NA CHRISTOPHER MSEKENA
Hivi karibuni wasichana wamekuwa mstari wa mbele katika kuchagiza mafanikio ya Bongo Fleva, hasa katika upande wa kuchezesha muziki kama ma-dj katika vituo vya utangazaji (redio na runinga), matamasha, klabu na kadhalika.
Warembo kama DJ Fetty, DJ Sinyorita, DJ Mamie, DJ Sweetlady na wengineo wameing’arisha tasnia ya u-dj kwa upande wa wasichana kiasi cha kuvunja ukuta wa dhana kwamba kazi hiyo ni kwa wanaume pekee.
DJ Sinyorita amefanya kazi kubwa katika redio, matamasha na klabu mbalimbali hapa nchini, ndiye DJ wa kike mwenye wafuasi wengi Instagram akiwa ametimiza milioni mbili.
Pia kuna DJ Mamie anayefanya vizuri Wasafi Media akitokea Redio ya EFM, amekuwa miongoni mwa ma-dj wenye ushawishi mkubwa kwa sasa hapa Bongo kwa kazi anayofanya.
Hali kadhalika DJ Sweetlady, alijizolea umaarufu zaidi kipindi kile cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 baada ya kuonekana katika mikusanyiko ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) akicheza nyimbo mbalimbali za chama hicho.
Leo tunakupa warembo kadhaa wanaofanya vizuri barani Afrika na wamekuwa wakicheza muziki na kukonga nyoyo za mashabiki sehemu mbalimbali duniani.
DJ Zinhle Jiyane
Jina lake halisi ni Ntombezinhle Jiyane, ila mashabiki wanamuita DJ Zinhle. Huyu ni mrembo kutoka Afrika Kusini anayefanya kazi ya muziki kwenye redio, runinga, matamasha na klabu mbalimbali za ndani na nje ya Afrika.
Zinhle mwenye jumla ya wafuasi milioni 3.5 katika mtandao wa Instagram ni mama wa mtoto mmoja na miaka kadhaa iliyopita aliwahi kuwa kwenye uhusiano wa mapenzi na Rapa AKA.
DJ Cuppy
DJ Cuppy ni mzaliwa wa Lagos, Nigeria na amewahi kufanya kazi Roc Nation ya Jay Z. Mbali na ku-dj muziki, Cuppy amekuwa akifanya ngoma kwa kushirikisha wasanii mbalimbali ndani na nje ya Afrika, mfano hivi karibuni aliachia wimbo ‘Jolloff On the Jet’ aliomshirikisha Rayvanny na Rema.
Cuppy ambaye ana shahada ya biashara ya muziki kutoka Chuo Kikuu cha New York City, Marekani amekuwa akitumbuiza Nigeria na London, Uingereza huku akijizolea wafuasi milioni 5.7 katika ukurasa wake wa Instagram.
DJ Pierra Makena
Kutoka Nairobi, Kenya. Mrembo Pierra Makena amejizolea heshima kubwa katika ulimwengu wa burudani kwa ku-dj muziki na kuzalisha kazi zake binafsi zinazofanya vema sokoni.
Pierra ambaye ni mama wa mtoto mmoja, mwigizaji na mtangazaji, anatajwa kama DJ ghali anayelipwa zaidi nchini Kenya akiwa amepiga shoo kadhaa katika nchi za Burundi, Ghana, Nigeria, Marekani na kwingineko.
DJ Nyce
Kutoka nchini Ghana. Miongoni mwa ma-dj wenye mafanikio katika sanaa hiyo ni DJ Nyce. Mrembo huyo hucheza muziki katika redio na kila wikiendi huwa anaburudisha kwenye Klabu ya The Honeysuckle.
DJ Nyce amejiongeza, kwa sababu mbali na kucheza muziki ni prodyuza anayeunda midundo ya nyimbo mbalimbali.
DJ Roxxi
Jina lake halisi ni Deshnie Govender. Ni miongoni mwa warembo wachache wenye asili ya Kihindi waliozaliwa Afrika Kusini. DJ Roxxi ambaye pia ni rapa, mwigizaji na mtangazaji amewahi kuchaguliwa kama DJ pekee na Kampuni ya AXE Jet Experience kwenda kula bata katika fukwe za Ibiza, Hispania na kuchezesha muziki mwaka 2017.
DJ Owami
Kutoka Afrika Kusini. Mrembo Owami Mafoate ambaye ni mtoto wa mwanamuziki nyota wa Kwaito, Arthur Mafokate, ameanza kujipatia mafanikio akiwa na miaka 16 kwa kuonekana katika runinga ya taifa akionyesha kipaji chake na hadi sasa ni miongoni mwa ma-dj warembo wanaokimbiza ndani na nje ya Afrika Kusini.