Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amevunja historia katika kutatua migogoro ya ardhi nchini na zamu hii ametumia zaidi ya saa 20 kusikiliza kero za wananchi akiwa ofisini Dar es Salaam.
JAMHURI limemshuhudia Lukuvi siku ya Ijumaa kuamkia Jumamosi iliyopita akitoka ofisini saa 08:30 baada ya kusikiliza kero za ardhi kutoka kwa wananchi 189 wa Kanda Mashariki inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Wananchi wengi wametoka Bagamoyo, Kibaha, Mkuranga, Kibiti na Rufiji, ambao ama walikuwa wameporwa ardhi au maeneo ya urithi kuchukuliwa bila kupata fidia stahiki.
Kati ya wananchi aliowasikiliza ni pamoja na aliyepata Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Matheo Qaresi ambaye eneo lake lilivamiwa pia.
“Kwa kweli nchi hii watu wanateseka. Kuna mtu unamwagalia unaona ana shida ya kweli. Unaona kabisa kaonewa na jitu lililojigeuza Mungu mtu. Mimi nasema mtu yeyote asijisikie mnyonge ndani ya nchi huru.
“Sitaonea wala kupendelea mtu. Mwenye haki atapata haki yake, ila ukija kwangu kutafuta haki uje na mikono misafi pia. Maana kuna wengine anakuja kwa kutegeshea tu, ukimwangalia unaona kabisa anajua hana haki, lakini anakutegeshea uteleze. Hapa ni umakini wa hali ya juu unahitajika,” Lukuvi ameliambia JAMHURI.
Amesema anakereka kuona Mtanzania mwenye haki anaporwa haki yake na amewaagiza maafisa ardhi na watendaji wote wa wizara yake kuhakikisha wanakuwa suluhisho la matatizo badala ya kukuza migogoro isiyo na tija kwenye ardhi.
Lukuvi ameongeza kuwa amepanga ratiba ya kutembelea kanda mbalimbali kutatua migogoro ya ardhi ambayo ni mingi mno nchini na inamkera.
Wakati Lukuvi akiendelea na kazi hiyo ya kusikiliza wananchi, Mkazi wa Vingunguti, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, Philipo Mpemba, na mke wake, Scolastina Beda, walimpa mshangao wa mwaka Lukuvi na maafisa wa wizara walioshiriki vikao hivyo.
Mpemba anadaiwa kumwambia Lukuvi kuwa yeye pamoja na baadhi ya mawaziri ni wala rushwa wakubwa na ndiyo waliochangia uwapo wa migogoro ya ardhi nchini ukiwamo mgogoro wa ardhi wa lililokuwa dampo la Vingunguti.
Akizungumza na JAMHURI, huku akiwa katika chumba maalum alichofungiwa kwa muda wizarani hapo baada ya kutoa kauli hiyo, Mpemba amesema Julai 11, mwaka huu alipigiwa simu na Msaidizi wa Waziri Lukuvi akimtaka afike wizarani siku ya Ijumaa kuonana na Waziri kwa ajili ya mazungumzo kuhusiana na mgogoro wa ardhi ya lililokuwa Dampo la Vingunguti.
Ameliambia JAMHURI, alifika wizarani saa 3:00 asubuhi na kuwa mtu wa kwanza kuitwa kuonana na waziri na baada ya kuingia katika chumba ambacho waziri pamoja na maofisa wengine wa wizara walikuwepo mazungumzo yalianza kwa kuulizwa maswali kuhusiana na barua kadhaa alizoziandika kwenda kwa Rais, Kamishna wa Ardhi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
“Waziri Lukuvi aliniuliza wewe ndiye Philipo, nikamwabia ndiyo, akasema umeniandikia barua nyingi sana ukapeleka Ikulu sasa Rais karudisha hapa nishughulikie na katika barua hizo umeshutumu sana kuhusu suala la rushwa, na kwamba nani ninayemhisi anakula rushwa na nikamtaja yeye (Lukuvi) na Waziri wa [wizara imehifadhiwa],” amesema Mpemba.
