*Kichapo cha JWTZ chawachanganya

*Wengine 1,000 wanaswa, waomba suluhu

*Kamati za Anna Abdallah, Lowassa zakutana

Sasa ni wazi kwamba waasi wa kundi la March 23 (M23), wamelewa kiasi cha kuomba mapambano yasimamishwe ili mazungumzo ya kuleta amani yaweze kutekelezwa. M23 wamelazimika kurudi nyuma baada ya kupigwa na Majeshi ya Umoja wa Mataifa (FIB) yanayoongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Kuna taarifa kuwa kwenye mapambano hayo, FIB waliwanasa waasi zaidi ya 1,000 na kuwanyang’anya silaha mbalimbali.

Habari kutoka kwenye uwanja wa mapambano zinasema M23 wamepoteza mwelekeo na kukimbia kutoka kwenye ngome zao ambazo wamezishikilia kwa muda mrefu. “Hivi sasa tuko katika kambi yao na tunawashikilia waasi zaidi ya 1,000 wengine wamekimbia, wametawanyika wengine wako msituni hawajui nini cha kufanya,” kimesema chanzo chetu kutoka Goma.

Mapigano makali yalitokea Agosti 21 hadi Agosti 24 katika vijiji vya Mutaho na Kibati umbali wa kilometa zaidi ya 20 kutoka Goma. Mapigano hayo makali yaliibuka baada ya kuuawa kwa Meja Khatibu Shaaban Mshindo wa JWTZ na kujeruhiwa kwa wanajeshi wengine wengine.

Ofisa huyo amesema kwamba tukio hilo liliwakasirisha mno wanajeshi wa JWTZ. “Kuuawa kwa Meja Mshindo kulifanya kila askari wa Tanzania na wenzetu kutoka nchi mbalimbali zinazoshiriki katika Majeshi ya MUNUSCO wawe na hasira,” amesema.

 

“Kifo cha Meja Mshindo kilitupa hasira na nguvu za ajabu, hawana hamu tena, nahisi huko waliko wanajuta. Hapa Goma pia katika ngome yao kuu mambo ni kimya kabisa, hakuna kelele za bunduki wala nini, wananchi wanafurahi,” amesema.

Meja Mshindo aliyefariki dunia Agosti 28, mwaka huu, baada ya kujeruhiwa kwa bomu, alizikwa kwa heshima zote nyumbani kwao katika Kijiji cha Mangapwani, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa Kaskazini Unguja. Alizaliwa Septemba 29, 1972 na kujiunga na JWTZ Machi 1995 na kutunukiwa heshima ya kamisheni Mei 17, 1997.

 

Kinachoendelea Goma

Habari kutoka Goma zinasema majeshi ya FIB kwa sasa yanasubiri hatima ya mazungumzo yaliyotarajiwa kuanza mjini Kampala, jana. “Kwa hali ilivyo sijui kama watafikia makubaliano, waasi wana msimamo wao, na Serikali ya DRC ina msimamo wake, sijui kama wataafikiana. “Mama Mary Robinson (Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa), ametangaza msimamo mkali. Kasema hata kama kutafikiwa makubaliano ya kumaliza mapigano, wahusika wa M23 na vikundi vingine waliofanya maovu ni lazima wafikishwe kwenye vyombo vya kisheria vya kimataifa. Kasema wazi hakuna kusameheana. Baada ya makubaliano wahusika watakamatwa.

 

“Msimamo huo umewafanya wengi waone kuwa suala la kufikia makubaliano ya kumaliza mapigano litakuwa gumu, lakini ukweli ndiyo huo,” kimesema chanzo chetu kutoka Goma.

Chanzo hicho kimethibitisha kuwa M23 kwa sasa wamekimbia. Anasema walikabiliwa na wakati mgumu baada ya kumuua Meja Mshindo.

 

“Tuliingizwa kwa nguvu na M23 wenyewe, sisi hapa hatupo kivita, tupo kuwanyang’anya silaha, lakini inapotokea tumeshambuliwa ni lazima tujihami,” amesema na kuongeza:

“Baada ya jamaa kuona hali imekuwa mbaya (kipigo kimewalemea) wakaamua ku-withdraw (kurudi nyuma), walishtuka kuwa wakifanya masihara tutawamaliza. Tulifika mahali tukasema enough is enough (imetosha),” amesema.

 

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge

Hadi tunakwenda mitamboni, kamati mbili za kudumu za Bunge za Ulinzi na Usalama, na Mambo ya Nje zilikuwa zimetakiwa zikutane jijini Dar es Salaam jana. Kamati hizo zilitakiwa zikutane Jumatatu saa 3 asubuhi katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini humo. Mkutano huo ulitarajiwa kuwa wa siku tatu. Haikuwekwa wazi dondoo za mkutano huo, lakini wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa wamedokeza kuwa huenda suala la majeshi ya Tanzania nchini DRC na kulegalega kwa utangamano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni mambo yaliyopewa kipaumbele.

 

“Wajumbe wote wa kamati hizi mbili tumetakiwa tuwe Dar es Salaam kuanzia Jumatatu bila kukosa. Tumesisitiziwa sana, inaelekea kuna mambo mazito,” amesema mmoja wa wajumbe wa kamati hizo.

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama inaongozwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah; ilhali ile ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inaongozwa na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.