Na Shaban Matutu, Dar es Salaam
Hatua ya kukwama kuuzwa mara tatu kwa nyumba mbili za mfanyabiashara, Said Lugumi, imeifanya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufikiria kuboresha sheria ili zitoe mwongozo kwa mali zilizokosa mteja mnadani.
Sababu ya kufikiria hilo imechangiwa na kukwama kwa mnada mara tatu wa kuuza nyumba hizo za Lugumi, ambao ulifanyika kwa mara ya kwanza Septemba 9, 2017. Mnada wa pili ulifanyika Novemba 9, 2017 na wa tatu ulifanyika Novemba 25, 2017.
Tangu kukwama kwa mnada huo mara ya mwisho Novemba 25, 2017 imepita miaka minne huku kodi iliyokuwa ikitarajiwa kufidiwa baada ya mnada ikiwa ni Sh bilioni 14 anazodaiwa Lugumi, ambazo alitakiwa kulipa.
Akizungumza na mwandishi aliyetaka kujua kinachoendelea kuhusu sakata hilo lililochukua miaka minne, Kamishna wa Kodi za Ndani, Hebert Kabyemela, amesema jambo hili la kuchelewa linachangiwa na utata uliomo kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato (Income Tax Act).
Kabyemela amesema sheria ya ‘Income Tax’ imekaa kimya, haielezi hatua ya kuchukua baada ya kukosekana mteja wa kununua bidhaa husika mnadani.
“Sheria hiyo ni tofauti na ile ya ‘Customs Law’ (Sheria ya Forodha). Hii ni rahisi, unaweza hata usipeleke mnadani ukaamua moja kwa moja kugawa kwa taasisi za serikali, lakini hii ya ‘Income Tax’ mambo ni tofauti, kwani inataka iwekwe mnadani hadi itakapopata wateja.
Ameongeza: “Nimejaribu kuangalia sheria nikabaini haikuona kama upo uwezekano wa kutokea mazingira ya kuwapo kwa kitu ambacho kitashindwa kuuzika pindi kitakapoingizwa mnadani. Sheria iliona hakuna kinachoweza kushindikana kuuzika mnadani, lakini inaonekana kukwama kwa nyumba hizi kumeonyesha zipo changamoto za kufanyia kazi.”
Akieleza kinachotakiwa kufanyika wakati wakiendelea kutafuta ufumbuzi wa sheria hiyo, amesema jambo la kufanya kwa sasa ni kuendelea kuziweka mnadani nyumba hizo hadi zitakapopata wateja.
Alipotakiwa kueleza kwa nini wao wamekaa muda mrefu bila kuendelea na mnada huo hadi kupatikana mteja, amesema: “Hapa katikati tulikuwa tukifikiria kuona namna ya kupendekeza jinsi ya kuiweka vizuri hiyo sheria pindi inapotokea kukwama kuuzika mnadani.”
Kabyemela ameongeza kuwa: “Kwa sasa ni sawa na ‘New experience’, ni vitu ambavyo vinatakiwa kukaa chini na kufikiria namna ya kuboresha sheria ili kukabiliana nayo pindi inapotokea changamoto kama hizo.”
Kampuni ya udalali yanena
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono, Scholastika Kevela, akizungumza na JAMHURI kuhusu uuzaji wa nyumba hizo amesema kazi yake iliishia pale alipokosa mteja mara ya tatu kwa nyumba hizo zilizoko Mbweni JKT, Wilaya ya Kinondoni.
Katika mnada huo kwenye nyumba ya kwanza walijitokeza watu watatu waliotaka kuinunua kwa Sh milioni 510, wakati nyingine, walijitokeza watu wawili waliotaka kuinunua kwa Sh milioni 650.
Lakini wote walikwama kununua kutokana na kutofikia kiwango kilichokuwa kimepangwa na serikali.
Kevela amesema viwango walivyokuwa wakifikia wateja havikuwa vikilingana na bei elekezi iliyopangwa na serikali ambayo hakuwa tayari kuiweka wazi kwa madai kuwa ilikuwa siri kati yake na serikali.
Majirani wanena
Jirani wa karibu na nyumba hizo Mbweni, Anna Ambwene, ameliambia JAMHURI kuwa tangu kukosekana kwa mnunuzi hajawahi kushuhudia mtu yeyote anayeishi au kufika na kufungua nyumba hizo.
“Kama unavyoona mwenyewe majani yamejaa katika nyumba hizi, hakuna usafi unaofanywa kutokana na kutokuwa na uangalizi,” amesema Ambwene.
Naye Hassan Mwelu, dereva wa bodaboda wa maeneo hayo amesema pamoja na Lugumi kuishi jirani na majengo hayo, hajapata kumuona akiingia kuyatazama au kuyafanyia usafi majengo yake.