Baada ya kusema hivyo, aliwekwa chini ya ulinzi na kuona hivyo aliamua kumpigia simu Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro, ambayo ilipokewa na msaidizi aliyesema Sirro yupo Nairobi, nchini Kenya na kumweleza kuwa atamuunganisha na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala alifanyie kazi suala lake.
“Nililazimika kupiga simu kwa IGP kutokana na hali ambayo haikuwa nzuri katika chumba nilichofungiwa na mke wangu na baada ya muda RPC Ilala alimtuma Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OCCID), lakini walikutana na askari wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam na ofisa mmoja kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambao nao walifika hapo kufuatilia suala hilo.
“Baadaye nilichukuliwa na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Kati na kuanza kunihoji kwamba Waziri Lukuvi amelalamika kwamba nimemshutumu kwamba amepokea rushwa.
“Nimewaeleza polisi kuwa nina nyaraka zote na nimewaambia wafuatilie mawasiliano kati ya Lukuvi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene, na mwekezaji aliyepewa eneo la lililokuwa dampo la Vingunguti.
JAMHURI lilifika katika ofisi za Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO) na kukuta Mpemba akihojiwa na askari toka saa saa 6:00 mchana hadi 10:30 jioni alipoachiwa.
Askari aliyekuwa akimhoji alilieleza gazeti hili kuwa baada ya mahojiano hayo kukamilika wataendelea kuwahoji watu wengine zaidi kuhusiana na suala hili na uchunguzi ukikamilika hatua zinazopaswa kuchukuliwa zitaelezwa.
Majibu ya Waziri Lukuvi
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amekiri kwamba mwananchi huyo alifika katika ofisi yake kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na barua alizoziandika ikiwamo ya aliyoipeleka kwa Rais John Magufuli.
Amesema katika mazungumzo hayo, Mpemba aliwasutumu baadhi ya mawaziri kuhusika na rushwa kwenye mgogoro wa ardhi wa lililokuwa dampo la Vingunguti.
“Yeye (Philipo) kukaa kwenye hicho chumba saa moja na nusu inahusu nini? Hivyo nilimwambia hata kama amenishutum na mimi aende huko polisi akayaeleze vizuri maana ndiyo sehemu salama.
“Si mara ya kwanza kwa huyu mwananchi kuandika barua, ameshaandika barua zaidi ya 10. Hivyo nikaona njia ili kukomesha suala hili nimsaidie akataje wahusika kwenye vyombo husika anaodai wamepewa rushwa katika sakata hilo.
Barua zilizoandikwa na Mpemba ni zenye kumbukumbu namba PM/005/2017 ya Juni 7, mwaka huu aliyomwandikia Kamishna wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, PM/007/2017 aliyomwandikia Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na barua mbili alizoandika Februari 14, mwaka huu na Novemba 7, mwaka jana alizomwandikia Rais John Magufuli.
Mwananchi huyo amefika ofisini kwangu mara kadhaa na wakati mwingine alitaka kujifanya kama informer wangu, lakini nikamshtukia maana ana maneno mengi sana.
Lukuvi amesema; “Katika kikao hicho alieleza kuwa kuna ki-note kimeonekana Manispaa ya Ilala ambacho eti nilikiandika, jambo ambalo limenishangaza sana, maana mimi sina tabia ya kuandika vi-note, hasa katika masuala ya ardhi ambayo maamuzi mengi yanaamuliwa kwa vikao na maandiko rasmi.
“Ndiyo maana niliwaita polisi na Takukuru nataka yote aliyoyasema akataje wahusika kama ana ushahidi japo hata suala la hicho ki-note hakueleza kina maandishi gani,” amesema Lukuvi.
Historia ya dampo
Eneo la dampo la Vingunguti awali lilikuwa linamilikiwa na wananchi kwa hati ya kimila ambao walikuwa wamejenga nyumba za kuishi.
Wakati wananchi wakiendelea kuishi eneo hilo na kufanya shughuli zao, kulianza kutokea mmomonyoko wa dongo uliotokana na bonde la Mto Msimbazi kuwa na maji mengi na hivyo wananchi wakahama na eneo hilo Manispaa ya Ilala ikaanza kujaza udongo na taka ili kuzuia uharibifu usiendelee.
