Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, amesema wanaodhani atakipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye utangazaji matokeo ya Uchaguzi Mkuu, wanajidanganya.
Amesema yeye ni mtu mwenye msimamo usioyumba na hawezi kuzuia uamuzi wa watu kwenye sanduku la kura: “Sitayumba katika kutangaza mgombea anayevuna kura nyingi kwa sababu nitafanya kazi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria zinazosimamia uchaguzi badala ya dhana ya upendeleo.
“Suyumbi, sitayumba kwa sababu nafanya kazi kwa mujibu wa sheria,” amesema Jaji Lubuva katika mahojiano maalumu aliyofanya na JAMHURI jijini Dar es Salaam na kuongeza:
“Lengo letu ni kutangaza [matokeo] mapema iwezekanavyo. Ningependa sana nitangaze matokeo kabla ya siku tatu tukikamilisha. Inawezekana kupata matokeo kutoka kila kona. Mapema iwezekanavyo. Tutatoa matokeo kuepuka speculations (uvumi). Tukichelewa watu watasema ni kwanini? Mnaweza mkawa na sababu nyingine, lakini ni vema, lengo letu [litimie].
“Hakuna upendeleo. Na hata matokeo nitatangaza yule aliyeshinda baada ya kukamilisha taratibu. Katika hili sitayumba na nimepanga angalau nitangaze mapema matokeo.”
Anasema ameagiza kwa mujibu wa taratibu, kura zipigwe, zihesabiwe na matokeo yabandikwe nje ya kituo husika.
Baada ya hapo, wasimamizi wa Uchaguzi watatakiwa wapokee matokeo kutoka kweye vituo vyote kwa ajili ya kujumlisha kura na kuwatangaza washindi. Wakurugenzi hao wataruhusiwa kutangaza matokeo ya udiwani na ubunge.
“Yale ya urais atayatuma huku ambako kwa mujibu wa Katiba, huku ndiko tunakotangaza matokeo ya urais na kuchukua rekodi za matokeo mengine yote,” anasisitiza Jaji Lubuva.
Kambi ya upinzani imekuwa ikieleza wasiwasi kuwa huenda chama tawala kikaiba kura au akatangazwa mgombea ambaye hakushinda, madai yaliyokanushwa mara kadhaa na CCM wakisema wanao mtaji mkubwa wa wapigakura hivyo hawana sababu ya kuiba kura.
Hata hivyo, msimamo wa kauli ya chama tawala unatiwa doa na kauli iliyotolea na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye anayesema CCM itashinda hata kwa goli la mkono. Kauli hiyo imelaaniwa na wapenda haki wakisema ni maandalizi ya kuiba kura.
Jaji Lubuva anakiri kusikia taarifa kuwa baadhi ya watu kuwa na wasiwasi wa kutoona majina katika orodha ya waliosajiliwa akisema: “Wasiwe na wasiwasi. Wajue tu, kuwa fomu zote tunazo. Kwa hiyo tunachofanya tunarudi kwenye fomu na kuzicheki na kuona kwamba kila mtu jina lipo.
“Kwa hiyo wananchi wasiwe na wasiwasi lengo ni kuona kila mmoja yupo mle na ndivyo sheria ninavyosema. Kwa hivyo hakuna suala la kuchakachua. Najiuliza, wasiwasi huu unatoka wapi? Unachakachua, unachakachua vipi? Lengo letu sisi ni kuona kwamba kuna usahihi katika daftari.”
Jaji Lubuva amewatoa hofu wapigakura akisema Daftari la Kudumu la Wapigakura limeratibiwa vema kiasi cha kufikia malengo ya kuandikisha watu wanaokaribia milioni 23.78.
Anasema kwa takwimu hizo Tume imefanikiwa kiasi cha kutosha ikilinganishwa na Kenya ambao walikuwa na mashine 30,000 na wakaandikisha watu milioni 14.
“Sisi kwa mashine 8,000 na kuandikisha watu milioni 24, nadhani ni moja ya mambo yanayoniwezesha kusema kwamba tumejitahidi vya kutosha na tumefanikiwa vya kutosha katika zoezi hilo,” anasema.
