Naibu Waziri wa Tamisemi Mh. Josephat Sinkamba Kandege ametoa maagizo 14 kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wote Tanzania bara ili kuboresha upatikanaji bora wa huduma za kijamii katika maeneo yao na kuondoa changamoto zilizopo.
Ametoa maagizo hayo katika majumuisho ya ziara yake ya siku 10 katika mkoa wa Rukwa yaliyowakutanisha watumishi wa Halmashauri Nne za Mkoa wa Rukwa yaliyofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Sumbawanga ambapo ni makao makuu ya Mkoa huo.
Maagizo hayo yamekuja baada ya Kutembelea miradi kadhaa katika Wilaya tatu za Mkoa na kubaini mambo ambayo yanakwamisha maendeleo ya wananchi wa mkoa huo na taifa kwa jumla.
Yafuatayo maagizo yake.
1. Watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidi kujituma kwa weledi mkubwa ili kuwa na utumishi wenye matokeo kukosekana kwa huduma hiyo iliyobora kunafifisha jitihada za wananchi katika kutafuta na kujiletea maendeleo hivyo ni vyema watumishi wa umma wakajitathmini wao binafsi kuona endapo wanaridhika na huduma wanayoitoa kwa jamii na kuchukua hatua ya kubadilika.
2. Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe kuwa wanashughulikia haki stahili za watumishi kwa wakati na kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu, ipo tabia ambayo imeanza kujengeka kwa waajiri kutolipa stahili kwa visingizia kwamba madai hayo yamewekwa kwenhye orodha ya madeni, tabia hii haikubaliki katika uongozi wa sasa. Maelekezo ya serikali ni kwamba waajiri wote wahakikishe hawazalishi madeni badala yake watenge fedha za kustosha kulipia gharama hizo. Makatibu tawala wa mikoa wahakikishe wanahakiki madeni yote yanayopokelewa kutoka halmashauri kabla ya kuwasilisha serikali kuu.
3. Wakurugenzi wote wa Halmashauri wahakikishe wanajaza nafasi zilizowazi za wakuu wa idara na vitengo kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo, baadhi ya Halmashauri watumishi wanakaimu nafasi hizo kwa muda mrefu. Hivyo hudumaza utoaji huduma wa idara. Makatibu tawala wa mikoa wasiamamie jambo hili na endapo kutakosekana maafisa wenye sifa wayawasilishe maomb I hayo ya maafisa wenye sifa kwenye OR TAMISEMI.
4.Wakuu wa Mikoa yote Tanzania bara kuhakikisha na kusimamia Halmashauri zote ambazo zina hoja za ukaguzi na maagizo ya kamati za bunge na serikali za mitaa (LAAC) zinajibiwa na kuwasilisha majibu ya hoja hizo na kuyawasilisha Ofisi ya CAG kwa mjuda uliopangwa, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi na Manispaa ya Sumbawanga ni miongoni mwa Halmashauri Mahususi zilizopewa maagizo na Kamati ya LAAC.
5.Mkoa wa Rukwa uhakikishe kwamba kuanzia mwaka wa masomo 2018 unaanzisha na kuendeleza mpango wa wanafunzi kula chakula wakiwa shuleni kutokana na ziada ya uzalishaji wa chakula iliyopatikana
6. Wataalamu wa Sekta ya ardhi wahakikishe wanatatua kero na migogoro ya Ardhi kwa kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi za vijiji na mipango miji, aidha wanatakiwa kuwa mbele ya wakati kwa kutambua na kupanga miji hasa inayoibuka ambayo iko chini ya sheria za ardhi ili kuzuia ujenzi holela na kuwa na miji isiyopangika, samabamba na hili wahakikishe wanashirikiana na idara za ujenzi na afya ili kuhakikisha kuwa nyumba zote zinazojengwa mijini zimepata kibali cha ujenzi, halmashauri zihakikishe zinatenga fedha za kutosha kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kutekeleza jambo hili.
