Kundi la waasi wa M23 limeendelea kushikilia mji muhimu wa Walikale, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, licha ya awali kutangaza mpango wa kuondoka ili kutoa nafasi kwa mazungumzo ya amani.

Kundi linaloungwa mkono na Rwanda la M23 lilitangaza Jumamosi kuwa limeanza kuondoa vikosi vyake nje kidogo ya mji wa Walikale ili kuweka mazingira mazuri ya “amani na mazungumzo ya kisiasa.” Hata hivyo, kundi hilo lilisema halitaruhusu jeshi la serikali kurejea katika mji huo wenye wakazi takriban elfu 60, likionya kuwa shambulizi au uchokozi wowote utafuta moja kwa moja uamuzi wao.

Wanajeshi wa serikali ya Kongo walisema Jumamosi jioni kuwa watafuatilia kwa umakini uondoaji huo wa M23 na hawatachukua hatua yoyote ya kijeshi, wakiwataka wanamgambo wanaoiunga mkono serikali wafanye hivyo pia ili kupunguza mvutano.

Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Therese Kayikwamba, alisema wanatazama kuona ikiwa kweli M23 itaondoka na kuipa kipaumbele njia ya mazungumzo.