Anasema kinachofanywa sasa na NEC ni kutimiza matakwa ya kisheria ya kupeleka daftari la awali kwa wasimamizi wa uchaguzi ambao ni Wakurugenzi katika Halmashauri wanaofanya kazi na wasaidizi wao katika kata.
“Sasa lengo la kupeleka huko ni kuona tu hawa ndio tulioandikisha na hatupeleki kila kituo. Tunapeleka na wao wanakagua na wakiishaangalia wanarudisha kwetu baada ya marekebisho na hatimaye tupate daftari la mwisho lenye taarifa sahihi,” anasema.
Anasema matatizo yaliyotokea Ghana na Kenya hayatokea Tanzania kwani walichofanya ni kutumia teknolojia ya BVR kuandikisha wapigakura tu, na si kufikia hatua ya kupiga kura kwa njia ya elektroniki ambayo kwa sasa inafanywa na Angola pekee barani Afrika.
Kuhusu baadhi ya wadau kuvunja ratiba ya mikutano ya kampeni, Jaji Lubuva akakazia akisema: “Watu wafuate ratiba kama tulivyotangaza. Tena hili nalikemea kweli, muda uliopangwa ufuatwe, kusiwe na kisingizio kwamba maadam fulani alichelewa kwa tarehe fulani na wewe uchelewe. Hii ni kwa wote,” anasema.
Anasema kwamba NEC inafarijika kuona kuna amani tangu kuanza kwa kampeni na kwamba dosari ni ya kupitiliza muda na anashukuru wadau, hususani wagombea na wafanyabiashara wameanza kufuata ratiba ya saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.
“Natambua kuna baadhi ya wengine walizidi muda. Si kwamba tuliwapa ruhusa. Hapana. Tunakemea hili. Siyo vizuri, lakini isiwe mfano wa watu kufanya makosa kama hayo kwa kulipa kisasi au kisingizio au chanzo cha wengine tuzidi hapo,” anasema.
Suala la uhamisho wa watumishi wa Tume yake, Jaji Lubuva anasema NEC haijatikiswa na kwamba watumishi wanahama kwa utaratibu wa kawaida, akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Malaba.
Anasema Malaba ni mchapakazi mzuri, waliyeteuliwa wote siku moja na alimpa baraka zote kwa kuwa alipanda ngazi kitaaluma.
“Niliona siyo uungwana kumkosesha ujaji kwa sababu za ukurugenzi wa Tume. Kupanda kwake ingekuwaje? Mimi mwenyewe nikasema Julius Malaba napenda awepo hapa, lakini nafasi aliyopata ya kupanda kitaaluma nikamwachia aende. Alikwenda kwa baraka zote za Tume,” anasema.
Watumishi wengine waliohamishwa, anasema ni uhamisho wa kawaida na kuongeza kuwa waliobaki pale amewatia moyo kufanya kazi kwa juhudi na wanaweza kufanya kazi popote.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa waliohamishwa ni Mkuu wa Idara ya Sera na Mipango, Eugenia Mpanduji aliyepelekwa Ofisi ya Rais Utumishi kama ilivyokuwa kwa Ruth Mashamu ambaye alikuwa Mkuu wa Idara ya Habari na Elimu; wakati Venosa Mkwizu aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Sheria amehamishiwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu.
Pia wamo Mhasibu Mkuu, Steven Darasia, ambaye amepelekwa Hazina; wakati Ofisa wa kutoa Elimu, Salvatory Alute yeye amepelekwa Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dodoma.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata zinasema kuhamishwa kwa watumishi hao kunahusishwa na ukaribu wao na chama kimoja cha siasa na mgombea urais, Edward Lowassa.
Hii ni wiki ya pili tangu kuanza rasmi kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika nchini kote Oktoba 25, mwaka huu. Mchuano mkali unaonekana upo kwa wagombea wa CCM dhidi ya wale wa vyama vya siasa vinavyoundwa Umoja wa Katiba (UKAWA). Wakati Ukawa wakiwakilishwa na Lowassa, CCM inaye Dk. John Magufuli.