Kipindi hiki ni cha kampeni. Nafuatilia aina ya ujumbe unaotumwa kwenye simu za mikononi, mijadala inayoendelea, sera zinazotamkwa na wagombea kutoka kwenye ilani zao kauli mbiu (slogan) za wagombea katika kampeni, mijadala inayoendelea kwenye vijiwe na mengine mengi.
Kama mwandishi wa siku nyigi kiasi, nieleze yaliyonishangaza. Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli hadi sasa likuwa akifanya vyema kwenye kampeni zake, na yapo makosa machache anayoyafanya ya kutamka majina ya viongozi wa nchi kama Iraq akawataja kuwa ni wa Libya, ingawa alisahihisha, hili halikunipa shida.
Dk. Magufuli amenipa shida kidogo alipoanza kuingia katika kubadili hata alama za msingi za CCM. Katika kampeni nimezoea kuona mgombea wa CCM kupitia sera yao ya Chama Kwanza, Mtu Baadaye, kuwa mabango ya wagombea katika uchaguzi wa mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010 yaliandikwa ama Chagua CCM au Chagua Mkapa.
Sitanii, zamu hii ni tofauti kidogo. Mabago yote ya Uchaguzi yameandikwa Chagua Magufuli. Nembo ya CCM imetumbukizwa katika bango hilo kwa maandishi madogo sawa na maandishi ya “Onyo, uvutaji wa sigara ni hatari.” Mara nyingi kama hujaangalia vizuri, unaweza hata usiyaone hayo maneno kwani ni madogo kiasi cha kutisha. Sijui kwa nini hawayafanyi makubwa kama Sportsman!
Hiyo kama haitoshi, pamoja na sera nzuri za ujenzi wa barabara, meli kwa wakazi wa mikoa mbalimbali inayotegemea maziwa na bahari kusafiri, shule bure mpaka kidato cha nne, upatikanaji wa maji na mengine mengi mazuri, kwa mwaka huu simsikii au siwasikii wapenzi wa CCM wakisalimiana kwa salaam yao ya siku zote ya “Kidumu Chama Cha Mapinduziiiiiii” kisha wakaitikia, “Kidumu chama tawala, kitaendelea kudumu na watu kibao…. CCM ina wenyewe babu weeeeee”.
Nikimsikiliza Dk. Magufuli, na wapambe wake wenye kumsaidia kunadi sera, mara zote wanasema kwa ufupi sana, “CCM Oyeee”, kisha anaingiza kibwagizo kipya. “Hapa kazi tu.” Ndiyo, hii hainipi shida mno. Hainipi shida maana inawezekana Magufuli amebaini kibwagizo kizuri cha kuvutia wananchini hiki cha “Hapa kazi tu.”
Nilianza kupata shida kidogo, pale Magufuli aliposimama kule Tunduma akatumia kaulimbiu ya chama cha upinzani cha Chadema ya “Peopleeeeees” kisha akasema hiyo power wampatie yeye.
Eneo la Mwanjelwa akiwa kwenye gari, baada ya vijana kuusonga msafara wake wakinyoosha vidole viwili, naye akaamua kunyoosha vidole viwili ishara inayotumiwa na Chadema kwenye kampeni zake.
Sitanii, nilipoangalia huo mkanda nikasema Magufuli mjanja. Ameamua kuvutia wapigakura kwa kunyoosha hadi vidole viwili, baadaye nikasikia ameanza kuzungumza mabadiliko. Hii sera ya mabadiliko imeasisiwa na wapinzani, na hata wamekwenda mbali baada ya tangazo la Mbowe ukisema mabadiliko, wanaitikia Lowassaaaa, Lowassa – Mabadilikoooo.
Kama hiyo haitoshi, nimepata mshituko wa mwaka nilipoona vimechapishwa vipeperushi vya M4C, wakisema ni Magufuli For Change. Katika soka tunaruhusiwa kubadili mfumo unapoona timu pinzani inacheza 4 4 2 au 1 3 5, lakini si kwenye siasa.
Katika ulingo wa siasa ukiwa kwenye jukwaa la CCM ukasema Peopleeees, basi ujua fika kuwa ama huamini katika kaulimbiu ya chama chako au unatamani kuwa kwenye jukwaa la wanaotumia hiyo kauli. Ingekuwa mtumbwi umeanguka baharini, ungesema ni dalili za mfa maji.
