Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kukabiliana na Ugonjwa wa Ukimwi, Winnie Byanyima, amesema kuwa idadi ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi huenda ikaongezeka mara sita zaidi ifikapo mwaka 2029, endapo Marekani haitaendelea na mpango wa kusiadia mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Byanyima ameonya kuwa mamilioni ya watu wanaweza kupoteza maisha, na pia aina mpya sugu ya virusi vya Ukimwi inaweza kuibuka kutokana na kukosekana kwa msaada wa kifedha.

Akizungumza na Shirika la Habari la AP akiwa nchini Uganda, Byanyima alisema kuwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi yamekuwa yakipungua kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni, na mwaka 2023 pekee visa vipya milioni 1.3 vilirekodiwa, punguzo la asilimia 60 tangu mwaka 1995 wakati maambukizi hayo yalipokuwa katika kiwango cha juu.

Hata hivyo, baada ya tangazo la Rais wa Marekani, Donald Trump kwamba nchi yake itasitisha misaada yote ya kigeni ndani ya siku 90, Byanyima alisema maafisa wanakadiria kuwa ifikapo mwaka 2029, maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi yanaweza kufikia milioni 8.7, vifo milioni 6.3 vinavyohusishwa na ugonjwa huo, pamoja na mayatima milioni 3.4.