Septemba 13, mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Vangimembe Lukuvi, alifanya mkutano na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam, ambapo alizungumzia tatizo la dawa za kulevya hapa nchini. kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, JAMHURI imeamua kuchapisha hotuba ya waziri huyo katika mkutano huo neno kwa neno kama ifuatavyo:
MAELEZO YA MAPENDEKEZO YA KUTUNGA SHERIA MPYA YA KUDHIBITI DAWA ZA KULEVYA NCHINI
Utangulizi
Nchi yetu inakabiliwa na tatizo la matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya. Tatizo hili huchangiwa na mambo mbalimbali yakiwemo; tamaa ya kupata utajiri wa haraka na mmomonyoko wa maadili.
Madhara ya dawa hizi ni makubwa ikiwa ni pamoja na kuathiri afya za watumiaji, ongezeko la uhalifu na magonjwa ambukizi kama vile homa ya ini, kifua kikuu na Ukimwi. Aidha, matumizi na biashara ya dawa za kulevya huathiri uchumi wa jamii na taifa kwa ujumla.
Jitihada zinazofanyika
Serikali imekuwa ikijitahidi kupambana na tatizo hili kwa muda mrefu sasa ikiwemo kufuta Sheria za kudhibiti dawa za kulevya zilizokuwa zikitumika tangu wakati wa ukoloni ambapo mwaka 1995 Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya [Sura 95] inayotumika hadi sasa ilitungwa.
Sheria hii ilianzisha Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa lengo la kuratibu na kusimamia udhibiti wa tatizo la dawa za kulevya nchini. Tume hii imekuwa ikishirikiana na vyombo mbalimbali vya dola vinavyojihusisha na udhibiti wa tatizo hili kama vile Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, Idara ya Uhamiaji, Idara ya Ushuru na Forodha na Asasi za Kiraia.
Mwaka 2006 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alianzisha Kikosi Kazi cha kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya ili kuongeza nguvu ya mapambano dhidi ya tatizo hili. Tangu kuanzishwa kwa Kikosi Kazi hiki kimefanya kazi nzuri sana ya kukamata wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kiasi kikubwa cha dawa hizi.
Mbali ya jitihada za ukamataji, matumizi ya dawa hizi yamekuwa yakidhibitiwa kwa kutoa elimu kwa jamii juu ya madawa ya kulevya pamoja na kuwapatia tiba waathirika wa dawa za kulevya.
Mafanikio ya jitihada hizo
Jitihada za kupambana na tatizo la dawa za kulevya nchini zimeleta mafanikio mbalimbali ambapo, katika kipindi cha mwaka 2008 hadi Machi 2013 jumla ya tani 208 za bangi zilikamatwa katika operesheni mbalimbali hapa nchini.
Pia katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2012, jumla ya ekari 504 na tani 3.2 za bangi ziliteketezwa. Aidha, katika kipindi cha mwaka 2008 hadi Machi 2013 jumla ya tani 44 za mirungi zilikamatwa. Halikadhalika, jumla ya kilo 728.3 za heroin zilikamatwa katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2012.
Kuanzia Januari hadi Machi 2013 jumla ya kilo 12 za heroin zilikamatwa. Jumla ya kilo 352.3 za cocaine zilikamatwa katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2012. Katika kipindi cha Jamuari hadi Machi 2013, kilo 3 za cocaine zilikamatwa.
Kuanzia mwaka 2009 hadi Septemba 7, 2013 watuhumiwa wa dawa za kulevya waliokamatwa katika baadhi ya mikoa ni kama ifuatavyo:
Watuhumiwa 149 walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Hata hivyo, ni kesi moja tu imemalizika ambapo washitakiwa watano walipatikana na hatia na kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 25 na kupigwa faini ya shilingi bilioni moja, na milioni 438 (1,438,364,400/=) kila mmoja, yaani (Jumla Tsh. 7,191,822,333/=). Aidha, kesi hii ndiyo iliyoamuriwa kwa washitakiwa kupewa adhabu kubwa na faini kubwa kuliko zote zilizowahi kuamuliwa.
