Na Magrethy Katengu,JamuhuriMedia,Dar es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na uratibu William Lukuvi ameanza kufanya ziara yake kuvitembelea vyama vya siasa 19 vilivyosajiliwa ikiwa ni lengo kutambua shughuli zao wanazozifanya viongozi wa vyama hivyo sambamba na kuwahamasisha kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kuanza mwaka huu.
Amebainisha hayo Oktoba 7, 2024 Dar es Salaam katika ziara hiyo ambapo amesema akiwa kama Waziri wa ameanza ratiba yake kwa kuvitembelea vyama vyote 19 kabla ya uchaguzi wa Serikali za mitaa na leo amefanikiwa kutembelea vyama vinne ikiwemo Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA), ACT – Wazalendo, Chama Cha Kijamii (CCK) na Chama Cha United People Democratic Party (UPDP)
Sanjari na hayo amewasihi kama viongozi wa vyama wanajambo lolote ushauri wanaruhusiwa kufika ofisini na kutosubiri mpaka Mabaraza ya Kisiasa na amewasihi kudumisha upendo na kufata falsa ya 4R za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wanapoelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Nimeanza utaratibu huu mpya wa kuwafuata viongozi wa vyama vya siasa ofisini kwao badala ya kukutana nao kupitia mgongo wa msajili wa vyama vya siasa Jaji Fransc Mutungi hadi kutimiza lengo lake la kuwasikiliza maoni yao na ushauri wao ” amesema.
Hata hivyo Waziri Lukuvi amesema leo na kesho atafanikiwa kutembelea vyama 8 baada ziara ya kesho atasitisha kidogo ratiba hiyo kwa sababu kuna mkutano wa baraza la vyama vya siasa utakaofanyika Dodoma na yeye hana budi kuhudhuria .
Sambamba na hayo amesema mpaka sasa vyama vyote vinakwenda kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa hivyo amewasihi viongozi na wananchi wote kushiriki uchaguzi huo utakao anza mapema mwezi Novemba ili wapate fursa ya kupiga kura na kuchagua kiongozi wanaemtaka ambapo zoezi la uandikishaji litaanza tarehe 11hadi 20 mwezi huu.
Awali, kiongozi wa Chama Cha ACT -Wazalendo Dorothy Semu alitoa hoja yake Waziri alipofika Makao makuu ya Chama hiko Magomeni alisema wanapokwenda kuwahamasisha watu kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa wamekua wakipokea malalamiko kutoka kwa wananchi hao, ambapo wamesema wamekuwa wakipokea vitisho kutoka kwa watendaji na viongozi mbalimbali jambo ambalo limeanza kuwapa hofu juu uchaguzi huo.
Waziri Lukuvi akijibu hoja ya Kiongozi wa chama Cha ACT -Wazalendo Dorothy Semu amesema kuwa Rais Dkt Samia ameahidi uchaguzi utakaofanyika chini ya uongozi wake utakua wa huru na haki ambao utafuata kanuni, sheria na taratibu walizokubaliana, hivyo hakuna mwananchi atakaepata vitisho kutoka kwa viongozi na yeyote atakayetishiwa atoe taarifa katika mamlaka husika .
Mohammed Massoud Rashid ni Katibu Mkuu wa chama Cha Umma amesema watashiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za mitaa kwani wameona mabadiliko makubwa ukilingalisha walipotoka toka kisiasa na walipo, hivyo wanaendelea kuhamasisha wananchi wajitokeze wa wingi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama Cha Kijamii (CCK) David Daud Mwaijojewe amesema licha ya kujipanga vyema kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuhamasisha wananchi kushiriki lakini wanakabiliwa na ukosefu wa ruzuku hali inayopelekea kujiendesha kwa kusuasua.