Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka huu yatafanyika Kimikoa ambapo kilele chake kitakuwa Aprili 26, 2025.
Amesema tangu kuasisiwa kwa Muungano kumekuwa na mafanikio makubwa katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii na umeendelea kuwa moja kati ya vielelezo vikuu vya Umoja, Udugu na Utaifa wetu kama Watanzania na kumeweza kunufaika na kukuza uhusiano baina ya nchi yetu na Jumuiya ya Kimataifa kwa manufaa ya pande zote za Muungano.

Ameyasema hayo wakati wa kongamano kuelekea Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililofanyika Aprili 22, 2025 jijini Dar es Salaam ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania: Muungano wetu ni dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa: Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025’’.
“Muungano huu ni wa watu, hivyo ni Muungano unaoishi ili kutimiza matakwa na malengo ya wananchi wake. Ni kwa sababu hiyo basi, licha ya mafanikio mengi yaliyopatikana, zimekuwepo pia changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa nyakati tofauti na kupatiwa ufumbuzi kwa lengo la kuuimarisha Muungano wetu.”
“Sehemu kubwa ya Watanzania ambao ni vijana kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, hawana uelewa wa kutosha kuhusu Muungano ikiwemo Viongozi. Ni kwa kutambua changamoto hiyo, ndiyo maana jitihada zinafanyika ili kukuza uelewa na ufahamu wa historia na matukio muhimu ya Taifa letu.” Amesema Waziri Masauni.
Aprili 26, 1964, Jamhuri ya Tanganyika chini ya uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar chini ya uongozi wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, ziliafikiana kwa mkataba kuunganisha nchi hizi mbili huru kuwa nchi moja inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa namna na umuhimu wa kipekee, natoa pongezi kwa Viongozi wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kuweka suala la kuimarisha Muungano kuwa ni moja ya vipaumbele na kuendelea kudumisha Muungano wetu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Mitawi amesema Aprili 22, 1964 ndio siku ambayo hati ya Muungano ilisainiwa katika Ikulu ya Zanzibar na aliyekuwa Rais wa Tanganyika Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amman Karume.
Ameongeza kuwa mazungumzo ya kufanikisha hayo yote yalikuwa ya siri kubwa kutokana na umuhimu wa tukio hilo na kwa kipindi hicho Zanzibar ilikuwa na watu wanaokadiliwa kuwa 300,000 na Tanganyika kuwa na watu milioni 12.
Aprili 25, 1964 ndio siku ambayo hati ililidhiwa ambapo kwa Zanzibar ililidhiwa na Baraza la Mapinduzi na Bara ililidhiwa na Bunge la Tanganyika na kusainiwa na Mwl Nyerere Aprili 26, 1964 ndio maana hadi leo Aprili 26 taifa huadhimisha miaka kadhaa ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Aprili 27, 1964 likawa Bunge la mwanzo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