Napata shaka, kuwa kwa Magufuli kuendekeza utamaduni wa kuiga kila kitu kinachofanywa na wapinzani, hadi uchaguzi unakwisha, unaweza kukuta CCM imevunja misingi yake yote. Hata T-shirt za CCM kwa sasa zimebadilishwa na kuwa na michirizi kama za Chadema.
Kuinga kila jambo la Chadema, itawafanya wapigakura kuiga hata jinsi Chadema wanavyopiga kura na hatimaye CCM itapoteza kila kitu na huo ndio mwelekeo. Ikiwa bado wanaipenda CCM basi wawe wabunifu, waache kuiga kila jambo. Hii ni hatari kwa ustawi wa CCM.
Sitanii, wakati nikizungumza hayo nimekuta katika vijiwe kadhaa wakizungumza Mussa alivyokulia utumwani Misri, baadaye akawaongoza wana wa Israel kupita katika Bahari ya Shamu na kurejea kwao kwenye nchi ya ahadi. Baadhi ya watu wanamlinganisha Lowassa na Mussa. Kwamba amekuwa CCM ndani ya miaka 38, na sasa ameamua kuwaongoza Watanzania kwenda kwenye nchi ya ahadi.
Kuhusu dhambi anazotajwa nazo Edward Lowassa nimekuta mjadala mzito. Watu hawa wanatumia mfano wa Sauli katika Kitabu cha Matendo ya Mtume. Sauli alikuwa mtesi wa Waisraeli. Hata hivyo, siku moja akiwa jangwani alisikia sauti ya Yesu ikimkemea, alipojibizana naye, Sauli akaongoka. Mimi sisemi hilo ndilo lililotokea kwa Lowassa, ila nimeona nichukue Sura ya 26 Kitabu cha Matendo ya Mitume kwenye Biblia mstari 1-31, usome ujumbe wake msomaji wangu, kisha ufanye uchambuzi binafsi.
Paulo anajitetea mbele ya Agripa
1 Basi, Agripa akamwambia Paulo, “Unaruhusiwa kujitetea.” Hapo Paulo alinyosha mkono wake akajitetea hivi: 2 “Mfalme Agripa, ninajiona mwenye bahati leo kujitetea mbele yako kuhusu yale mashtaka yote ambayo Wayahudi walikuwa wamesema juu yangu. 3 Hasa kwa vile wewe mwenyewe ni mtaalamu wa desturi za Wayahudi na migogoro yao, ninakuomba basi unisikilize kwa uvumilivu.
4“Wayahudi wanajua habari za maisha yangu tangu utoto, jinsi nilivyoishi tangu mwanzo kati ya taifa langu huko Yerusalemu. 5 Wananifahamu kwa muda mrefu, na wanaweza kushuhudia, kama wakipenda, kwamba tangu mwanzo niliishi kama mmoja wa kikundi chenye siasa kali kabisa katika dini yetu, yaani kikundi cha Mafarisayo.
6 Na sasa niko hapa nihukumiwe kwa sababu ninaitumainia ile ahadi ambayo Mungu aliwaahidi babu zetu. 7Ahadi hiyo ndiyo ileile inayotumainiwa na makabila kumi na mawili ya taifa letu, wakimtumikia Mungu kwa dhati mchana na usiku. Mheshimiwa mfalme, Wayahudi wananishtaki kwa sababu ya tumaini hilo!
8Kwa nini nyinyi mnaona shida sana kuamini kwamba Mungu huwafufua wafu? 9Kwa kweli mimi mwenyewe niliamini kwamba ni wajibu wangu kufanya mambo mengi kulipinga jina la Yesu wa Nazareti. 10Mambo hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Mimi binafsi, nikiwa nimepewa mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu, nilipata kuwatia gerezani wengi wa watu wa Mungu.
Nao walipohukumiwa kuuawa, nilipiga kura ya kukubali. 11Mara nyingi niliwafanya waadhibiwe katika masunagogi yote nikiwashurutisha waikane imani yao. Hasira yangu kwao ilikuwa kubwa hata nikawasaka mpaka miji ya mbali.
