–Alishirikiana na Samora Machel kuikomboa Msumbiji
Na Albano Midelo, JamhuriMedia, Songea
Tanzania haitamsahau Dikteta Idd Amini Dada aliyeitawala Uganda kwa mabavu kisha kuvamia Tanzania mwaka 1978 ambapo Tanzania iliingia vitani na kufanikiwa kumng’oa mvamizi huyo mwaka 1979.
Luteni Kanali Mstaafu Daniel Gangisa pichani kulia akiwa na rafiki yake Dikteta Idd Amini Dada amefariki Dunia Mei 6,2024 nyumbani kwake Chandarua Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,ratiba ya maziko itatolewa na ndugu wa marehemu .
Akihojiwa na mwandishi wa Makala haya wakati wa uhai wake Luteni kanali Mstaafu Gangisa anasema anamfahamu vizuri Dikteta Idd Ami kwa sababu walisoma na kufanyakazi pamoja kwa miaka mitatu Nakuru nchini Kenya.
Gangisa alizawaliwa mwaka 1927 katika eneo la Ruhuwiko mjini Songea ambapo alijiunga na jeshi la wakoloni mwaka 1947 ambapo mwaka 1953 alikwenda chuo cha Jeshi Nakuru Nchini Kenya ili kupata mafunzo Zaidi ya kijeshi ambako alikutana na Dikteta Idi Amini.
“Nimesoma na Idd Amini miaka mitatu kuanzia 1953 hadi 1955 alikuwa rafiki yangu sana,tulikuwa tunalala chumba kimoja bwenini, baada ya kumaliza kozi mimi na Amini tulipata alama za juu hivyo chuo kilitupa mkataba wa kuwa walimu tulifanya kazi sote tukiwa na cheo cha Sajenti kwa miaka mitatu’’,anasema Luteni Kanali Mstaafu Gangisa.
Hata hivyo Gangisa anasema licha ya Amini katika kipindi hicho kuonekana kuwa ni kijana mtulivu na ambaye hakuwa mgomvi sana isipokuwa alikuwa mpiganaji wa ngumi na kwamba Amin alimwomba Gangisa amfundishe ngumi,lakini alikataa.
Gangisa anasema kwa muda alioishi na Idd Amin aligundua dosari kubwa aliyokuwa nayo tangu kipindi hicho Dikteta Idd Amin alipenda sana vyeo hata aliposikia amepindua nchi hakushangaa kwa sababu alimfahamu.
Luteni Kanali Mstaafu Gangisa anasema baada ya kumaliza mkataba wa kufundisha Nakuru alirudi Nyeri nchini Kenya kambi yake ya Jeshi kuendelea na Vita ya Maumau kisha alikwenda kwenye vita nchini Mauritius na Idd Amin alirudi kwao Uganda ambapo mara ya mwisho kuonana na Idd Amin anasema ilikuwa mwaka 1960 nchini Kenya.
Anasema mwaka 1964 alishiriki katika kuunda JWTZ Jeshi jipya lenye heshima nchini Tanzania na kwamba yeye ni miongoni mwa maafisa waliunda JWTZ ambapo yeye ni Ofisa wa 50 wakati huo akiwa na cheo cha Luteni Kanali.
Kwa mujibu wa Luteni Kanali Mstaafu huyo,Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere wakati anaanza harakati za uhuru na kuunda chama cha TANU yeye alikuwa na Idd Amini Nakuru Kenya.
“Idd Amini ndiye aliyenipa taarifa kwamba wewe Mswahili nyumbani kwako kuna bwana ameanzisha Chama cha kupigania uhuru,alinitisha kwamba MAUMAU itaamia kwetu,nikamwambia Mungu yupo,alikuwa anaongea Kiswahili kizuri,alikuwa rafiki yangu mkubwa sana’’,alisisitiza Gangisa.
Gangisa aliacha kazi ya JWTZ mwaka 1978,lakini baada ya kusikia Idd Amini amepindua nchi ya Uganda na kuvamia sehemu ya Kaskazini ya Tanzania aliamua kurudi jeshini kupambana na rafiki yake Idd Amin.
“Nilisema kama amevamia nchi yetu narudi jeshini,tulipambana naye,nilifika hadi kijijini kwake,Kampala pale alinusurika kuuawa, akatorokea njia ya Kenya,tuliwaomba Kenya wafunge mpaka walikataa hivyo Idd Amin akanusurika akatoroka ukawa ndiyo mwisho wa Vita ya Uganda’’alisema.
Luteni Kanali Mstaafu Gangisa pia anasema alishirikiana na Samora Machel wa Msumbiji wakati wa harakati za kupigania Uhuru wa Msumbiji ambapo mara kadhaa amelala kwenye mashimo na Samora Machel.
Anasema Samora Machel mara baada ya Uhuru alifika Songea mwaka 1975 wakati anazungumza na wananchi alimshukuru Luteni Kanali Gangisa akisema alishiriki naye kwa kutoa silaha na walilala wote kwenye mashimo na kula mihogo ya watu wakati wa mapambano ya wareno.
Gangisa anatoa rai kwa serikali kuwakumbuka wastaafu waliolitumikia Taifa kwa uzalendo mkubwa ili kumalizia kwa furaha maisha yaliobaki hapa duniani.