7. Halmashauri zote zihakikishe kwamba majengo yote ya taasisi za umma hasa vituo vya kutolea huduma za afya na shule yanapimwa na kupatiwa hati ili kuepusha migogoro na jamii inayozunguka maeneo hayo.
8. Mameneja wote wa TARURA Tanzania bara wafanye kazi kwa kushirikiana na Halmashauri, mipango ya ujenzi na matengenezo ya barabara itokane na maamuzi na vipaumbele vya Halmashauri isipokuwa Wakala waweke kipaumbele kulingana na bajeti iliyopo. Aidha Dhana ambayo imeanza kujengeka kwa baadhi ya watendaji wa TARURA kuwa wakala ni chombo huru hivyo hakiingiliwi ni dhana potofu.
9. Halmashauri zihakikishe kwamba zinatumia Force Account kwa miradi yote ya ujenzi ambayo utaalamu na ujuzi wake vinapatikana katika mazingira ya miradi husika inapotekeleza ili kuharakisha utekelezaji wa miradi hii ili kuounguza gharama pamoja na kutoa ajira kwa jamii inayozunguka miradi hiyo.
10. Kutokana na upungufu mkubwa wa watumishi ulioripotiwa na Halmashauri katika vituo vya kutolea huduma, Shule, huduma za afya na ofisi za watendaji wa kata na vijiji kutokana na sababu mbalimbali kama zoezi la uhakiki na baadhi kuhamia TARURA, Mikoa ifanye tathmini ya awali ya mgawanyo wa watumishi ndani ya mikoa na halmashauri kubaini maeneo yenye ziada na upungufu kufanya mgawango sawia wa watumishi kabla ya kuwasilisha maombi hayo kwa OR – TAMISEMI, maombi hayo yaambatane na maombi ya watumishi wa kada hiyo ndani ya Mkoa.
11. Kutokana na muitikio wa uchangiaji mdgogo wa wananchi katika mfuko wa afya ya jamii (CHF) Halmashauri zinaelekezwa kuendelea kuhamasisha jamii umuhimu wa kuchangia mfuko. Mganga Mkuu wa Mkoa na Halmashauri wanaagizwa kuwa hadi kufikia Mwisho wa Mwaka wa Fedha 2017/2018 uchangiaji wa CHF uwe umefikia Walau asilimia 50
12. Wakurugenzi wote Tanzania Bara wahakikishe wanatambua na kujaza nafasi zote zilizowazi za uongozi katika serikali za vijiji na mitaa hadi kufikia Juni 2018. Aidha Mikoa iandae na kuwasilisha OR TAMISEMI Orodha ya nafasi wazi za viongozi katika ngazi hizi.
13. Wakurugenzi wa Halmashauri Tanzania Bara kupitia wakaguzi wa ndani wa halmashauri wahakikishe kuwa wanafanya ukaguzi wa hesabu za kata, vijiji, vituo vya kutolea huduma ikiwemo vituo vya afya, zahanati na shule katika kila robo na kujadili katika vikao halali vya halmashauri kwakuwa takwa hili ni la kisheria chini ya sheria ya fedha ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa Sura 290 kuliko suala hili sasa hivi limeachwa kwenye mikutano mikuu ya vijiji ambavyo haifanyiki ipasavyo. Kamati za vituo vya kutolea huduma haziwasilishi taarifa hizo kwenye kata na vijiji.
14. Mkoa wa Rukwa uhakikishe kuwa tunaendelea kutunza, kuhifadhi na kuendeleza ng’ombe wenye asili ya kifipa, ng’ombe hawa wana uwezo wa kustahimili magonjwa na uwezo mkubwa wa kushiriki kwenye nguvu kazi kwa maana ya shughuli za kilimo. Mikoa mingine lazima kufunga zaidi ya jozi “pear” moja lakini kwa huku jozi moja inatosha hivyo ni vizuri tukahakikisha kwamba ng’ombe hawa wenye asili ya kifipa tunwalinda kuwahifadhi na kuwaendeleza.