pia itazaa masikini na Tanzania itakuwa na masikini wengi sana .

 

Sasa nataka niseme kuwa nimetumia Kiwanda cha Sigara kama mfano tu kuonyesha kwamba nchi haiwezi kuendelea hata kidogo kwa kupuuza viwanda. Sasa tunafunga viwanda. Sijui hiyo inaitwa sera ya kuondoa ama kuzuia viwanda, lakini haya ni matatizo ambayo tunayo na usifikiri ni Tanzania peke yake. Nilikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kusini. Nimepita pita Afrika, Asia na Amerika ya Kusini. Nimeshuhudia mawazo na mipango ya aina hiyo kuwa ndiyo inayoongoza na kutawala. Hilo ndilo nililowambia hivi punde kwamba, wakati Waingereza wanatawala India , waliwaambia Wahindi. “Hapana kutengeneza nguo.”

 

Hali hiyo inaendelea na wala haijabadilika mpaka leo kwani bado duniani tunaona nchi zenye viwanda huvibana vi-nchi vidogo viache mambo ya viwanda. Sasa taabu yetu, wala si Tanzania peke yake kuna vi-nchi vingi, ni kwamba viongozi wetu hawakatai. Wanakubali tu. Lakini sisi ni madodoki? Dodoki ulitumbukize katika maji, hata yenye takataka, linazoa tu!

Kusema kweli, duniani watu wanafikiri kwamba labda sisi ni masikini. Lakini umasikini mbaya kulio wote ni umasikini wa mawazo. Ni mbaya sana . Duniani kuna kujitegemea na kutegemea. Unaweza kutegemea, lakini kutegemea kokote ni kubaya sana . Kwa hali yo yote ile, kutegemea kubaya kupita kote kabisa ni kutegemea mtu mwingine kwa mawazo. Ni kwa ovyo sana kunakunyima utu wako.

 

Watu tunaafikiana na wazo. Lakini mawazo ambayo wazi wazi ni ya kijinga lazima tuyakatae. Kwa sababu mtu mwenye akili akikupa mawazo ya kipumbavu, usipoyakataa, atakudharau. Narudia, mtu yeyote mwenye akili akikupa mawazo ya kipumbavu na wewe una akili na unajua ni ya kipumbavu na ukayakubali, atakudharau. Sasa hatuwezi tukakubali mambo ya kipumbavu Tanzania .

 

Itaendelea