Na Angalieni Mpendu 0717/0787 113542
Lugha ni chombo cha mawasiliano, na kinaunganisha pande mbili katika mambo mbalimbali: kama vile elimu, mahusiano na kadhalika. Lugha pia ni mpangilio wa sauti na maneno unaoleta maana ambayo hutumika na watu kuanzia familia, taifa hadi mataifa.
Lugha ikitumika vizuri hujenga umoja wa kitaifa na diplomasia kati ya taifa na mataifa katika mambo ya mahusiano, uchumi. kilimo n.k. Ikitumika vibaya hubomoa umoja wa kitaifa na diplomasia ya kimataifa kwa maana ya kuvunja mwendelezo wa uhusiano baina ya taifa na mataifa.
Sauti na maneno hupangwa na mzungumzaji akiwa na nia yake mahususi kufikisha ujumbe wake kwa mtu anayemkusudia, ima kwa heri au kwa shari. Lugha kama chombo cha mawasiliano hufikisha ujumbe huo na majibu hurudishwa kwa lugha ile ile.
Kwa mfumo huu wa mawasiliano, mtumiaji wa lugha anawajibika kupokea majibu ya lugha aliyoitumia. Mtu au taifa lina dhima ya kuchunga lugha kabla haijatoka kinywani au kuandikwa kwa sababu lugha ni tamu na chungu inapotumika.
Tangu zama za mababu, lugha ilipewa staha katika matumizi kukwepa mvurugano. masemezano, mapigano kati ya mtu na mtu, kundi na kundi, taifa na taifa. Pale ilipokosa hifadhi ya staha makundi yote hayo yaliingia katika mifarakano, mapigano na vita.
Nazungumzia lugha kwa maana ya maneno na matumizi yake, na mtindo anaotumia mtu kujieleza. Wahenga wametuambia,” lugha nzuri humtoa nyoka pangoni.” Waimbaji wanasema, ” lugha tamu haishi hamu.” na Wanafasihi wanasema,” lugha ni pingamizi kubwa kwa watu duniani.”
Juma lililopita nilisema nafsi za watu zinasababisha dunia kuwaka moto. Leo narudia kusema nafsi inapotamka lugha chafu au tata inasababisha dunia kuonekana kama kwamba ina kwenda ovyo. Dunia kwenda ovyo ni hatari kwetu wanadamu na viumbe wote kuangamia.
Lugha zinazozungumzwa na baadhi ya viongozi wa nchi, wanasiasa, wanaharakati na viongozi wa madhehebu ya dini, zinadalilisha kuvuruga taratibu, kanuni na sheria kuvunja amani iliyowekwa kwa mujibu wa makubaliano kitaifa na kimataifa.
Hebu chungulia kule Korea Kaskazini na Urusi. Tazama yanayofanyika Syria. Sikiliza malalamiko ya Palestine na ona furaha ya Israel. Tega sikio kusikia lawama kutoka Afrika na kodolea maamuzi ya Marekani juu ya nchi nyingine. Ni ghasia tu.
Tanzania kwa namna fulani inasogezwa kwenye matumizi ya lugha isiyokifu haja, inayozungumzwa na baadhi ya viongozi wa siasa, wanaharakati, viongozi wa madhehebu ya dini na hata wasomi na wapigania haki za binadamu.
Baadhi ya lugha zinazotolewa na makundi haya hazikosoi bali zinalaumu. Hazitoi sifa au kasoro wala shukurani, kama vile hakuna kinachofanyika au kilipata kufanywa na mamlaka katika kuwapa maendeleo wananchi.
.
Tukitumia lugha kama burudiko la masikio na akili, au zoezi la ulimi na midomo kutamka maneno, iko siku tutaumia. Waswahili wanasema, “Mwanzo wa ngoma lele.” Naamini Watanzania hatutaki kucheza ngoma kama ile ya Libya au Congo- DRC.
Tukumbuke kuchagua lugha safi katika mazungumzo yetu kujenga nguvu ya hoja si hoja ya nguvu. Tanzania ipo na itakuwapo. Sisi leo tupo na kesho hatutakuwapo, vizazi vyetu ndivyo vitakuwapo na vitahitaji amani.
Hivi kuna mkono wa muungwana gani unaopenda kulambwa damu, sembuse kumwaga damu? Tujitathimini.