Kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali maambukizi ya ugonjwa wa malaria nchini Tanzania umeshuka kutoka asilimia 18.1 kwa mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 8.1 kwa mwaka 2022.
Hali hiyo imetokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Mpango wa Kudhibiti Malaria kutoka Wizara ya Afya ikiwemo kuanzishwa kwa utaratibu wa kutoa huduma ya kupima na kutibu malaria katika vijiji ambazo vipo mbali na vituo vya Afya.
Akizungumza leo Aprili 21, 2023 jijini Dar es Salaam katika semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari, Dkt. Abdallah Lusasi Kutoka Mpango wa Kudhibiti Malaria Wizara ya Afya, amesema kuwa kwa ujumla hali ya maambukizi ya malaria imeshuka lakini baadhi ya mikoa bado kuna maambukizi malaria.
“Tumeweza kuwajengea uwezo baadhi ya watu katika vijiji kwa ajili ya kutoa huduma ya kupima malaria pamoja kutoa dawa katika maeneo ya vijiji ambavyo vipi mbali na huduma ya afya” Dkt. Lusasi.
Ameeleza kuwa kwa sasa asilimia 41 ya watanzania wapo katika maambukizi ya chini ya asilimia moja.
Dkt. Lusasi amesema kuwa baadhi ya Mikoa ikiwemo Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Songwe pamoja na Mwanza maambukizi ya ugonjwa wa maralia yapo chini.
“Kupungua kwa maambukizi ya ugonjwa wa malaria kumetokana na kutoa kinga kwa watoto chini ya mwaka mmoja katika maeneo yenye maambuzi ya juu pamoja na kutoa vifaa kinga kwa watoto wa Shule za Msingi, kwani imebainika watoto wengi wanaishi na vimelea vya maambukizi “amesema Dkt. Dkt. Lusasi.
Hata hivyo amebainisha kuwa Mikoa inayoongoza kwa maambukizi ya malaria ni Tabaro ambapo unaongoza kwa asilimia 23.4, Mtwara asilimia 20, Kagera asilimia 18, Shinyanga asilimia 16 pamoja na Mara asilimia 15.