Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema mazingira ni suala mtambuka hivyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki kikamilifu katika kuyahifadhi.

Mhandisi Luhemeja amesema hayo wakati akizungumza na Watanzania wanaoshiriki Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaofanyika katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan.

Amesema kuwa sekta zote na mtu mmoja mmoja anapaswa kuguswa na kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuhifadhi mazingira wakati Ofisi ya Makamu wa Rais imepewa dhamana ya kusimamia.

Katibu Mkuu amewakumbusha Watanzania kuwa kupenda mazingira si lazima uwe na uwezo wa kifedha bali ni utashi wa mtu kwani anaweza kutumia muda katika kuhakikisha mazingira yanayomzunguka yanakuwa endelevu.

Aidha, Mhandisi Luhemeja ametoa wito kwa washiriki kuyachukua mazuri yote waliyoyapata wakati wa ushiriki wao kwenye COP29 mjini Baku hususan yanayohusu namna bora ya kuhifadhi mazingira na kuyatekeleza pindi warudipo Tanzania mara baada ya mkutano.

“Tunataka sisi sote tuliokuja hapa hili suala la hifadhi ya mazingira ambalo tunalishuhudia hapa kwa wenzetu tukalitekeleze nyumbani (Tanzania) tunaporudi,” amesisitiza Mhandisi Luhemeja.

Hivyo, ameongeza kuwa mara baada ya Mkutano wa COP29 kuna umuhimu wa kuandaa taarifa ya Ufuatiaji na Tathmini ya yale yote yalitekelezwa wakati wote wa mkutano huo mkubwa duniani.

Mkutano wa Katibu Mkuu Luhemeja na Watanzania wanaoshiriki COP29 umefanyika katika banda la Tanzania ambapo viongozi mbalimbali, wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara na Taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali wameshiriki.