Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea
Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kupungua kwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU )nchini Tanzania kutoka asilimia 7 mwaka 2003 /2004 hadi asilimia 4.4 mwaka 2022/2023 na kiwango cha maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kimepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwaka 2022 .
Hayo yameelezwa jana na mgeni rasmi Waziri wa Afya Jenista Mhagama kwenye kongamano la kitaifa la kisayansi lililofanyika kwenye ukumbi wa mkutano wa chandamali manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Alisema kuwa ofisi ya Waziri mkuu itaendelea kuratibu ufanyaji wa tathimini ya mikakati mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu, upunguzaji wa maambukizi, ushawishi na ubadilikaji wa tabia kwani itakuwa fursa kwa serikali ,wananchi pamoja na wadau wote wa mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kufanya tathimini walipotoka, walipo na wanakoelekea.
Alisema kuwa lengo ni kuweka mikakati mipya na endelevu ya mapambano dhidi ya ya vvu na Ukimwi kutokomeza unyanyapaa na vifo vitokanavyo na Ukimwi na kutoa elimu kuhusu masuala yote yanayohusu vvu na Ukimwi ikiwemo athari za kiuchumi na kijamii zinazotokana na janga hill.
” maendeleo chanya katika mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi Shirika la Afya Duniani (WHO) na Taasisi za Taifa zinazoshughulikia masuala ya afya zimeripoti kwamba idadi ya watu wanaoambukizwa VVU imepungua kwa kiwango kikubwa, hususani miongoni mwa makundi ya hatari kama vile wapenzi wengi, wanaotumia madawa ya kulevya kwa sindano, na wanawake wajawazito.”alisema Waziri wa Afya Jenista Mhagama.
Hii ni hatua muhimu kutokana na juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kutoa huduma za elimu, matibabu, na kinga. Matumizi ya dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs) na kuzuia uhamishaji wa VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, pamoja na mikakati ya kuelimisha jamii kuhusu uhalisia wa ugonjwa huu, vimekuwa ni vitu muhimu vilivyosaidia kupunguza maambukizi.
Hata hivyo, changamoto bado zipo, ikiwemo umuhimu wa kuhakikisha huduma za afya zinawafikia watu wote, hasa katika maeneo ya vijijini. Serikali inaendelea kufanya juhudi za kuongeza ufahamu na kupunguza unyanyapaa unaohusiana na VVU ili kuhakikisha kuwa watu wanapata huduma bila hofu.
Kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU ni hatua muhimu lakini inahitaji kuendelezwa kwa umakini ili kudumisha mafanikio haya na kufikia lengo la kuzuia maambukizi mapya kwa asilimia 90 ifikapo mwaka 2030.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi TACAIDS Jerome Kamwela alisema kuwa utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi nchini Tanzania wa mwaka 2022/23 ukisimamiwa na serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania bara na ZAC kwa Zanzibar utafiti ambao umeratibiwa na kutekelezwa kwa pamoja na ofisi ya taifa ya takwimu (NBS) utafiti huo ambao umefadhiliwa na mipango wa dharura wa Rais wa marekani wa Ukimwi (PEPFAR) na kupata msaada wa kiufundi kutoka kitengo cha kuzuia magonjwa cha marekani (CDC) pamoja na shirika la ICAP kutoka chuo kikuu cha Columbia nchini Marekani hufanyika kila baada ya miaka 5 na ni tafiti za kiwango vya haki ya juu katika kupima maendeleo ya Ukimwi katika nchi hakika.