Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Watanzania kukemea vitendo vya ukatili ulioshamiri dhidi ya wanawake na watoto na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa dhidi ya wahusika.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Kanda ya Magharibi lililofanyika katika Ukumbi wa NSSF mkoani Kigoma. Ametaja baadhi ya vitendo hivyo kama mauaji, ubakaji, ulawiti, kupigwa, kunyanyaswa, kunyimwa haki za kumiliki ardhi na mali nyingine za familia, urithi, fursa za elimu, ukeketaji, adhabu kubwa zisizowiana na kosa alilotenda mtoto.
Makamu wa Rais amesema baadhi ya vitendo hivyo vinafanywa na wanafamilia au ndugu wa karibu na sehemu kubwa ya vitendo hivyo havitolewi taarifa kwenye vyombo vya sheria ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa. Ameongeza kwamba wakati mwingine, baadhi ya mila na desturi katika jamii hutumika kuwakandamiza wanawake na watoto.
Aidha Makamu wa Rais ametoa rai kwa Kongamano hilo ambalo idadi kubwa ya washiriki wake ni wanawake na ambao ni walezi wa familia, kuelekeza nguvu pia katika kumlinda mtoto wa kiume ili kumhakikishia usalama wake. Amesema uwekezaji jitihada kidogo kwa mtoto wa kiume imepelekea mtoto wa kiume kujikuta katikati ya matatizo lukuki yakiwemo matumizi ya madawa ya kulevya, ushoga na aina nyingine za ukatili.
Makamu wa Rais ili kuendelea kuongeza mchango na ushiriki wa Wanawake katika utunzaji wa mazingira na kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia, hakuna budi kongamano hilo kujadili na kuibua mikakati madhubuti na yenye kutekelezeka ili kufikia malengo hayo.
Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha utoaji wa elimu na hamasa kwa umma kuhusu utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia. Amesema elimu kwa umma na hamasa ni muhimu katika utunzaji endelevu wa mazingira kwa kuwa tabiawatu ndiyo kisababishi kikuu cha uharibifu wa mazingira.
Makamu wa Rais ametoa rai kwa taasisi kama Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), TEMDO na nyingine kutafiti na kutengeneza teknolojia mbalimbali zinazotumia nishati safi na zenye gharama nafuu ili ziweze kusaidia uhamaji kwenda kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia. Aidha ametoa wito kwa wafanyabiashara wakubwa na sekta binafsi kwa ujumla kujitolea kusaidia majiko na teknolojia rahisi kwa shule na vituo vinavyolea watoto na watu wenye mahitaji maalum.
Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2024 – 2034 ambao unalenga kuhakikisha 80% ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Vilevile amesema Serikali imesaini makubaliano ya awali na wawekezaji kuhusu Ruzuku ya Sh. Bilioni 8.64 kwa ajili ya nishati safi ya kupikia, ambapo jumla ya majiko 452,455 yamepata ruzuku kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa wananchi kwa gharama nafuu.
Hali kadhalika Makamu wa Rais amewasihi wanawake kushiriki kikamilifu katika kutoa hamasa kuhusu jukumu muhimu la kujiandikisha kupiga kura, kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kushiriki kuchagua viongozi wanaowapenda. Amesema ni jukumu la kila mmoja kujenga na kudumisha umoja, amani, mshikamano na kuepuka vurugu katika mchakato wote wa uchaguzi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema dhima ya kongamano hilo ni kuhimiza wanawake na jamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi. Amesema pia Kongamano limedhamiria kuhamasisha wanawake kukaa na familia pamoja na kupata muda mzuri zaidi ili kujenga malezi na makuzi kwa mustakbali wa familia bora.
Kongamano la wanawake kanda ya magharibi ni sehemu ya maadhimisho ya Siku Kimataifa ya Wanawake Duniani ambayo kilele chake kitakuwa tarehe 8 Machi, 2025 Jijini Arusha. Kongamano hilo lina kaulimbiu isemayo ‘Mchango na ushiriki wa Wanawake katika matumizi ya nishati safi na utunzaji wa mazingira’.











Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhi majiko ya gesi kwa wanawake wawakilishi kutoka Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kigoma ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Kanda ya Magharibi ikiwa ni shamrashamra kuelekea Siku ya Wanawake Duniani linalofanyika katika Ukumbi wa NSSF mkoani Kigoma leo tarehe 03 Machi 2025.