“Sisi ndio tunapakia bodaboda eneo hili jirani, sijawahi kumuona jamaa (Lugumi) akifika eneo hili kutazama au mtu yeyote kufanya usafi,” amesema Mwelu.
Naye Joseph John, mmoja wa majirani anayeishi mtaa mmoja na Lugumi unaoitwa Magufuli huko Mbweni, amesema Lugumi hana tatizo na majirani zake ila anakiri kuwa kuonekana kwake si rahisi.
“Tangu ilipotokea taarifa ya kuuzwa kwa nyumba zake amekuwa haonekani na kwa sasa amepunguza ulinzi na msafara… kila asubuhi anapotoka kwanza lazima waanze vijana wake kutoka nje ya geti wakiongozwa na kiongozi wao anayeitwa ‘komandoo’ kuangalia usalama ndipo wanaruhusu gari kama mbili kutoka ambazo zina vioo vyeusi, zinazofanya kutojua yeye amepanda ipi,” amesema John.
Jirani mwingine anayeishi Mtaa wa Magufuli ni Aika Mushi, ambaye amesema maisha ya Lugumi hayapo kama ya watu wengine.
“Unajua baba yangu, jamaa huyu hatujawahi kuona hata mtoto au mke wake anaishi humo zaidi ya wafanyakazi wake. Kwa kifupi taarifa zake hazieleweki,” amesema Aika.
Dk. Shika aliyetikisa
Katika sakata la uuzwaji wa nyumba hizo jina la Dk. Louis Shika lilitokea kupata umaarufu kutokana na kuibuka mnadani na kujifanya anaweza kununua nyumba hizo za kifahari wakati hakuwa na fedha hizo.
Dk. Shika ambaye sasa ni marehemu, alitokea katika mnada wa pili uliofanyika Novemba 9, 2017 na alitangazwa kushinda mnada kwa kununua nyumba zote kwa gharama ya Sh bilioni 3.2.
Nyumba ya kwanza iliyoko Mbweni, Kitalu namba 57 yenye ukubwa wa mita za mraba 1,500 alitangaza kuinunua kwa Sh bilioni 1.1, iliyofuata kitalu namba 47 yenye ukubwa wa mita za mraba 1,500 ‘iliuzwa’ kwa Sh milioni 900.
Nyumba ya Upanga, iliyoko kitalu namba 701, yenye ukubwa wa mita za mraba 400, iliuzwa kwa Sh bilioni 1.2.
Hata hivyo, Dk. Shika alishindwa kulipa asilimia 25 ya fedha zote ambazo ni Sh milioni 800, hatua iliyosababisha akamatwe na kuwekwa ndani.
Aliwekwa ndani katika Kituo cha Polisi Salender, kisha kuhamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi, alikokaa kwa siku mbili kisha akaachiwa.
Mwandishi wa JAMHURI amemuuliza Mwanasheria, Apolinary Zambi, kuhusu tukio la mteja kutaja fedha asizokuwa nazo katika mnada kama alivyofanya Dk. Shika katika minada ya Lugumi, lakini baadaye akawa hana fedha za kulipa, amesema suala hilo linasimamiwa na Sheria ya Ardhi Namba 4 ya Mwaka 1999, Kifungu cha 52 na Kifungu cha 179.
Zambi amesema: “Sheria ya Ardhi namba 4 ya Mwaka 1999, Kifungu cha 52 na Kifungu cha 17 inazungumzia Kanuni za uendeshaji wa Minada na Zabuni. Kanuni hizo zilichapishwa kwenye Gazeti la Serikali namba 73 la tarehe 4/5/2001.
“Ukizisoma vizuri Kanuni hizo (za minada na zabuni) zinaeleza kwamba minada yote itaendeshwa kwa uwazi na yule ambaye atakuwa ametaja bei ya kununua ya juu zaidi ndiye atakayeshinda mnada husika.
“Ukiendelea kuzisoma zaidi Kanuni hizo zinaeleza kwamba mshindi wa mnada atalipa asilimia 25 ya bei ya kununua siku hiyo hiyo ya mnada. Kanuni ya 9 (3) inaeleza kwamba iwapo asilimia 25 hiyo haitalipwa siku hiyo ya mnada, mnada utarudiwa tena hadi mshindi atakapopatikana.
“Kama Shika alishindwa kulipa asilimia 25 ndani ya hiyo siku, alikuwa amejipokonya haki yake ya ushindi na mnada ulitakiwa kurudiwa upya na kumpata mshindi mwingine,” amesema mwanasheria huyo.
Mtu wa karibu na Dk. Shika
Catherine Kahabi, aliyekuwa Meneja wa Dk. Shika, akizungumzia sakata hilo amesema Dk. Shika ambaye alifariki dunia Agosti 23, 2020 kwa ugonjwa wa figo kufeli hakuwa na fedha za kununua nyumba hizo na ndiyo sababu ya kukwama kuzinunua kwani aliulaghai umma.