Waasi wa M23 wameripotiwa kuendelea kusonga mbele kuelekea mji wa Bukavu, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku Rwanda ikionya kwamba kundi hilo linaweza kuchukua udhibiti wa maeneo mengine zaidi.
Balozi wa Rwanda katika eneo la Maziwa Makuu, Vincent Karega, amesema M23 itaendelea kuteka maeneo mengine nchini Congo, na Goma haitakuwa lengo lao pekee.
Hata hivyo, aliashiria kuwa mazungumzo kati ya waasi hao na serikali ya Congo yanaweza kuwa suluhu, ingawa alisema kuwa hana imani na utekelezaji wa jambo hilo.
Serikali ya Congo imekataa kufanya mazungumzo na waasi wa M23, ambao inawaona kama magaidi wanaoungwa mkono na Rwanda.
Vyanzo vimebaini kuwa waasi hao sasa wanakaribia mji wa Bukavu, huku Goma ikiwa chini ya udhibiti wa M23. Hali ya usalama bado ni mbaya, huku mamia ya wanajeshi wa Congo na mamluki kutoka Romania wakijiunga na jeshi la Rwanda.
Papa Francis ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano, akitaka raia wa Goma na maeneo mengine waliyoathiriwa kulindwa.
Aidha, Rais wa DRC, FĂ©lix Tshisekedi, anatarajiwa kutoa hotuba kuhusu mgogoro huu leo, lakini amesema hatahudhuria mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika jioni.