Na Angalieni Mpendu
Lugha yoyote ni chombo cha lazima kwa mawasiliano na uelewano kati ya wanadamu. Lugha ikitumika vizuri na kwa ufasaha katika kundi moja na jingine au Taifa moja na taifa jingine huleta tija, maendeleo na uhusiano mwema. Ikitumika vibaya hujenga chuki na mifarakano.
Unapoitathmini lugha katika matumizi mazuri huneemesha hekima, hujenga umoja na hudumisha amani, kuanzia familia hadi taifa. Mwanadamu au taifa lisilo na lugha nzuri na fasaha ni sawa sawa na mwanadamu aliyeshika kaa la moto. Ataungua tu.
Vile vile, malumbano ya shari, mapigano au vita vinavyotokea ndani ya nyumba ya mtu, nchi au taifa na taifa; iwe ya kijamii, kisiasa au kiuchumi inatokana na matumizi mabaya ya lugha katika kuwasilisha au kupokea hoja.
Lengo au shabaha ya hoja yoyote inapotolewa huwa ni ya kuanzisha, kurekebisha au kudumisha jambo fulani. Uwasilishaji wa hoja usipotolewa sawa sawa, bila ya hadhari na subira; ukweli hujenga kasheshe kwa mpokeaji na kurudisha hamaki kwa mtumaji wa hoja.
Hali hiyo inapotokea husababisha hekima kumezwa na hasira, umoja hutetereka na amani huvunjika. Hii ina maana hekima, umoja na amani kama nguzo katika taifa huvunjika. Ni vyema kukumbuka kuwa kubomoa ni rahisi na kujenga ni ngumu na ghali.
Nasisitiza kusema ni busara kwanza kambi ya msemaji kutumia hekima katika kuchagua neno la kusema. Pili, kuwa makini wakati wa kutamka na kuwasilisha hoja kwa mpokeaji, awe na kilio moyoni na furaha machoni.
Kadhalika, mpokeaji hana budi kupokea hoja iliyo moto au baridi ndani ya subira. Achambue kupata kiini cha ujumbe na kuwa shupavu kurudisha majibu. Na hapo malumbano ya hoja hunoga na kuwa tamu kama asali.
Uhenga huo unapopewa nafasi; mhemko, ushabiki na hasira havipati mchirizi wa kutiririsha hisia za fulani anaonewa, hapendwi au kuonewa gele. Aidha, fulani ni mbabe na hafai kwa jambo lolote la kuleta maendeleo ya wananchi.
Kwa hiyo, huyu wa kwanza anastahili kupata msukosuko na kipigo. Huyu wa pili anastahili kupewa kejeli na lugha chafu. Katika mazingira kama hayo maelewano huwa haba na utulivu tabu kupatikana tena. Yamkini wote wana hasara mbele ya wananchi.
Hali ilivyo sasa nchini ya kamatakamata kutokana na baadhi ya wananchi na viongozi kutumia lugha chafu, uchochezi, malumbano ya kitaaluma na kiuweledi na hatimaye kufikishana mbele ya vyombo vya sheria kutafuta nani ana haki mbele ya wananchi si mwenendo mzuri. Una dalili ya kuvunjika utulivu uliopo.
Huu si wakati wa kudhalilishana na kukebehiana; si wakati wa kubishana na kuoneshana ubabe; si wakati wa kuoneshana sura na kuficha kichogo na wala si muda wa kufurahia madhila yanayoundwa na matumizi ya lugha chafu. Si ustaarabu. Kila mwananchi anastahili heshima ya utu wake.
Ni busara na uungwana kuacha mwenendo huo na kupokea pendekezo lililotolewa wiki iliyopita na Mbunge wa Vunjo, Mheshimiwa James Mbatia, kama alivyokaririwa na chombo cha habari kimoja nchini (siyo JAMHURI).
Mbatia amependekeza kuwepo meza ya mazungumzo kati ya chama tawala CCM, vyama vya Upinzani na viongozi wa dini ili kurudisha utu na mshikamano. Anasema,
“Kitu kikubwa tunachojivunia Tanzania ni umoja wetu bila kujali tofauti za dini, kikabila au itikadi za vyama vya siasa na ukanda na ndiyo inayosababisha Tanzania itambuliwe kama kisiwa cha amani. Lakini viashiria hivyo vya kutoweka pamoja vinasambaratika kwa kasi kubwa.”
Nasema huu ni wakati wa kuelewana na kushauriana; kurekebishana na kukubaliana mambo ya kufanya. Ni wakati wa kutiana hamasa zaidi kufanya mabadiliko ya ukweli na kufanya kazi ya kujenga nchi ya viwanda kwa mtaji wa rasilimali tulizonazo.