- Wananchi kukata tiketi kupitia mitandao ya simu
Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) imesema maandalizi ya maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) maarufu kama ‘Sabasaba’ yamekamilika kwa asilimia 79.
Aidha imesema kuwa maonesho ya mwaka huu yatakuwa ya kipekee ukilinganisha na miaka nyuma ambapo wananchi wataweza kukata tiketi kwa njia ya mitandao ya simu.
Hayo yamebainishwa leo Juni 20, 2021 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade, Latifa Khamis wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maonesho hayo.
“Tantrade kama kawaida inaendelea na maandalizi yake ya maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam ambayo yanatarajiwa kuanza Juni 28 hadi Julai 13, mwaka huu.
“Maonesho ya mwaka huu tunatarajia yatakuwa ya kipekee kwani kuna mambo mbalimbali yatakuwepo. Mojawapo wananchi kuweza kukata tiketi kupitia mitandao ya simu ambapo tumeshirikiana na Vodacom lakini pia Utamaduni wa kukata tiketi hapa hatutauondoa kwahiyo mtu atachagua akate tiketi kwa kutumia njia gani,” amesema.
Pia amesema kutakuwa na milango ya kielekloniki ambapo wananchi na magari mengine wataweza kuingia kupitia milango hiyo tuliyoiandaa ambayo itapunguza usumbufu na msongamano.
Amebainisha kuwa mpaka sasa Nchi 25 zimethibitishwa kushiriki, Kampuni za nje 223 na Washiriki wa Ndani 2979.
“Haya ni mafanikio makubwa kwasababu siku bado lakini kampuni nyingi tayari zimethibitisha na hii haijawa kwa bahati mbaya kama mnavyofahamu Rais Dkt . Samia Suluhu Hassan amekuwa akisafiri Nchi mbalimbali kuitangaza Tanzania kwahiyo haya ni matokeo.
“Lakini kama mnavyofahamu maonesho yetu sio ya kawaida watu tu kuja kutembea yana mambo mengi pia ikiwemo kuleta ajira pamoja na kuchochea uchumi wa Nchi yetu,” amefafanua.
Ameongeza kuwa katika Maonesho ya hayo, pia kutakuwa na program tisa (9) a na siku za mataifa saba ambazo zitafanyika kwa siku tofauti tofauti.
“Kutakuwa na Siku ya Taifa ya China, Egypt, Urusi, India, Japan, Korea na nyingine. Pia kutakuwa na onesho la roboti ambazo tayari zimeshaingia na ziko kwenye majaribio.
“Nitoe wito kwa Watanzania wasiache kutembea maonesho haya kwani sisi tunaamini maonesho ni kituo cha fursa zote, hivyo wajitokeze kwa wingi kutembelea,” amesema.
Ameongeza kuwa viingilio havijabadilika ambapo mtoto ni Sh. 1000 na mkubwa ni Sh. 3000.