Mgogoro ulivyoanza
Mgogoro ulianza baada ya wananchi kuhamishwa katika eneo hilo na kujazwa udongo ili mmomonyoko usiendelee na baada ya mmomonyokio kwisha inadaiwa alijitokeza mfanyabiashara mmoja aliyetajwa kwa jina la Mohamed Kiluwa na kudai kuwa eneo hilo ni mali yake hali iliyozua mgogoro mkubwa.
Katika mgogoro huo ambao ulifika hadi mahakamani, Kiluwa alisema atawalipa fidia ya Sh 700,000 kila mmoja wananchi wote wanaostahili kama agizo la mahakama lilivyoelekeza.
Diwani mstaafu wa kata ya Segerea, Azurly Mwambagi, alisema katika mgogoro huo Kamati ya Fedha na Utawala Manispaa ya Ilala ilikataa pendekezo lililotolewa na Kamati ya Mipangomiji na Mazingira.
Mwambagi ambaye alikuwa diwani kipindi cha 2010-2015, anasema Kamati ya Mipango Miji na Mazingira ilitoa pendekezo la kutaka eneo la dampo hilo lipimwe viwanja.
Amesema Kamati ya Fedha na Utawala ambayo ipo juu kikanuni ilikataa kutokana na kuwepo kwa mgogoro wa wananchi waliokuwa wakidai walipwe fidia na Manispaa.
Mwambagi anasema sababu nyingine za kukataa pendekezo hilo ni baada ya kubainika kuwa kulikuwa na mpango uliokuwa umesukwa na baadhi ya watu wakiwamo viongozi kutaka kummilikisha mwekezaji eneo hilo kwa maslahi yao binafsi.
“Mimi nilikuwa mjumbe wa Kamati ya Fedha na Utawala. Tulilikataa pendekezo la Kamati ya Mipango Miji, sasa leo hii anapojitokeza mtu kwamba eneo hilo ni la urithi hivyo ni mali yake siyo kweli. Huku nikutaka kudhurumu haki za wanyonge,” amesema.
Akizungumza na JAMHURI, mfanyabiashara anayetuhumiwa kuwahonga viongozi, Mohamed Kilua, amesema yeye hajawahi kumhonga waziri yeyote labda kama huyo aliyetoa tuhuma hizo ana ushahidi.
“Nimuhonge waziri ili afanye nini? Waziri anahusika na nini? Anapoongea kitu mtu lazima uulize je, waziri anahusika na nini? Ni kama nani katika suala hilo?.
“Kimsingi hakuna mgogoro wowote eneo la Vingunguti kwa sababu eneo hilo ni mali yangu. Walikuwa wakiishi wazazi wangu miaka ya nyuma.
“Ninachokijua Philipo alikuwa kibarua wangu, ndiye alikuwa anaweka nguzo katika eneo la dampo vingunguti, lakini nikamfukuza kutokana na mwenendo wake usioridhisha. Hata viongozi wa Serikali ya Mtaa wanafahamu
“Kimsingi suala hili ni la kutengeneza wakati Philipo akiwa kibarua alifikia hatua ya kughushi nyaraka mbalimbali nikamfukuza na ningeweza hata kumfunga sababu nilikuwa na ushahidi lakini nikaamua kumwacha,” amesema Kilua.
Amesema anao ushahidi wa Mpemba kupokea malipo kutoka kwake kwa kazi ya kusimika nguzo za mipaka ya shamba kabla hajamfukuza kazi. Hata hivyo, Mpemba amesema katika maisha yake hajawahi kuajiriwa na huo ni uongo anaoutunga Kilua kuhalalisha hila zake.
Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum (ZCO), Camilius Wambura, amesema japo suala hilo analifahamu, lakini yeye siyo msemaji wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya hakupatikana kueleza suala hilo.
Takukuru wazungumza
Msemaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mussa Msalaba, alipoulizwa wamebaini nini baada ya kumhoji mwananchi huyo anasema suala hilo bado halifahamu kwa sababu alikuwa na majukum mengine.
“Suala hilo jibu sina kwa sasa hadi nifuatilie siku ya Jumatatu maana siyo rahisi kuwa na taarifa ya kila jambo hasa ikizingatiwa tuna idara nyingi,” amesema.
Na Thobias Mwanakatwe