Paulo anaeleza alivyoongoka
(Mate 9:1-19; 22:6-16)
12“Kwa mujibu huo huo, nilikwenda Damasko wakati mmoja, nikiwa na mamlaka na maagizo kutoka kwa makuhani wakuu. 13Mheshimiwa, wakati nilipokuwa njiani, saa sita mchana, niliona mwanga mkubwa kuliko wa jua ukiangaza kutoka mbinguni, ukanizunguka mimi na wale wasafiri wenzangu. 14Sisi sote tulianguka chini, nami nikasikia sauti ikiniambia kwa Kiebrania: ‘Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa? Unajiumiza bure kama ng’ombe anayepiga teke fimbo ya bwana wake.’
15Mimi nikauliza: ‘Ni nani wewe Bwana?’ Naye Bwana akajibu: ‘Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa. 16Haidhuru, inuka sasa; simama wima. Nimekutokea ili nikuweke rasmi kuwa mtumishi wangu. Utawathibitishia watu wengine mambo uliyoyaona leo na yale ambayo bado nitakuonesha.
17Nitakuokoa na watu wa Israeli na watu wa mataifa mengine ambao mimi ninakutuma kwao. 18Utayafumbua macho yao na kuwawezesha watoke gizani na kuingia katika mwanga; watoke katika utawala wa Shetani, wamgeukie Mungu; ili kwa kuamini, wapate kusamehewa dhambi na kuchukua nafasi yao kati ya wale ambao wamepata kuwa watu wa Mungu.’
Paulo anaongea juu ya utumishi wake
19“Hivyo, mfalme Agripa, sikuweza kuwa mkaidi kwa maono hayo ya mbinguni. 20Ila nilianza kuhubiri kwanza kwa watu wa Damasko, halafu kwa wale wa Yerusalemu na nchi yote ya Yudea, na pia kwa watu wa mataifa mengine. Niliwahimiza wamgeukie Mungu na kuonesha kwa vitendo kwamba wamebadilisha mioyo yao.
21Kwa sababu hiyo, Wayahudi walinikamata nikiwa hekaluni, wakajaribu kuniua. 22Lakini Mungu alinisaidia; na hivyo mpaka siku ya leo nimesimama imara nikitoa ushuhuda kwa wote, wakubwa na wadogo. Ninayosema ni yale ambayo manabii na Mose walisema yatatukia; 23yaani ilimpasa Kristo ateseke na kuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu, ili atangaze kwamba mwanga wa ukombozi unawaangazia sasa watu wote, Wayahudi na pia watu wa mataifa mengine.”
24Paulo alipofika hapa katika kujitetea kwake, Festo alisema kwa sauti kubwa, “Paulo! Una wazimu! Kusoma kwako kwingi kunakutia wazimu!” 25Lakini Paulo akasema, “Sina wazimu mheshimiwa Festo. Ninachosema ni ukweli mtupu. 26Wewe Mfalme unayafahamu mambo haya, kwa hiyo ninaweza kuongea bila woga mbele yako.
Sina mashaka kwamba matukio hayo yanajulikana kwako maana jambo hili halikutendeka mafichoni. 27Mfalme Agripa, je, una imani na manabii? Najua kwamba unaamini.” 28Agripa akamjibu Paulo, “Kidogo tu utanifanya Mkristo!” 29Paulo akamjibu, “Namwomba Mungu kwamba, kwa muda mfupi au mrefu, si wewe tu bali wote wanaonisikia leo wapate kuwa kama nilivyo mimi, lakini bila hii minyororo.”
30Hapo mfalme Agripa, mkuu wa mkoa, Bernike na wale wote waliokuwa pamoja nao, walisimama. 31 Walipokwisha ondoka, waliambiana, “Mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo au kifungo.”
Sitanii, najaribu kuwaza kwa sauti tu kuwa hivi binadamu huwa habadiliki? Hivi ni sahihi kumhukumu mtu kwa historia isiyoweza kuthibitishwa? La msingi, Tanzania inahitaji amani. Amani itaendelea kuwapo iwapo mshindi anapatikana kwa njia ya kura na si goli la mkono. Tujiandae bila jaziba tukapige kura Oktoba 25, na atakayeshinda akabidhiwa nchi. Mungu ibariki Tanzania.