Kesi kubwa za dawa za kulevya zilizopo mahakamani ambazo thamani yake ni zaidi ya Tsh. 10 milioni kuanzia mwaka 2010 ni kama ifuatavyo:
Kwa upande wa kupunguza matumizi ya dawa hizi, huduma za tiba zimekuwa zikitolewa katika hospitali za mikoa kwenye vitengo vya afya ya akili nchini. Kwa mfano mwaka 2012, jumla ya watumiaji wa dawa za kulevya 836 walipatiwa matibabu jijini Tanga, 130 mkoani Tabora, 422 mkoani Mwanza na 43 mkoani Iringa.
Pia, ujenzi wa kituo cha tiba unaendelea katika maeneo ya Itega mkoani Dodoma ambacho kitatoa huduma za matibabu na utengemao (urekebishaji tabia) kwa watumiajiza wa dawa kulevya.
Halikadhalika, huduma ya tiba kwa kutumia dawa aina ya methadone inaendelea kutolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mwananyamala jijini Dar es Salaam. Huduma kama hiyo inategemea kuanzishwa katika Hospitali ya Temeke mkoani Dar es Salaam.
Aidha, asasi za Kiraia zimeendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya kwa kuanzisha vituo ambapo watumiaji waliopata nafuu husaidia kuwapa mafunzo watumiaji wa dawa za kulevya ya jinsi ya kujiepusha na matumizi ya dawa hizo. Mfano wa Asasi hizi ni ‘Changamoto ni Matumaini’ iliyopo maeneo ya Boko na Pilimissanah Foundation iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam.
Pia, elimu juu ya athari za dawa za kulevya, imekuwa ikitolewa katika matukio maalum ya kitaifa. Kwa mfano, dawa za kulevya ni mojawapo ya ujumbe uliomo katika mbio za mwenge ambao hukimbizwa nchi nzima. Katika mbio hizi machapisho na makala zinazohusu athari za dawa za kulevya huwafikia wananchi katika ngazi zote.
Mapungufu katika utekelezaji wa sheria iliyopo
Pamoja na jitihada na mafanikio yaliyopatikana, dawa za kulevya bado ni tatizo linaloendelea kulikabili taifa letu ambapo Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya [Sura 95] haikidhi kikamilifu udhibiti wa tatizo la dawa za kulevya nchini. Hivyo, Serikali imeona kuwa kuna umuhimu wa kufuta Sheria hii na kutunga Sheria mpya.
Sheria iliyopo kuwa na mapungufu mengi ambayo yanakwamisha jitihada za udhibiti na kusababisha maamuzi katika baadhi ya kesi za dawa za kulevya kuacha hisia mbaya na kuleta utata katika jamii. Yafuatayo ni baadhi ya mapungufu katika sheria ya sasa:
Baadhi ya vifungu katika Sheria hii vinatoa adhabu isiyoendana na ukubwa wa makosa husika jambo linalochochea kuendelea kushamiri kwa biashara hii haramu. Mfano, kifungu cha 21 kinachohusu wafadhili wa biashara haramu ya dawa za kulevya kinatoa adhabu ndogo ambapo hawa ndiyo wanaomiliki biashara hii haramu na wanapaswa kudhibitiwa vikali. Adhabu iliyopo ni ya faini ya shilingi milioni kumi au kifungo cha maisha haitoshelezi. Adhabu hii inampa uhuru Jaji au Hakimu kutoa uamuzi wa kifungo au kumtoza faini mtuhumiwa kadiri atakavyoona inafaa.
Kifungu cha 12 cha Sheria iliyopo kinachohusu uzalishaji na biashara haramu ya dawa za kulevya za mashambani kama vile bangi na mirungi kinatoa adhabu ndogo ya faini ya shilingi milioni moja tatizo ambalo ni kubwa kutokana na kushamiri kwa kilimo cha bangi hapa nchini.
Suala la kumiliki/kukutwa na zana, mitambo, maabara au vifaa vya kutengenezea dawa za kulevya adhabu yake haitoshelezi.
Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya ilianzishwa kwa sheria iliyopo ili kusimamia mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya tu. Hata hivyo, Tume haikupewa mamlaka ya kutosha ya kuweza kutekeleza jukumu hilo kwa sababu haina mamlaka kisheria ya uchunguzi, ukamataji na upekuzi katika kesi zinazohusu dawa za kulevya. Mamlaka hayo vimepewa vyombo vingine vya dola kama Polisi, Uhamiaji na Idara ya Ushuru na Forodha.
Sheria iliyopo haibainishi wazi juu ya utaratibu mzuri wa kuwalinda watoa taarifa za siri kuhusiana na biashara ya dawa za kulevya. Aidha, haibainishi vizuri hatua za kuwachukulia watendaji wanaovujisha taarifa za siri kwa wahusika.
Sheria iliyopo inatumia thamani ya dawa za kulevya kama kigezo cha kutoa dhamana na adhabu na hivyo kuleta ushawishi kwa baadhi ya watu kujiingiza katika biashara hiyo haramu.
Vilevile, sheria inataka mshitakiwa wa kosa la dawa za kulevya zenye thamani inayozidi shilingi milioni kumi iliyothibitishwa na Kamishna asipewe dhamana, utolewaji wa hati ya Kamishna unategemea aina na uzito wa dawa iliyothibitishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali.
Kwa vile utambuzi wa dawa unahitaji uchunguzi wa kina wa kimaabara inakuwa siyo rahisi kupata hati zote mbili kabla ya kumfikisha mtuhumiwa mahakamani katika muda wa masaa 24 kama sheria inavyotaka. Kutokana na sababu hiyo kuna uwezekano wa mahakama kuwachia watuhumiwa kwa dhamana hata kama thamani ya dawa za kulevya ni shilingi milioni kumi au zaidi.
Makusudio ya Serikali katika kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya nchini:
Katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya, Serikali inakusudia kufanya mambo muhimu yafuatayo:
* Kutungwa kwa Sheria Mpya ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya ili kukabili kikamilifu na kuzuia mianya yote inayokwamisha jitihada za udhibiti wa taizo la dawa za kulevya nchini kwa kuwa vifungu vingi vya Sheria iliyopo vinaguswa kwa namna moja au nyingine na kuhitaji marekebisho kama vile kuondoa thamani ya dawa za kulevya na kutumia uzito, kuongezwa kwa adhabu katika vifungu vingi, chombo kipya kuwa na mamlaka kamili ya kuchunguza, kukamata na kupeleleza. Serikali imeona umuhimu wa kuifuta sheria ya sasa na kutunga nyingine ambayo itazingatia mabadiliko hayo makubwa yanayohitajika.
* Kuanzishwa kwa chombo Mahususi cha Kuzuia na Kupambana na tatizo la dawa za kulevya. Serikali inatarajia kukipa chombo hiki mamlaka ya kutosha ya kupambana na matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya.
* Serikali inakusudia kuanzisha Mahakama Maalum kwa ajili ya kushughulikia makosa ya dawa za kulevya ili kuharakisha usikilizwaji wake.
Ushirikishwaji wa wadau katika mchakato wa kutunga Sheria Mpya
Serikali imeamua kushirikisha wadau wengi kwa kuwa wana uelewa wa kutosha kuhusiana na tatizo la dawa hizi ili waweze kuichambua Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya na kutoa michango, maoni na ushauri utakaowezesha kupatikana kwa Sheria madhubuti itakayokidhi hali halisi ya tatizo na kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.
Hata hiyo, wadau wanaruhusiwa kutoa maoni yao ambayo hayamo kwenye Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya yenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa Sheria bora ya kuimarisha udhibiti wa tatizo hili.
Halikadhalika, Serikali inatoa mwaliko kwa wadau ambao hawatapata nakala ya Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya [Sura 95] (The Drugs and Prevention ofi Illicit Traffic in Drugs Act) pamoja na marekebisho ya Sheria hiyo ya mwaka 2012 (Miscellaneous Amendments) (No.2) Act, 2012) kutembelea tovuti ambayo ni HYPERLINK “http://www.pmo.go.tz/documents” www.pmo.go.tz/documents kuisoma Sheria hii na kutuma maoni yao kupitia kwenye mtandao ambao ni [email protected]