DAR ES SALAAM
NA JUMA SALUM
Awali ya yote naomba nikuhakikishie ndugu
msomaji kuwa hii si hadithi ya kusadikika au
tuseme ni stori ya kutunga, hii ni habari ya
kweli ambayo haikujulikana kwa miaka
mingi na kwa watu wengi.
Kutojulikana kwa jambo kunatokana na
tatizo kubwa linalotokana na kutoandikwa
kwa historia ya Kisiwa cha Mafia
kulinganisha na historia ya visiwa jirani vya
Unguja au Kilwa.
Kisiwa cha Mafia kina historia ndefu na
yenye kuvutia kwa miaka zaidi ya 2,000
iliyopita inayoelezea mafungamano ya
kibiashara kati ya kisiwa hiki na nchi ya
Misri ya kale pamoja na miji mingine ya
Mashariki ya Kati.
Leo sizungumzii Kisiwa cha Chole, au mji
wa Kua uliokuwapo katika Kisiwa cha Juani,
ama hata eneo la Kisimani – Mafia lenye
magofu yaliyoliwa na bahari. Makala hii
inahusu mji ambao wengi hawaujui pengine
kutokana na kuzama baharini.
Februari, 2013 mtalii na mzamiaji (diver),
Alan Sotton wa Uingereza akiwa na
wenzake walitumia helikopta kutoka Dar es
Salaam kwenda Mafia kwa lengo la kutalii
na kutafuta eneo ilipojengwa ngome ya
Wareno kisiwani Mafia wakati wa utawala
wa Wareno kwa pwani ya Afrika ya
Mashariki katika karne ya 15.
Helikopta ikiwa juu katikati ya bahari karibu
na Kisiwa cha Mafia, kina Alan waliona
jambo lisilo la kawaida baharini.
Kwa ushahidi wa picha, Alan anasema
waliona kitu kama eneo pana
lililozungushiwa ukuta mkubwa mithili ya
uzio wa tofali kuzunguka mji. Kwa haraka
ungeweza kudhani labda ni miamba, lakini
si kwa Mafia – kisiwa ambacho kijiografia ni
mchanga.
Eneo hili linapatikana kaskazini – magharibi
mwa Kisiwa cha Mafia, karibu na Kijiji cha
Chunguru, ama tuseme Tumbuju ukiwa
unaitafuta Jojo au Banja. Ni eneo la wavuvi
ambako wenyeji wao hudhani ni mwamba
tu.
Baada ya kujaribu mara kadhaa kwa miaka
mitatu mfululizo kulitafuta eneo hili kwa boti
na kwa msaada wa mwenyeji wa Mafia
aitwaye Athumani Bakari, Machi 21, 2016
Alan akafanikiwa kufika eneo husika akiwa
na mwenziwe aliyeitwa Jane Hannah.
Wakachukua picha na video kwa mara ya
kwanza na kutuma katika mtandao
wa seaunseen.
Kinachoonekana ni kuta za nyumba
zilizobomoka pamoja msingi wake. Ukuta
huo una urefu wa takriban kilometa 3.7
unaoanzia mashariki kwenda magharibi na
upana wa kilometa moja uliokaa
kusini/kaskazini. Tofali zake zikiwa na
ukubwa tofauti, nyingi zikiwa na ukubwa wa
mita tano kwa mita tano na unene wa
sentimita 40.
Tofali hizi zikiwa zimejengwa na malighafi
tofauti, lakini zinazooneka kwa urahisi ni
mawe aina ya sandstone na aina fulani
fulani ya saruji. Kuta zikiwa zimejengwa kwa
mtindo sawa na majengo ya kale
yanayopatikana maeneo mengi ya pwani ya
Tanzania. Ukubwa na mtindo wa ujenzi wa
eneo hili bila ya shaka si tu unatuambia
kuwa ulikuwa mji, bali ni mji wenye
umuhimu wake.
Swali muhimu la kujiuliza ni mji gani huo?
Nani na lini aliujenga? Na kwanini
umezama?
The Periplus Maris Erythraei (Voyage
around the Erythraean Sea): Haya ni
maandishi ama tunaweza kusema ni kitabu
kilichoandikwa na baharia – mfanyabiashara
Mmisri aliyekuwa anazungumza Kigiriki,
asiyefahamika jina katika nusu ya karne ya
kwanza aliyefanya safari kwa majahazi.
Maandishi haya yanajikita zaidi kuelezea
njia mbili za kibiashara kwa njia ya bahari –
ya kwanza ni East – West, yaani kutoka
Misri kwenda Bara Arabu na Asia kwa
ujumla; na ya pili ni North – South, yaani
kutoka Misri kwenda pwani ya Afrika
Mashariki mpaka Tanzania ya sasa.
Mwandishi ameelezea kuhusu urefu wa
safari, njia ilivyo, misimu ya kusafiri, bidhaa
za kwenda kuuza na kununua maeneo
husika, watu na watawala na maeneo ya
kutia nanga.
Sehemu ya kwanza hadi ya 18 ya kitabu
hiki mwandishi anazungumzia njia ya North
– South na mambo yake.
Kulingana na Periplus, kusini mwa pwani ya
Afrika ya Mashariki kulikuwa na soko kubwa
la bidhaa mbalimbali zikiwamo za meno ya
ndovu na magamba ya kobe, eneo hilo
likiitwa Raphta, likiwa karibu na kisiwa
kilichoitwa Menouthesias.
Hadi hapa niandikapo wana historia wengi
wanatofautiana kuhusu eneo hilo ‘Raphta’
lilipokuwa. Wapo wanaosema
Menouthesias itakuwa Zanzibar na Raphta
ipo kati ya Bagamoyo na Dar es Salaam;
wakati wengine wakisema Raphta ipo kati
ya Rufiji na Kilwa na Menouthesias ni
Kisiwa cha Mafia.
Lakini tangu miaka hiyo Raphta imekuwa
kitendawili na ikitafutwa bila mafanikio na
huwafanya baadhi ya watafiti kudhani kuwa
Raphta labda itakuwa imezama katika
ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi katika
maeneo ya Mafia, Kilwa na Rufiji.
Kugundulika kwa magofu haya chini ya
bahari wengi wanadhani kuwa ‘Raphta’
imepatikana.
Je, ni ngome ya Wareno?
Miaka ya 1890 mpelelezi maarufu wa
Kijerumani ambao wengi wetu tulimsoma
kuanzia darasa la tano, Carl Peters, alifika
Mafia kukusanya taarifa za kisiwa hiki na
kati ya kazi alizofanya ni kuchora ramani ya
Mafia.
Miongoni mwa maelezo katika ramani ni
uwepo wa ngome ya Wareno upande wa
magharibi mwa Kisiwa cha Mafia
iliyobomolewa na kumezwa na bahari.
Mbali na hayo ya Carl Peters, Marco
Ramineri, ambaye ni mtafiti na mtaalamu
wa makazi ya kale ya Wareno alipata
baadhi ya nyaraka za Wareno za mwaka
1636 zinazoelezea uwepo wa kituo au
ngome iliyokuwa ikilindwa na askari 12.
Licha ya maelezo yote hapo juu, hadi leo
hakuna anayefahamu ni wapi ngome hiyo
ilikuwapo kisiwani Mafia. Kwa kiasi fulani
wengine hudhani huu mji ni hiyo ngome ya
Wareno.
Umri wa tumbawe waongeza utata
Kwa ‘kimombo’ matumbawe huitwa ‘corals’.
Tumbawe ni nini? Labda naweza kwa
maneno machache kusema ni viumbe hai
vyenye maumbile tofauti tofauti vinavyoishi
baharini na kuwa mazalia ya samaki.
Sasa basi, wakati Alan anafanya uchunguzi
wa kina eneo hilo alikuta tumbawe aina
ya porites corals limejishika katika ukuta
likiwa na urefu wa mita 2.5. Aina hii ya
tumbawe hukua kwa wastani wa milimita
4.5 kwa mwaka.
Ukifanya hesabu utaona tumbawe hilo lina
umri wa takriban miaka 555. Hii ina maana
gani? Maana yake ni kuwa ukuta ule upo
kwenye maji kwa zaidi ya miaka 555. Kwa
maana hiyo majengo yale yalishazama
kabla Wareno kuja katika karne ya 16. Hili
linathibitishwa na ukweli kwamba kwa
miaka 2,000 iliyopita kina cha bahari
kimeongezeka kwa mita nne tu. Kwa hiyo ni
vigumu kuamini kuwa mji huu umejengwa
karne ya 16 au 15 na eti labda umezama
majini kwa sababu bahari imeongezeka
kina. Japo kuna ukweli unaothibitisha kuwa
matetemeko ya ardhi
kama tsunami iliyoikumba dunia miaka
kadhaa iliyopita yamechangia kufanya
majengo haya yajichimbie zaidi, lakini si
kufanya yafike kina cha mita tano wakati wa
maji mafu.
Maoni ya Profesa Felix Chami
Akielezea kitendawili hiki, mtaalamu wa
mambo ya kale kutoka Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, Profesa Felix Chami, anasema
huenda haya majengo yalijengwa na
Wareno ambao nao walijenga juu ya
magofu mengine waliyoyakuta eneo hilo.
Hitimisho
Hadi sasa hakuna aliyeweza kuthibitisha na
kuelezea kwa kina na kitaalamu juu ya
kitendawili hiki cha haya magofu
yaliyoonekana baharini. Kwa hakika
itawachukua muda mrefu wasomi wetu
kufikia hitimisho lisiloacha chembe ya shaka
kuhusu mji uliozama baharini.
Mnakaribishwa kwa maoni na tafakuri.
Mwandishi wa makala hii
amejitambulisha kuwa ni Juma Salum,
ambaye ni msomi wa masuala ya
maliasili aliyehitimu katika Chuo cha
Usimamizi wa Wanyamapori Mweka.
Anapatikana kwa simu: 0657 972723
Mwisho